1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Erdogan asema EU itakwamisha kujiunga kwa Ukraine, Moldova

Iddi Ssessanga
19 Desemba 2023

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema Umoja wa Ulaya utazikwamisha Ukraine na Moldova kujiunga na kanda hiyo, na kuongeza kuwa Ankara ilipata haki ya kiunga muda mrefu lakini inasubirishwa kwa sababu za kisiasa.

https://p.dw.com/p/4aLh3
Hungary | Waziri Mkuu wa Hungary Orban na rais wa Uturuki Erdogan
Rais Erdogan akipeana mkono na Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban baada ya kushaini mkataba wa ushirikiano mjini Budapest, Hungary, Desemba 18,2023. Picha: Denes Erdos/AP Photo/picture alliance

Viongozi wa Umoja wa Ulaya walikubaliana wiki iliyopita kuanzisha mazungumzo na Ukraine hata kama inaendelea kupambana na uvamizi wa Urusi, huku pia wakianza mazungumzo na Moldova. Lakini umoja huo haukuweza kukubaliana juu ya msaada wa kifedha wa euro bilioni 50 kwa Kyiv kutokana na upinzani kutoka Hungary.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy alipongeza hatua hiyo kama "ushindi" kwa Ukraine na bara la Ulaya.

Akizungumza na waandishi wa habari akiwa safarini kutokea Hungary, Erdogan alisema Uturuki, ambayo imekuwa mgombea wa Umoja wa Ulaya tangu 2005, ilipata haki ya kujiunga na umoja huo kwa muda mrefu lakini imekwama kutokana na kile alichokiita vikwazo vya kisiasa.

Soma pia: Erdogan: Uturuki inaweza kusitisha juhudi za kujiunga na EU

"Kuwapa hadhi ya mgombea haimaanishi kuwa watakuwa wanachama wa EU. Mchakato utaanza nao, watakwama pia. Hakuna kati ya nchi hizo inafana na Uturuki," Erdogan alinukuliwa na ofisi yake akisema yake.

"Ni makosa kwa Uturuki, ambayo iko tayari zaidi kujiunga na EU kuliko baadhi ya nchi wanachama, kuwekwa mlangoni kwa miaka mingi kutokana na vikwazo vya kisiasa," aliongeza.

Volodymyr Zelenskiy
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesifu hatua ya Umoja wa Ulaya kuanzisha mazungumzo ya uanachama na nchi yake, akiyataja kuwa ushidni kwa Ukraine na Ulaya.Picha: AFP/Getty Images

Haki ya muda mrefu ya Uturuki

Jitihada za Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya zimesitishwa kwa miaka mingi kutokana na wasiwasi wa Umoja wa Ulaya juu ya rekodi ya Uturuki kuhusu haki za binadamu na tofauti kuhusu sera za kikanda, hasa eneo la mashariki mwa Mediterania na kisiwa chenye mgawanyiko wa kikabila cha Cyprus. Umoja huo unategemea msaada wa Uturuki, ambayo ni mwanachama wa NATO, hasa juu ya uhamiaji.

Ingawa uanachama unaweza kuchukua miaka mingi kupatikana, uamuzi uliotolewa katika mkutano wa kilele mjini Brussels unaipeleka Ukraine hatua karibu na lengo lake la kimkakati la muda mrefu la kujiekeza upande wa Magharibi na kujikomboa kutoka kwenye mzunguko wa Moscow.

Soma pia: Umoja wa Ulaya wasema umebaki na wasiwasi juu ya Uturuki

Erdogan alisema uwezo wa "kimkakati na kiuchumi" wa Uturuki kwa muda mrefu umeipatia haki ya kujiunga na umoja huo - ambao Ankara inasema ni lengo la kimkakati - na akaongeza kuwa maendeleo yanaweza kuonekana katika mchakato huu wakati wa muhula wa urais wa Hungary, ambayo Uturuki ina mahusiano mema nayo.

"Umoja wa Ulaya unahitaji kujirudi kutokana na kosa hilo sasa," alisema Erdogan kwa mujibu wa ofisi yake.