1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ECOWAS yataka utawala wa kiraia kurejeshwa Mali

Amina Mjahid
7 Septemba 2020

Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS imeatoa wito kwa wanajeshi walioasi Mali kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia kufuatia mapinduzi yaliofanyika Agosti 18

https://p.dw.com/p/3i7i1
Niger Treffen der afrikanischen Union in Niamey - Mahamadou Issoufou
Picha: AFP/I Sanogo

Jumuiya hiyo ya wanachama 15 tayari imeiwekea Mali vikwazo baada ya mapinduzi ya kijeshi ikiwemo kufungia mipaka yake, marufuku ya biashara, kuzuwia mtiririko wa kifedha huku ikitaka uchaguzi ufanyike baada ya miezi 12.

Rais wa Niger Mahamadou Issoufou, ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa jumuiya hiyo ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS amesema ni jukumu la jumuiya hiyo kuisadia Mali kurejesha kwa njia ya kidemokrasia, utawala wa kiraia katika taasisi zote za serikali. Rais Issoufou amesema wanajeshi waasi walioipundua serikali wanapaswa kuwasaidia ili na wao waisaidie Mali.

Rais huyo wa Niger amesema vikwazo ilivyowekewa Mali vitaondolewa kulingana na namna jeshi litakavyotekeleza matakwa ya jumuiya ya ECOWAS. Viongozi takriban wanane akiwemo rais wa Senegal Macky Sall, Alassane Ouattara wa Ivory Coast na rais wa Guinea-Bissau Umaro Sissoco Embalo walikuwepo katika ufunguzi wa leo wa mkutano wa kujaribu kusuluhisha mgogoro wa Mali uliofanyika kwa njia ya video.

Mwanzoni mwa juma hili, jeshi lililoasi lilifanya mazungumzo na makundi ya kisiasa kuhusiana na ahadi yake ya kurejesha nchi katika utawala wa kiraia baada ya shinikizo kutoka kwa nchi jirani juu ya hofu ya kuyumba zaidi kwa uthabiti wa taifa hilo linalokumbwa na vita.

Rais Keita kutibiwa nchi za nje kwa masharti

Mali I Ibrahim Boubacar Keita
Rais wa zamani wa Mali Ibrahim Boubakar Keita Picha: Getty Images/AFP/P. Ekpei

Huku hayo yakiarifiwa Afisa mmoja katika serikali ya Mali amesema rais wa zamani wa nchi hiyo aliyepinduliwa madarakani mwezi uliopita, alisafiri kuelekea Umoja wa falme za kiarabu kwa matibabu. Kulingana na Ali Diallo mfanyakazi wa serikali, Keita alifika huko siku ya Jumamosi. Rais huyo wa zamani aliye na miaka 75 alipelekwa hospitalini mjini Bamako siku chache zilizopita, akiwa na dalili zinazoelezea kuwa alipatwa na kiarusi.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari UAE vilivyonukuu taarifa kutoka wizara ya mambo ya kigeni, hatua ya Keita kupata matibabu zaidi ilifikiwa baada ya ombi kutoka kwa jeshi la Mali, ikiungwa mkono na mwenyekiti wa ECOWAS rais Mahamadou Issoufou.

Baada ya ombi hilo, kamati ya baraza la kijeshi la mpito lilitoa ruhusa ya Keita kutibiwa nje ya nchi kwa masharti kuwa atarejea nyumbani baada ya miezi mitatu. Mali iliingia katika mgogoro wa kisiasa mwezi mmoja uliopita, wakati Keita alipokamatwa na viongozi wa wanajeshi walioasi na kulazimishwa kujiuzulu.

Ibrahim Boubakar Keita ameiongoza Mali kuanzia mwaka 2013 baada ya eneo la kaskazini kutwaliwa na wanamgambo na makundi mengine ya waasi kufuatia mapinduzi mengine yaliyofanyika mwaka mmoja kabla.

Mashirika kadhaa ya kigaidi yanabakia kuwa na nguvu nchini Mali, baadhi ya mashirika hayo yanayofungamana na kundi la dola la kiislamu au hata kundi la kigaidi la al Qaeda. Vikosi vya Umoja wa Ulaya nchini humo pamoja na kile cha Umoja wa Mataifa bado vinaendelea kuwepo kujaribu kulinda amani Mali.

Chanzo: reuters/afp