1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"DW yampatia Mama Batuli haki ya kurithi"

23 Januari 2013

Hiki ni kisa cha kubuni cha namna msichana Batuli alivyohamasika na kuihamasisha familia yake kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW na kutumia faida za matangazo hayo kupigania haki ya urithi wa mama yake.

https://p.dw.com/p/17QEu
Wettbewerb zum 50-jährigem Jubiläum. Khalid Maulid Saburi Dar Art Youth (Day) P.O. Box 79505 Dar es Salam, Tanzania 0714124081 0718656020
50 Jahre Kisuaheli Redaktion WettbewerbPicha: DW

Ilikuwa jioni wakati Mama Batuli akiwa jikoni akipika majani ya maboga kwa ajili ya chakula cha usiku. Mboga ilipokaribia kuiva, akageuka kuchukua chumvi, lakini hakuiona. Akatazama juu kwenye kabati, akaiona. Akaita kwa nguvu: "Batuliiiiii….”

Mama Batuli hakusikia chochote, huzuni kidogo ikamtawala, akainuka mwenyewe akachukua chumvi, akatia kwenye mboga, akaonja. Akaita tena.

“We Batuliii weee....!!” Kimya.

Akaipua mboga, akakaa akitegemea kumuona Batuli japo hakusikia akiitika. Ulipita muda mrefu kidogo bila kumuona Batuli kuitikia kuitwa kule. Akaghadhabika.

Huku akibwatabwata, Mama Batuli akainuka haraka akaenda hadi chumbani kwa Batuli.

“Batuli” aliita kwa sauti ya chini, ila yenye ukali kidogo, akitikisa kichwa chake taratibu, macho yake makubwa yalimtazama kwa ghadhabu kuu alipomuona kajibweteka kitandani akitazama kompyuta yake ambayo alinunuliwa na hayati baba yake ambaye alifariki wiki tatu zilizopita.

Wakati wote huu, Batuli alikuwa ameinamia kompyuta yake akiwa na visikizi alivyovivisha masikioni, akitazama na kusikiliza habari na vipande vya video vilivyorekodiwa vya idhaa ya Kiswahili ya DW, -hakuweza kusikia chochote zaidi ya sauti iliyosikika kwenye visikizi vile.

Mama Batuli aliona kudharaulika na kwamba binti ameanza kumshinda, -kwa ghadhabu akamsogelea kwa mwendo wa haraka, akamvuta nywele kwa nguvu. Batuli alishtuka, akageuka haraka, akazabwa kofi kabla ya kugundua nani aliyefanya ghasia ile, akamuona mama yake akiwa na hasira, mdomo kaukunja kuashiria hasira, aliangalia chumba chake huku huko harakaharaka, kujua wapi kakosea, hakuona kosa, akaangalia saa ya ukutani mara moja, akaona ni saa moja na dakika kadhaa, akaguna, “mmh!” huku machozi yakimlengalenga, akafungua kinywa chake,

“Mama kwani ku...” kabla hajamaliza mama yake akamkatiza, tena kwa kubwata kwa ukali;

“Yaani mie nakuita weee..., we umebweteka tu, tena nakufuata hata huku, hujali. Unaona umekua eh? Sasa kama ndivyo mjifunzayo huko chuoni, utahama humu ndani kwani nitashindwa kukuvumilia Batuli. Hebu simama haraka, uende jikoni ukasonge ugali sasa hivi...” akafikicha vidole vyake viwili vilivyotoa sauti wakati akimuhimiza kufanya haraka. Batuli alimwangalia mama yake, machozi yakamtoka, kisha akasema, tena kwa upole;

“mama, nisamehe. Wakati wote huo mimi sikukusikia. Nilikuwa nikisikiliza na kutazama habari. Nitaenda kupika sasa.” Akafuta machozi na kuondoka. Alimsikia mama akifyoza, machozi yakamtoka tena, akafuta.

