GAZA: Israil yamtia nguvuni waziri mwengine wa Hamas. | Habari za Ulimwengu | DW | 26.05.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

GAZA: Israil yamtia nguvuni waziri mwengine wa Hamas.

Majeshi ya Israil yamemkamata waziri mwengine wa chama cha Hamas baada ya shambulio la mkesha wa kuamkia leo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Waziri wa afisi ya rais, Wafsi Qabha alikamatwa nyumbani kwake.

Wakati huo huo wanamgambo wa Kipalestina wameipa Israil muda wa saa 48 za kukubali kusitisha mapigano katika ukanda wa Gaza.

Mjumbe wa Rais Mahmoud Abbas aliyeshirika mazungumzo ya dharura pamoja na wanamgambo hao amesema makubaliano ya muda ni mwanzo wa hatua nyingine ya mwafaka wa kusitisha mapigano uliotangazwa na rais huyo wa Wapalestina pamoja na Waziri Mkuu wa Israil, Ehud Olmert mwezi Novemba mwaka uliopita.

Hata hivyo makundi ya wanamgambo yamekanusha taarifa hizo yakisema yanatathmini mapendekezo ya Rais Abbas ya kuweka amani Gaza kwa muda wa mwezi mmoja.

Jana wanamgambo wawili wa chama cha Hamas waliuawa baada ya gari lao kuvurumishiwa makombora katika ukanda wa Gaza.

Kufikia sasa watu zaidi ya arobaini wameuawa tangu mapigano yalipoongezeka siku kumi zilizopita.

Makombora zaidi ya mia moja na hamsini yamerushwa katika kipindi cha wiki mbili zilizopita hali ambayo imevuruga utulivu uliokuwepo.

Mapema juma hili, mwanamke mmoja raia wa Israil aliuawa katika mji wa Sderot baada ya shambulio la kombora.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com