1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU kuichukulia hatua za kinidhamu Urusi

Grace Kabogo
23 Machi 2018

Nchi wanachama za Umoja wa Ulaya zimekubaliana kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya Urusi katika siku zijazo, kutokana na kuhusika kwake katika shambulizi la sumu dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi nchini Uingereza.

https://p.dw.com/p/2urtq
Belgien - EU-Gipfel Angela Merkel
Picha: Getty Images/J. Taylor

Akizungumza leo mjini Brussels, Ubelgiji Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron amesema nchi yake pamoja na Ujerumani zitakuwa miongoni mwa nchi zitakazochukua hatua ambazo viongozi wengine wamesema huenda zikajumuisha kufukuzwa kwa maafisa wa Urusi na uwezekano wa hatua nyingine za kulipiza kisasi. Macron alikuwa akizungumza pembeni ya Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel.

Katika mkutano wao wa kilele, viongozi hao jana walikubaliana kuwa Urusi inahusika na shambulizi dhidi ya Sergei Skripal pamoja na binti yake. Afisa mmoja anayefatilia mazungumzo hayo, amesema kiwango cha hatua hizo katika wiki zijazo, kinaweza kuwa cha kushangaza. Amesema hakuna mazungumzo kuhusu vikwazo vya kiuchumi, ambavyo utekelezaji wake umewahi kuugawa Umoja wa Ulaya katika kipindi cha nyuma.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Czech, Andrej Babis amesema anafikiria kutangaza kuwafukuza maafisa kadhaa siku ya Jumatatu. Naye Rais wa Lithuania, Dadlia Grybauskaite amesema yuko tayari kuwafukuza wapelelezi wa Urusi ambao amesema shughuli zao ni hatari. Rais wa Romania, Klaus Iohannis amesisitiza kuwa serikali za kitaifa zinataka kuendeleza udhibiti wa taarifa katika eneo ambako wanalinda uhuru wao.

Hata hivyo, Urusi leo imeyaelezea madai ya Umoja wa Ulaya kama yasiyo za msingi na imeukosoa umoja huo kwa kuendeleza kampeni za chuki za kuipinga Urusi iliyoanzishwa na Uingereza pamoja na washirika wake.

Theresa May
Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa MayPicha: picture-alliance/empics/S. Rousseau/PA Wire

Ama kwa upande mwingine, Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May amepongeza hatua ya viongozi wa Umoja wa Ulaya kuidhinisha kipindi cha mpito ili kuongeza uanachama wa Uingereza katika soko la pamoja la Umoja wa Ulaya baada ya nchi hiyo kujiondoa kwenye umoja huo, huku akiwataka wawe na nguvu mpya katika mazungumzo yanayokuja ya biashara.

''Hii itawahakikishia watu na wafanyabiashara, itawapa ufafanuzi wa kupanga mustakabali wao na kuhakikisha kwamba watafanya marekebisho mara moja, patakuwa na nafasi moja ambapo tutaingia katika uhusiano na Umoja wa Ulaya katika siku zijazo,'' alisema May.

May amesema anaamini hatua hiyo itakuwa kwa maslahi ya Uingereza na Umoja wa Ulaya katika kufikia makubaliano. Pia amepongeza kuidhinishwa kwa mwongozo wa mazungumzo ya Brexit kuhusu mustakabali wa uhusiano kati ya Uingereza na Umoja wa Ulaya.

Wakati huo huo, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker, amesema leo kuwa tarehe iliyowekwa na Marekani ya Mei Mosi kuhitimisha majadiliano na umoja huo katika kupata msamaha wa kudumu kutokana na hatua ya Marekani kutoza ushuru wa chuma cha pua na aluminium inayoingizwa nchini humo kuwa ni jambo lisilowezekana.

Rais wa Marekani, Donald Trump anapanga kutoza ushuru wa asilimia 25 katika chuma cha pua kinachoingizwa nchini humo pamoja na asilimia 10 katika aluminium.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP, Reuters
Mhariri: Josephat Charo