1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaddafi aweza kubakia Libya akijiuzulu

20 Julai 2011

Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi anaweza kubakia Libya ikiwa atajiuzulu,amesema waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa katika kile kinachotazamwa kuwa ni jitahada mpya ya kutafuta suluhisho la kisiasa kwa mzozo wa Libya.

https://p.dw.com/p/RaqF
Former prime minister Alain Juppe speaks in the French parliament, Paris, Wednesday, 04 February 2004. Alain Juppe has rejected calls to step down as chief of France's governing party after his conviction for illicit party financing, and vowed to clear his name at an appeal later this year. Foto: WITT dpa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Alain JuppePicha: picture-alliance/dpa

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa, Alain Juppe, amesisitiza kuwa Kanali Gaddafi anaweza kubakia nchini Libya kwa sharti kuwa atajiuzulu. Amesema, kumalizika kwa vita vya Libya, kunategemea iwapo Gaddafi atangatuka madarakani kama mkuu wa majeshi na serikali. Leo wajumbe wawili wa Baraza la Mpito la taifa la Waasi wa Libya wanakutana na Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy mjini Paris. Ufaransa ilikuwa ya kwanza kulitambua baraza hilo na wa kwanza kufanya mashambulio ya anga dhidi ya vikosi vya Gaddafi, zilipoanza operesheni za kijeshi ambazo sasa, zinaongozwa na jumuiya ya kujihami ya NATO.

Kuhusu uwezekano wa kujadiliana na Gaddafi, Juppe amesema kwa hivi sasa hakuna mpango huo, bali mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa ndio aliepewa jukumu la kushughulikia mawasiliano kama hayo. Amesema suala sio iwapo Gaddafi ataondoka bali lini na vipi. Kwa upande mwingine, Kanali Gaddafi katika kanda ya sauti iliyotangazwa hiyo jana alikula kiapo, kupigana dhidi ya waasi na NATO. Amesema, yeye na mamilioni ya Walibya, watapigana kufa kupona, kutetea hadhi ya Walibya, pamoja na mafuta na utajiri wao. Amesema, hivyo ni vita walivyolazimishwa kupigana.

In this image made from Libyan TV, Libyan leader Moammar Gadhafi holds a meeting with tribal leaders from eastern Libya, in Tripoli, Libya, Wednesday, May 11, 2011. (AP Photo / Libyan TV via APTN) TV OUT LIBYA OUT
Kiongozi wa Libya, Muammar GaddafiPicha: dapd

Waasi wa Libya wanapigana tangu mwezi wa Februari katika jitahada ya kutaka kumtimua Gaddafi alie madarakani kwa miaka 42. Vikosi vya waasi vilivyodai hiyo jana kuudhibiti mji wa mafuta Brega, mashariki ya nchi, vinasema kuwa majeshi ya Gaddafi yanasukumwa nyuma. Wakati huo huo, duru za waasi zinasema kuwa vikosi vyao, vinakawia kuingia katika mji huo, kwa sababu ya mabomu mengi yaliyozikwa ardhini na majeshi ya Gaddafi.

Serikali ya Gaddafi ikiendelea kushinikizwa kidiplomasia, maafisa wa Marekani walikuwa na mkutano wa nadra pamoja na waakilishi wa serikali ya Libya mwishoni mwa wiki iliyopita. Urusi nayo ikiendelea na jitahada za upatanishi katika mgogoro wa Libya, hii leo inamkaribisha waziri wa mambo ya nje wa Libya Abdelati al-Obeidi. Yeye,ni afisa wa ngazi ya juu kabisa wa Gaddafi, kwenda Moscow tangu mzozo wa Libya kuzuka katikati ya mwezi wa Februari. Waziri huyo wa nje, atakuwa na mazungumzo pamoja na waziri mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov.

Mwandishi: MartinP/afpe,rtre,dpae

Mhariri:Abdul-Rahman