1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Finali ya kombe la Afrika jumapili hii:

8 Februari 2008

Finali ya Kombe la 26 la Afrika itakua kati ya mabingwa Misri na simba wa nyika Kamerun.

https://p.dw.com/p/D4LA

Finali ya Kombe la 26 la Afrika keshokutwa jumapili mjini Accra,Ghana, itakua kati ya mabingwa watetezi Misri na simba wa nyika-Kamerun.Ni marudio ya mpambano wao wa kufungua dimba katika kundi lao pale Misri ilipowazaba simba wa nyika mabao 4-2. Misri ilizikata jana pembe za Tembo wa Ivory Coast kwa mabao 4:1 wakati simba wa nyika Kamerun,walizima kelele za wenyeji Black Stars-Ghana kwa bao 1:0.

Kesho jumamosi,Ghana na Ivory Coast zinatakutana kuania taji la nafasi ya tatu na sherehe zote zilizopangwa na waghana mjini Accra,Kumasi Sekondi na Tamale jumapili hii kusherehekea ushindi zimevunjwa.

Mafirauni wa Misri, waliwachimbia jana kaburi Tembo wa Corte d’Iviore na kuwazika mjini KUmasi, baada ya kutekleteza ndoto za akina Didier Drogba na Abdelkadir Keita za kurudi na kombe Abidjan .

Mabao 2 kila dakika 5 za kipindi cha pili aliopachika Amr Zaki yalivunja miguu ya Tembo ambako kwa tafsiri yoyote ya uchambuzi wa dimba, walizidiwa mbinu na Hassan Shehata-kocha wa mafirauni.

Abdelkader keita,akipigana kufa-kupona kuwafufua tembo kutoka kaburi waliochimbiwa na Zaki,aliutandika mkwaju mkali na maridadi ajabu ambae hata kipa maridadi kabisa wa Misri Essam Al Hadari hakuona.Al Hadari-alikua hatari kweli katika lango la Misri,kwani bila yeye,pengine mpambano huu ungemalizika vyengine.Aliokoa mabao 2 ya kichwa ya Drogba yalioelekea kimiyani.

Kwahivyo, baada ya Simba wa nyika kuilaza Ghana jana kwa bao 1:0,timu 2 bora kabisa katika historia ya kombe la Afrika-Misri na Kamerun zina miadi jumapili hii mjini Accra tena chini ya wiki 3 tu tangu zilipokumbana

Wakati Misri wataania jumapili hii kombe lao la 6,wasisahau jambo moja:Simba wa nyika wamelazwa mara i tu katika finali ya kombe la Afrika pale timu hizi mbili zilipokutana katika finali ya 1986 mjini cairo.Misri,kama katika kombe lililopita ilipoitoa Cortte d’Iviore, ilitwaa kombe kupitia changamoto za mikwaju ya penalty.Kamerun katika finali ya jumapili itabidi kujifunza madhambi iliofanya wiki 3 nyuma ilipokomewa na Misri 4:2.