Elimu kwa wote | Masuala ya Jamii | DW | 25.06.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Elimu kwa wote

Watoto wote wanasoma bure nchini Kenya. Baadae waliofanya vyema zaidi hupatiwa msaada wa fedha kuendelea na masomo. Lakini watoto wa familia zinazojimudu tu ndio wenye nafasi nzuri zaidi ya kupata maksi nzuri.

default

Shule ya Ngong karibu na Nairobi nchini Kenia

Watoto na vijana kwa pamoja wanafikia nusu ya wakaazi jumla wa Kenya. Wakaazi wengi wa Kenya ni vijana na kwa kiwango cha wastani kila mwanamke mmoja anazaa watoto wanne.Wengi kati ya watoto hao wanaacha kwenda katika shule hizo za serikali "ambazo hazihitaji kulipiwa" hata kabla ya kuingia darasa la nane, kwasababu shuleni watu wanahitaji sare, viatu, vitabu, kalamu na  madaftari- na kwa familia nyingi vitu hivyo ni ghali. Shule za serikali zimejazana na kila mwalimu mmoja ambae halipwi vizuri anabidi kuwasomesha watoto 40 au zaidi.

Hakuna madawati ya kuwatosheleza wanafunzi wote shuleni.Vitabu au ramani hakuna, na sakafu mara nyingi itakuwa ni ya udongo mtupu.

Badala yake shule za kibinafsi ni ghali, lakini ni bora zaidi. Waalimu katika shule hizo wanalipwa vizuri na wameelimika vizuri zaidi.

Baada ya wanafunzi kumaliza miaka minane shuleni, wanalazimika kufanya mtihani unaosimamiwa na serikali kuweza kuamuliwa nani anastahilli kuendelea na masomo katika shule ya sekondari.

Wanafunzi wa shule za kibinafsi wanajipatia maksi nzuri zaidi na wana nafasi nzuri ya kuanza shule za sekondari.

Chaguo la mapema

Shule za sekondari za serikali zinawagharimu wanafunzi takriban Euro moja kwa siku. Kwa wakenya wengi hizo ni fedha nyingi ambazo hawamudu kulipa, kwasababu kila mkenya mmoja kati ya watano analazimika kuishi kwa chini ya Euro moja kwa siku. Shule ghali za sekondari ambazo ni za kibinafsi ni wachache tu-wanaojiweza- ndio wanaomudu kwenda. Kuanzia darasa la tisa, inaamuliwa kwa hivyo kama mtoto aendelee baadae na masomo au la: Bila ya masomo ya shule ya sekondari, mtoto anakuwa anamaliza mafunzo yake shuleni baada ya miaka minane tu. Lakini hata  aliyeingia katika shule ya sekondari ya serikali ana nafasi finyu ya kuweza baadae kuendelea na masomo katika chuo kikuu.

Kwakuwa masomo ya chuo kikuu pia yanagharimu fedha, serikali inawasaidia wale wanafunzi waliojipatia maksi nzuri tu. Katika shule za kibinafsi za sekondari, idadi kubwa ya wanafunzi huwa wanapata maksi nzuri na kwa namna hiyo wanaweza kutegemea msaada wa fedha wa serikali kuendelea na masomo yao.

Wazee matajiri wanaweza pia kuwaachia watoto wao wandelee na masomo hata kama maksi zao ni mbaya, ikiwa wao wenyewe ndio wanaolipia karo za shule. Gharama za masomo ni sawa na mishahara ya miezi mitano anayolipwa mwalimu mmoja.

Kiu cha kupata elimu na kuzidi kuongezeka vyuo vikuu

Licha ya vizingiti, watu nchini Kenya wanathamini sana elimu. Wazee wengi wako tayari kujibebesha madeni au kuuza mashamba ili mradi tu watoto wao wapate elimu nzuri. Njia mojawapo ambayo vyuo vikuu na taasisi nyengine za elimu zinatumia kukidhi kiu cha shahada ni kwa kutoa mafunzo tofauti ya muda mfupi na ya daraja tofauti. Kwa bahati mbaya, mara nyingi mafunzo hayo hayalingani na viwango vya kimataifa.

Katika vyuo vikuu vya serikali, idadi ya wanafunzi imeongezeka mara tano katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Na ili kuweza siku za mbele kuwa na idadi ya kutosha ya wahadhiri wenye ujuzi kwa idadi fulani ya wanafunzi, Kenya itabidi iruhusu kujipatia angalao wasomi elfu moja waliojipatia shahada ya juu ya uzamivu. Mnamo miaka ya nyuma Kenya ilikuwa na wanafunzi chini ya 230 waliofanikiwa kupata shahada hiyo na 50 kati yao wameipata nafasi hiyo kupitia taasisi ya Ujerumani ya kubadilishana taaluma-DAAD.Tatizo kubwa, lakini, ni jinsi ya kuwahimiza vijana wavutiwe na elimu. Wanafunzi wengi utakuta hawajajiandaa vya kutosha kuweza kutayarisha shahada ya juu ya uzamivu.

Katika nchi inayoendelea kwa kasi, mfumo wa vyuo vikuu unajikuta ukikumbwa na vizingiti  vya ukuaji huo .

Wanawake hawana nafasi nzuri

Shida kubwa zaidi wanakumbana nazo vijana wakike. Familia zinagharimia kwa uchache elimu ya wasichana. Ingawa kiwango cha maksi kwa wasichana kuweza kuingia vyuo vikuu ni cha chini, idadi ndogo tu ya wasichana ndio wanaoingia vyuo vikuu. Wanawake wanakamata asili mia 40 ya wanafunzi jumla wa vyuo vikuu.

Kwa miaka sasa faamilia ndizo zinazogharimia elimu ya watoto wao. Hali hiyo sio tu inawapa nguvu watoto wa matajiri,bali pia inawadhulumu wasichana.Kijadi watu wanategemea mwanamke ataolewa,atazaa na kuishughulikia familia.

Wasichana wanapokwenda chuo kikuu, mara nyingi wanachagua kusomea fani ya elimu jamii na fani nyenginezo ambazo haziwapatii sifa kubwa wala mapato makubwa.Wachache tu katika vyuo vikuu ndio wanaofanyakazi kama wahadhiri, maprofesa au wakuu wa vyuo vikuu, kwa namna ambayo inawaia shida wasichana kuendelea na masomo hadi kupata shahada ya uzamili seuze uzamivu. Kwa namna hiyo hali ya ukosefu wa wezani sawa inazidi kuselelea.

Mifano inayotia moyo

Kuna wanafunzi wakike na wa kiume, lakini ambao hadithi zao zinatia moyo.Kijana mmoja wa kutoka Nyeri alifanikiwa kupata maksi nzuri kuwapita wote wengine baada ya kumaliza darasa la nane. Shule mashuhuri ya sekondari ya mjini Nairobi ilimfadhili aendelee na masomo yake na kumpatia dahalia ili aweze kuishi na kuendelea na masomo katika fani ya kiuchumi na lugha ya kijerumani.Mfano maarufu kabisa wa mwanafunzi wa Kenya aliyefanikiwa ni ule wa Auma Obama-dada yake Barack Obama: Baada ya kumaliza vizuri mafunzo yake nchini Ujerumani kwa msaada wa shirika la DAAD la Ujerumani, alijipatia shahada ya juu, na hivi sasa anafanya kazi na shirika la kimataifa la Care-International.

Mwandishi: George Verweyen/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Miraji Othman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com