Ethiopia yawaruhusu wafanyakazi wa kiutu kuingia Tigray | Matukio ya Afrika | DW | 09.02.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Ethiopia yawaruhusu wafanyakazi wa kiutu kuingia Tigray

Serikali ya Ethiopia imeyaruhusu mashirika ya Umoja wa Mataifa kuwatuma wafanyakazi zaidi wa misaada, katika mkoa uliokumbwa na machafuko wa Tigray.

Serikali ya Ethiopia imeyaruhusu mashirika ya Umoja wa Mataifa kuwatuma wafanyakazi zaidi wa misaada, katika mkoa uliokumbwa na machafuko wa Tigray. Umoja wa Mataifa unadai kuwa mkoa huo unakabiliwa na kitisho cha njaa na sehemu kubwa ya mkoa huo imekuwa ngumu kufikiwa na wafanyakazi wa kutoa misaada ya kibinadamu. 

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema makubaliano hayo ni hatua muhimu kuelekea uhakikisho kwamba wafanyakazi wa kutoa huduma za kiutu mkoani Tigray wataweza kusambaza misaada inayohitajika. Ripoti iliyotolewa wiki iliyopita ilisema kuwa maisha ya raia mkoani Tigray imekuwa ya kutisha sana tangu mapigano yalipozuka mwezi Novemba baina ya vikosi vya serikali ya Ethiopia na vile vya mkoa wa Tigray.

Serikali inadai kwamba zaidi ya watu milioni moja katika mkoa huo wameweza kufikiwa na misaada, ingawa wafanyakazi wa mashirika ya kiutu wanaripoti tofauti.

Mawasiliano magumu mkoani Tigray

Wanajeshi wa Ethiopia wakielekea mkoa wa Tigray

Wanajeshi wa Ethiopia wakielekea mkoa wa Tigray

Huku mapigano yakiingia mwezi wake wa nne, shikinizo za kimataifa zimeongezeka dhidi ya Ethiopia,nchi ya pili yenye watu wengi barani Afrika, ili kuwaruhusu wafanyakazi wa kutoa misaada, waandishi habari na wataalamu wa haki za binadamu kuwasili jimboni Tigray.

Hivi sasa mawasiliano ni magumu na ni taarifa chache kabisa zinazojitokeza kuhusu hali halisi ya wakaazi wapatao milioni 6 wa jimbo hilo.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephan Dujarric alisisitizia ahadi nzuri baina ya serkali ya Ethiopia na maafisa wa Umoja wa Mataifa, akiwemo mkuu wa shirika la Mpango wa Chakula Dunia, David Beasley ambaye amehitimisha ziara yake nchini Ethiopia.

Beasly amesema kwamba shirika la WFP lilikubali ombi la serikali ya Ethiopia la kuwaunga mkono viongozi wa serikali na mashirika ya misaada kwa ajili ya kusafirisha misaada kwenye jimbo la Tigray.

Pande hizo mbili zimekubalina pia kuwapelekea misaada watu wapatao milioni moja walioko kwenye jimbo hilo.

Dujarric amesema kwamba wafanyakazi 60 wa mashirika ya kiutu walioko mjini Addis Ababa,wamesubiri kwa hamu ridhaa kutoka kwa serikali ili kupeleka misaada jimboni Tigray.

Ukiukwaji wa haki za binadamu?

Ripoti ya shirika la kiutu la kupambana na njaa, linalohudumiwa na Marekani, inaonyesha kwamba familia nyingi hazina chakula au zinaweza kukosa chakula mnamo kipindi cha miezi miwili ijayo. Ripoti hiyo imesema kwamba huduma za afya haziwafikii walio wengi kwenye jimbo la Tigray.

Kwenye taarifa nyingine tofauti, Alice Wairimu Nderitu, mshauri maalumu waUmoja wa Mataifakwa kupinga mauwaji ya kimbari, amesema alipokea taarifa za umakini kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye jimbo la Tigray, yakiwemo mauwaji, ubakaji na uporaji.