Eliud Kipchoge ashinda London Marathon
23 Aprili 2018Bingwa wa Olimpiki Eliud Kipchoge ameshinda taji lake la tatu la mbio ndefu marathon mjini London jana Jumapili na kukamilisha ushindi mara mbili wa Wakenya baada ya Vivian Cheruiyot kushinda mbio hizo kwa upande wa wanawake.
Kipchoge mwenye umri wa miaka 33, alimshinda Muithiopia Tola Shura pamoja na Mo Farah wa Uingereza na kushinda mbio zake za tatu za London Marathon kwa kutumia muda wa masaa 2 dakika 4 na sekunde 17, akimaliza zaidi ya nusu dakika mbele ya Kitata na Mo Farah akiwa wa tatu kwa kutumia masaa 2 dakika 21 na sekunde 40.
"Hii ni siku kubwa kwangu. Kushinda London Marathon na mashindano ya dunia. Ni mkusanyiko wa mataji mawili. Najisikia vizuri sana."
Nayo kamati ya kimataifa ya Olimpiki IOC leo imewataka viongozi wa mji wa Tokyo, ambao ndio utakuwa mji utakaotayarisha mashindano ya mwaka 2020 ya olimiki kujitayarisha kwa uchunguzi zaidi baada ya mafanikio makubwa ya mashindano ya majira ya baridi yaliyofanyika mjini Pyeongchang Korea kusini.
Wakati wa mradi wa mapitio wa siku mbili kwa ajili ya olimpiki ya mwaka 2020, makamu wa rais wa IOC John Coates aliweka mbinyo kwa Tokyo kutayarisha mashindano yenye mafanikio katika muda wa miaka miwili kuanzia sasa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre
Mhariri: Yusuf , Saumu