1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Federer abanduliwa na chipukizi Miami Open

26 Machi 2018

Kinyang'anyiro cha Miami Open kinaendelea huko Marekani. Mchezaji nambari moja duniani Roger Federer alishangazwa na Muaustralia Thanasi Kokkinakis.

https://p.dw.com/p/2v204
Roger Federer Tennis
Picha: Getty Images/A. Bello

Federer alibanduliwa kwenye raundi ya pili aliposhindwa kwa seti tatu za 3-6 6-3 7-6.

Kokkinakis mwenye umri wa miaka 21 na ambaye anaorodheshwa katika nafasi ya 175 duniani anasema bado haamini kama alimshinda bingwa huyo.

"Ni ushindi ambao sikuutarajia, nimefanya mazoezi naye mara nyingi na nimekuwa nikijifunza mengi kutoka kwake kwa kuwa bila shaka ni kielelezo chema kwa mchezo wa tennis," alisema Kokkinakis. "Amenialika Dubai mara kadhaa kwa mazoezi kwa hiyo niliyachukua machache niliyojifunza kutoka kwake na nikacheza mchezo wangu na nikashinda," aliongeza mchezaji huyo.

UK Tennis - ATP World Tour Finals | Dimitrov gegen Goffin
Mchezaji Tennis wa Bulgaria Grigor DimitrovPicha: Reuters/T. O'Brien

Federer baada ya mechi hiyo alisema tu kwamba bahati haikuwa upande wake na kila kitu kilikoseka kutoka mwanzo wa mechi.

"Ni jambo la kuvunja moyo sana. Sijui ni kwanini sikuweza kufika katika kiwango ambacho kingenifurahisha leo lakini wakati mwengine kunakuwa na mechi kama hizi ambapo kuna wakati unazishinda ila leo sikuwezakufanya hivyo," alisema Federer.

Mchezaji mwengine wa hadhi ya juu aliyebwagwa ni Grigor Dimitrov wa Bulgaria ambaye alibanduliwa na Jeremy Chardy wa Ufaransa kwa seti mbili za 6-2 6-2.

Mwandishi: Jacob Safari/DPAE/Reuters/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman