1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan, Putin na Rouhani wakutana kuijadili Syria

Amina Mjahid16 Septemba 2019

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amewakaribisha wenzake wa Iran na Urusi katika mkutano wao wa hivi karibuni wa kujadili mgogoro wa Syria kipaumbele kikiwa shinikizo la serikali dhidi ya ngome ya waasi mkoani Idlib

https://p.dw.com/p/3PgWJ
Russland Iran Türkei Erdogan Putin Rohani Sotschi
Picha: Reuters/S. Chirikov

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amewakaribisha wenzake wa Iran na Urusi katika mkutano wao wa hivi karibuni wa kujadili mgogoro wa Syria huku kipaumbele kikiwa shinikizo la serikali mjini Damascus dhidi ya ngome ya mwisho ya waasi mkoani Idlib.

Rais Vladimir Putin na Hassan Rouhani wamekutana na rais wa Uturuki Tayyip Erdogan katika mji mkuu wa Uturuki Ankara kwa mkutano wao wa tano tangu mwaka 2017 kujadili mgogoro wa Syria. Iran na Urusi wamekuwa waungaji mkono wakubwa wa Rais wa Syria Bashar al Assad huku Uturuki ikitaka rais huyo kuondolewa madarakani na kuwaunga mkono wapiganaji wa upinzani.

Lakini wakati nafasi ya rais Assad ikionekana kuwa thabiti msimamo wa Uturuki umebadilika na sasa inajaribu kuzuwia wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Idlib Kaskazini Magharibi mwa Syria. Uturuki ina wasiwasi wa vikosi vya serikali kusonga mbele katika eneo hilo. Vikosi hivyo vinaungwa mkono na jeshi la angani la Urusi licha ya uwepo wa makubaliano kadhaa ya kusitisha mapigano.

Uturuki ina vituo 12 vya uangalizi mkoani Idlib, kuhakikisha vikosi vya kijeshi havifikii maeneo kusikoruhusiwa mapigano, ikiwa ni sehemu ya makubaliano yaliofikiwa mwaka mmoja uliyopita kati yake na Urusi ili kuzuwia mgogoro huo kupanuka zaidi. Lakini vituo hivyo vinazidi kuwa hatarini kufuatia kusogea kwa vikosi vya serikali mkoani Idlib.

Mashambulizi ya anga yazidi kurindima licha ya makubaliano ya kuyasitisha

Mashambulio ya angani kutoka Urusi yameendelea mkoani humo licha ya kuwepo makubaliano hayo yaliofikiwa Agosti 31. Mshauri wa Ikulu ya Urusi, Kremlin Yuri Ushakov amesema idadi kubwa ya magaidi bado wapo katika eneo hilo na wapiganaji wanaendelea kushambulia maeneo yanayoshikiliwa na serikali.

Russland Moskau Treffen Wladimir Putin und Tayyip Erdogan
Rais wa Uturuki Recep Tayyip ErdoganPicha: Reuters/Kremlin/A. Nikolsky

Duru kutoka kwa rais wa Uturuki zinasema viongozi hao watatu watajadili matukio ya hivi karibuni katika mgogoro huo wa Syria, pamoja na kuhakikisha mikakati ya wakimbizi wanaotaka kurejea kwa hiari na kujadili pia hatua za pamoja za kuchukuliwa kukiwa na nia ya kupata suluhu ya kisiasa katika mgogoro huo wa zaidi ya miaka mitano.

Kulingana na mchambuzi wa taasisi ya kimataifa ya kutatua migogoro Dareen Khalifa suluhu hiyo ya kisiasa ikipatikana itampa Putin ushindi wa kisiasa  kuongezea katika ushindi wa majeshi yake. Lakini amesema matarajio hayo ni madogo sana.

Iran imekuwa mdau muhimu katika uwanja wa mapambano nchini Syria, lakini imekuwa kimya katika miezi ya hivi karibuni, ikiweka kipaumbele katika kuzizuia Israel na Marekani kuingia katika mzozo huo.