1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

El-Sisi aapishwa kuwa rais wa Misri

Mohamed Dahman8 Juni 2014

Mkuu wa majeshi wa zamani ameapishwa kuwa rais mpya wa Misri Jumapili(08.06.2014) na kutowa wito wa kujenga nchi itayokuwa na utulivu zaidi baada ya miaka kadhaa ya machafuko na uasi.

https://p.dw.com/p/1CEbF
Rais Abdel-Fattah al-Sisi wakati wa kuapishwa kwake mjini Cairo. (08.06.2014)
Rais Abdel-Fattah al-Sisi wakati wa kuapishwa kwake mjini Cairo. (08.06.2014)Picha: Reuters

Jemedari Mkuu huyo mstaafu Abdel- Fattah el-Sisi aliyempinduwa madarakani kiongozi wa kwanza aliechaguliwa kidemokrasia nchini humo mwezi Julai mwaka jana,akihutubia katika hafla iliofanyika katika kasri la rais mjini Cairo saa chache baada ya kuapishwa kwake na Mahakama Kuu ya Kikatiba amewataka wananchi wajibidiishe ili kwamba haki na uhuru wao uimarishwe.

El-Sisi ambaye alimpinduwa rais wa itikadi kali za Kiislamu Mohammed Mursi,anakuwa rais wa nane wa Misri tokea kupinduliwa kwa ufalme nchini humo hapo mwaka 1953 ukiwa ni mwaka mmoja baada ya mapinduzi ya kijeshi.Mbali na Mursi na raia wawili wengine waliotumikia nyadhifa za urais wa muda, marais wote wa Misri wanatoka kwenye jeshi lake la ulinzi.

Mizinga 21 ilimlaki el-Sisi wakati alipowasili katika kasri la rais lilioko kwenye wilaya ya wenye kipato ya Heliopolis mjini Cairo baada ya kuapishwa kwake.El-Sisi pia alikaguwa gwaride la kijeshi kwa heshima yake.

Aliwakaribisha waheshimiwa kadhaa wenyeji na wa kigeni wakiwemo wafalme wa Jordan na Bahrain,emir wa Kuwait na wana warithi wa ufalme wa Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mataifa matano ya Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia,Kuwait na Umoja wa Falme za Kiarabu yaliunga mkono hatua ya el- Sisi ya kumpinduwa Mursi na tokea wakati huo yamekuwa yakiipatia nchi hiyo inayokabiliwa na ukata wa fedha mabilioni ya dola.

Wito wa umoja

Akihutubia wageni wake katika kasri la Ittihadiya el-Sisi ametowa wito wa kuwepo kwa umoja na kukomeshwa kwa machafuko ya miaka mitatu yaliozuka tokea kuangushwa kwa dikteta Hosni Mubarak hapo mwaka 2011.

Rais Abdel-Fattah al-Sisi wa Misri na Rais wa muda aliyeondoka madarakani Adly Mansour mjini Cairo. (08.06.2014)
Rais Abdel-Fattah al-Sisi wa Misri na Rais wa muda aliyeondoka madarakani Adly Mansour mjini Cairo. (08.06.2014)Picha: picture-alliance/AP Photo

Amesema "Wakati umefika wa kujenga mustakbali utakokuwa imara zaidi na kufunguwa njia ya uhalisia mpya kwa mustakbali wa taifa hili."Ameendelea kusema kwamba bidii ya kazi jambo ambalo amekuwa akilirudia kulitolea wito katika wiki za hivi karibuni itawawezesha wananchi wa Misri kuyawekea nadhari masuala ya haki na uhuru wao kwa kuyaimarisha na kuyaendeleza.

Amesema "tutafautiane kwa matlaba ya taifa na sio juu ya taifa letu;tufanye hivyo kama sehemu ya hatua za taifa za kusonga mbele ambapo kwayo kila upande utakuwa unasikiliza wengine kwa njia ya tija bila ya kuwa na dhamira za pembeni.

El-Sisi amemshukuru rais aliyemaliza muda wake Adly Manosur ambaye ni jaji kitaaluma.

Amemwambia Mansour, "Misri likiwa kama taifa na wananchi wanapenda kukupa shukrani kwa huduma adhimu ulizowapatia."

Baadae wote wawili walisaini "waraka wa kukabidhiana madaraka" mbele ya waheshimiwa kadhaa wenyeji na wageni waliohudhuria hafla hiyo.

Dosari ya uchaguzi

El-Sisi alijipatia ushindi mkubwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi uliopita kwa kupata asilimia 97 ya kura kutokana na asilimia 47.45 ya watu waliojitokeza kupiga kura.

Wafuasi wa al-Sisi mjini Cairo.
Wafuasi wa al-Sisi mjini Cairo.Picha: Reuters

Uchaguzi huo wa siku tatu umetangazwa kuwa huru na haukuwa na udanganyifu lakini umeingia dosari kutokana na hatua zisizo za kawaida zilizochukuliwa na serikali kuwataka watu wajitokeze kupiga kura ikiwa ni pamoja na vitisho vya kuwatoza faini wale wanaobakia majumbani, kuongeza siku moja ya kupiga kura na kutowa usafiri wa bure wa treni na wa mabasi ili watu warudi kwenye maeneo walikozaliwa kupiga kura zao.

Uchaguzi huo pia imefanyika wakati kukiwa na udhibiti mkubwa wa uhuru katika kipindi cha miezi 11 tokea kupinduliwa kwa Mursi na ukandamizaji mkubwa wa wafuasi wa Udugu wa Kiislamu,mamia ya wafuasi hao wameuwawa katika mapambano na vikosi vya usalama.Wafuasi wa Mursi wameususia uchaguzi huo.

Vyombo vya habari vyenye kuliunga mkono jeshi navyo vimekuwa vikiupakazia sifa mbaya sio tu Udugu wa Kiislamu bali pia wanaharakati mashuhuri wasio na misimamo ya kidini waliohusika na vuguvugu la uasi wa mwaka 2011.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP

Mhariri : Iddi Ssessanga