Alipofika sebuleni, kabla ya kufika jikoni, akawasha redio yao kubwa iliyokuwa na spika mbili za kisasa, akabofyabofya kitufe kimojawapo hadi alipomsikia mtangazaji wa idhaa ya kiswahili ya DW akizungumza. Akatabasam kidogo, akaongeza sauti kiasi cha alichodhani angeweza kusikia akiwa jikoni.

Huku nyuma mama ya Batuli alizima ile kompyuta, akaifunga, akaiweka katika begi lililokuwa chini, akaibeba hata chumbani kwake, akaifungia kwenye kabati, funguo akaficha sehemu nyingine ambayo Batuli asingeweza kujua.

Batuli akakoroga uji, akaacha utokote ili apate kusonga ugali. Wakati huu alisikia wimbo, alitabasamu akaanza kucheza, ghafla akapigwa na butwaa alipotambua hakuna sauti ya muziki zilizosikika tena masikoni mwake, akasimama, akaenda kwa upesi hadi sebuleni, kufika mlangoni alistaajabu alipomuona mama yake akichomoa spika zote mbili.

Mama Batuli akabeba moja na kuingia mlango uliokuwa ukielekea kwenye milango ya vyumba vya kulala. "Anahamisha spika?", alijiuliza Batuli kimoyomoyo. Akasikia mlango wa chumba cha mama yake ukifunguliwa, akasubiri sekunde kadhaa kisha akanyata hata alipofika chumbani kwake, alistaajabu tena alipogundua kuwa mama yake alichukua hata kompyuta yake.

Machozi yalimlenga Batuli, lakini alijizuia kulia, alikumbuka kama wakati huu anapaswa kuwepo jikoni akipika ugali. Akachukua simu yake na spika ndogo za simu za masikioni, akabofyabofya simu yake hadi alipofanikiwa kupata matangazo ya idhaa ya kiswahili ya DW, akaunganisha spika zile kisha akazivaa masikioni, akaiweka simu yake kwenye mfuko wa sketi yake nzuri ya rangi ya samawati, akatabasamu tena.

Akanyata tena, alipofika sebuleni, hakuiona spika ile ya pili, wala mama yake, akajua mama yake atakuwa amekwisha ichukua nayo pia, naye yupo chumbani. Akanyata tena kwa upesi hadi jikoni.

Uji ule ulikuwa umetokota kiasi cha kuanza kukakamia, -akatia unga na kuusonga ugali hata ulipoiva, -akatandika meza, kisha akawaita wote waje kula. Mezani Batuli alionekana na kisikizi upande mmoja, mama yake alimtazama kwa hasira ambayo hakutaka wengine wajue.

Batuli alitazama chini kwani alijua mama yake hakupenda kusikiliza kwake habari hata kwa njia ya simu ila alikuwa ana uhakika ya kwamba mama yake asingeweza kumnyang’anya simu yake.

Walipomaliza kula, Batuli alikusanya vyombo vyote na kwenda kuviosha na wakati huu aliweka visikizi vyote kwenye masikio yake. Mama yake alikasirika na akafikiri moyoni mwake ya kuwa binti yake amekuwa na kiburi. Wakatawanyika wote na kwenda kulala.

Siku nne baadaye, Mama Batuli alishtushwa na ujio wa ugeni ambao haukuwa na taarifa ya awali, wageni hao walikuwa ni ndugu upande wa marehem mume wake. Aliwapokea vema. Na baada ya chai na mapumziko mafupi, mmoja kati ya ndugu wale akasema;

“Shemegi, naamini unajua sheria vema ya kwamba baada ya mume kufariki, mke anapaswa kuacha watoto, nyumba na mali zote za marehem na hana haki ya kurithi.” Akameza mate kisha akaongeza “na ndiyo sababu ya mtoto wa dada yake marehemu, Guido, alibaki hapa kwani mpwa wa akina Haruni ni mrithi halali.”

Mama Batuli hakusema jambo kwa muda, alionekana kuwa mwenye huzuni kuu wakati yule aliyemuita shemeji akiongea, kisha akasema,

“Sawa, najua sheria na taratibu hizo, ila mali mnazoziona nilichuma pamoja na marehemu mume wangu. Zaidi ya yote hawa ni watoto wangu mie na marehemu. Nafikiri nina haki ya kuishi nao...”.

Kabla hajaendelea alikatishwa na ndugu mwingine: “Usitufanye wajinga wewe mama. Hapa utake, usitake, lazima uondoke. Na hiyo ndiyo kauli yetu ya mwisho. Tusibishane.”

Huyu ndugu alikuwa mwenye sauti ya ukali na macho yake madogo yalionesha hasira na chuki. Hivyo ndivyo Batuli na mama yake walivyayaona.

“Sawa, nimewaelewa. Ila naomba mnipe siku mbili, kisha nitaondoka,” alisema Mama Batuli huku machozi yakimlengalenga. Wakakubaliana hivyo na wale ndugu wakaondoka.

Kesho yake mchana, kama kawaida, Batuli alikuwa akisikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, ndipo aliposikia Makala ya Wanawake inayozungumzia kupitishwa kwa sheria mpya Tanzania ambayo inawapa haki wanawake kurithi mali na watoto. Mwisho wa makala, mtayarishaji akasema kwamba makala hiyo ingelirejewa tena kesho yake jioni. Alifurahi sana ila hakumwambia mama yake saa ile, akasubiri hadi hiyo jioni ya kesho ifike. Ulipofika muda wa matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW jioni hiyo, Batuli akategeshea mpaka pale nusu ya mwanzo ya habari na uchambuzi umemalizika na makala zinaanza, akapandisha kubwa inayosikika. Hata mama yake akasikia hiyo maklaa.

Mama Batuli hakuamini, akamtazama Batuli akauliza: “Jamani Batuli, hasa nitawezaje kufanikiwa?”

“Twende mahakamani,” alisema Batuli kwa moyo wa imani kuwa mama yake atabakia pale na wao, na mpwa wake atarudi kwa shangazi yake.

Kesho yake waliwahi mapema. Hatua zote za muhimu zilizopaswa kufanyika zilifanyika, hadi hatimaye Mama Batuli akapata haki yake ya kuwa mrithi halali wa mali na watoto aliozaa na marehemu mumewe.

“Nisamehe mwanangu Batuli, nilijua unapoteza muda na sikuuona umuhimu, ila sasa nimeuona. Pia nawashukuru hawa watendaji wa hii Idhaa ya Kiswahili ya DW, kwani wanazo njia nyingi za kutufikia, simu, redio na hata kwa njia ya mtandao! Nitarudisha spika zote sebuleni, na nitakupa kompyuta yako, pia chukua fedha hii ukanunue kifurushi cha intaneti cha shilingi 50,000 utumie kwenye modemu yako ili uzidi kuyapata matangazo yao kwa njia ya mtandao. Pia nitakununulia spika imara za masikoni, ili hata ninapokutuma sehemu mbalimbali kama benki na maofisini, uendelee kusikiliza habari pindi usubiripo huduma. Nakupenda sana mwanangu.”

Batuli akafurahi, akamrukia mama yake na kumkumbatia.

Kuanzia siku ile mama yake na Batuli, Batuli na Haruni walikuwa hawapitwi na matangazo ya Idhaa ya kiswahili ya DW kwani waliamini inahabarisha, inafundisha, inaadilisha, inaburudisha na zaidi ya yote hutumia lugha fasaha ya Kiswahili ambayo kila mzungumzaji wa lugha hiyo huelewa.

Na wao wakawa sasa ni wachangiaji wakubwa wa maoni kwa njia za ujumbe mfupi wa maandishi kwa simu ya mkononi, ukurasa wa Facebook na hata barua.

Tanbihi: Hadithi hii ya kubuni imeandikwa na Sarah Hosea Msemwa wa Ruvuma, Tanzania kwa ajili ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Idhaa ya Kiswahili ya DW.