1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Gaddafi aendelea kung'ang'ania madaraka

24 Februari 2011

Utawala wa Gaddafi unaonekana kupoteza udhibiti wa sehemu kubwa mashariki mwa nchi hiyo, kufuatia mapinduzi yanayoendelea, huku mataifa ya magharibi yakijitayarisha kwa uhamiaji mkubwa wa watu kutoka taifa hilo.

https://p.dw.com/p/10OgC
Umwagikaji damu mkubwa umeshuhudiwa Libya.Picha: AP

Maelfu ya watu waling'ang'ana kuikimbia Libya, ambayo sehemu ya maeneo yake, yamedhibitiwa na upinzani huku maeneo mengine yakikumbwa na uhalifu.

Muammar al-Gaddafi Libyen Rede Ansprache
Kiongozi wa Libya Moammar Gaddafi.Picha: Libya State Television via APTN/AP/dapd

Milio ya risasi ilisikika mjini Tripoli hapo jana usiku, mashariki mwa vitongoji duni. Hii leo asubuhi mitaa katika mji mkuu huo haikuwa na watu.

Mojawapo ya wanawe saba wa Gaddafi, Saadi, hii leo ameliambia gazeti la Financial Times kuwa baada ya miongo minne chini ya utawala wa babake, huenda babake akageuka kuwa mshauri mkuu chini ya serikali mpya.

Gaddafi ageukwa

Wakati majenerali wakuu na makomredi wa kiongozi huyo kutoka mapinduzi waliofanya mnamo mwaka 1969, wakimpinga na kujiunga na mapinduzi yanayoendelea, upinzani unaonekana kuidhibiti pwani ya mashariki mwa nchi hiyo kutoka mpaka wa Misri kupitia miji ya Tobruk na Benghazi, yaliopata umaarufu kwa kuwa maeneo makuu ya mapigano katika vita vya pili vya dunia.

Waandishi habari waliwaona wapinzani wa utawala, wengi wao wakiwa wamejihami katika barabara kuu inayoambatana na pwani ya eneo hilo.

Naibu waziri wa mambo ya nje, Khalid Khaim amesema kundi la kigaidi la Al Qaeda limeunda makao katika eneo la Derna katikati mwa Tobruk na Benghazi, yanayoongozwa na aliyekuwa mfungwa wa jela la Guantanamo.

Hata hivyo wakaazi wa eneo hilo wamekanusha taarifa hizi, wakisema ni hatua ya serikali kujaribu kuiogopesha Ulaya.

Maandamano yaendelea

Na huku maandamano hayo yakiingia siku ya kumi hii leo, mwanawe Gaddafi, Said al Islam Gaddafi, amesisitiza kupitia kituo cha redio ya taifa, kuwa hakuna aliyejeruhiwa katika mashambulio ya ndege za kivita yaliozilenga ghala za silaha.

Libyen Saif al Islam Gadhafi in Tripolis
Saif al-Islam Gaddafi.Picha: dapd

Vyombo vya habari vya kiarabu vimeripoti mashambulio ya angani katika siku za hivi karibuni, dhidi ya kambi za kijeshi na ghala za silaha, yalionuiwa kuwazuia wapinzani wa serikali kuzifikia silaha.

Hata hivyo mashahidi waliripoti kuwa ndege za kivita pia ziliwashambuliwa waandamanaji.

Mamia ya waandamanaji wanaaminika kuuwawa na maafisa wa usalama wa Gaddafi.

Kamati ya serikali ya usalama jumla, hii leo imewaomba waandamanaji kuwasilisha silaha zao na imesema itatowa zawadi kwa wale watakao toa taarifa kuhusu viongozi wa maandamano hayo.

Maafisa wa usalama nchini humo wamekuwa wakifanya misako dhidi ya wapinzani na mapigano yakienea katika mji mkuu Tripoli.

Mwandishi Maryam Abdalla/RTRE/DPAE/AFPE
Mhariri: Josephat Charo