1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EFES Uturuki : Papa atuliza Waislamu

29 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCoK

Akiwa katika siku yake ya pili ya ziara ya siku nne nchini Uturuki Papa Benedikt wa 16 leo ameutembelea mji wa Ephesus mji wa kale ambapo inaaminika kuwa Bikira Maria Mama wa Yesu Kristo alitumia siku zake za mwisho.

Akiwa kwenye mji huo Papa aliendesha misa na kusisitiza kwamba kumtukuza kwa pamoja mama wa Yesu Kristo ni kiungo kengine chenye kuwaunganisha Wakristo na Waislamu.

Ziara ya Papa nchini Uturuki ambayo ni ya kwanza kuifanya katika nchi hiyo yenye idadi kubwa kabisa ya Waislamu inakusudia kutuliza uhusiano kati ya Wakristo na Waislamu duniani.

Uturuki imempongeza Papa Benedikt kwa kauli yake hiyo inayoonyesha kutaka usuluhishi na Waislamu na kile kinachoonekana kama kuunga mkono kwake upya jaribio la Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Leo jioni atakuweko Instanbul kwa ajili ya kukutana na Askofu Mkuu Bartholomew wa Kwanza wa Wakristo wa Madhehebu ya Orthodox kwa nia pia ya kuondowa mfarakano kati ya matawi hayo mawili ya Kikristo duniani.