Dortmund wawaonyesha kivumbi Bayern | Michezo | DW | 05.03.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Dortmund wawaonyesha kivumbi Bayern

Borussia Dortmund walipiga hatua kubwa katika kuhifadhi taji lao la ligi ya soka Ujerumani – Bundesliga, baada ya kuwafunga Mainz magoli mawili kwa moja.

Wachezaji wa Dortmund wanaonekana kuwa na mshikamano

Wachezaji wa Dortmund wanaonekana kuwa na mshikamano

Ushindi huo ulifungua mwanya wa alama saba kileleni mwa ligi huku ikiwa imesalia mechi kumi pekee msimu kukamilika. Mjapani Shinji Kagawa alifunga bao la ushindi katika dakika ya 77, dakika tatu baada ya Mohamed Zidan kuwasawazishia Mainz bao la kwanza. Dortmund ilisonga hadi pointi 55 kutokana na mechi 24 huku nambari mbili Bayern Munich wakisalia na pointi 48 baada ya kushindwa na Bayer Leverkusen magoli mawili kwa nunge, ambako wachezaji Stefan Kiessling na Karim Bellarabi walitikisa wavu.

Nambari tatu Borussia Moenchengladbach walishindwa na Nuremberg goli moja bila jawabu, huku Nao Schalke 04 wakiduwazwa na Freiburg kwa kufungwa mabao mawili kwa moja.

Ferguson: Ligi kuamuliwa tarehe 30 Aprili

Manchester United iko pointi mbili nyuma ya Manchester City

Manchester United iko pointi mbili nyuma ya Manchester City

Katika ligi ya Uingereza, viongozi wa Ligi Manchester City walisajili ushindi wa nyumbani wa magoli mawili kwa nunge dhidi ya Bolton Wanderers nao Manchester United wakashinda mchuano wao dhidi ya Tottenham Hotspurs mabao matatu kwa moja. United sasa wako alama mbili nyuma ya City. Mkufunzi wa Manchester United Sir Alex Ferguson anasema sasa mchuano wa Man United na Man City wa tarehe 30 Aprili ndio utakaoamua mshindi wa taji la msimu la Ligi. Spurs wako alama 13 nyuma ya viongozi City huku kukiwa kumesalia mechi 11. Arsenal wako katika nafasi ya nne na faida ya pointi tatu dhidi ya Chelsea, wakati Robin Van Persie alipowapa ushindi wa kibahati wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Liverpool.

Afisa Mkuu wa Chama cha Mameneja wa Ligi Richard Bevan ameishtumu klabu ya Chelsea kwa kumpiga kalamu kocha Andre Villas-Boas, akionya kuwa klabu hiyo imeanza kuwa “Aibu” kwa Premier League. Bevan amesema Mmiliki billionaire wa Chelsea Roman Abramovich huenda anazo fedha lakini hajatambua siri ya kuijenga klabu yenye mafanikio. Villas-Boas alifutwa kazi jana Jumapili siku moja baada ya Chelsea kushindwa goli moja kwa nunge na Westbromwich Albion. Kichapo hicho kilikuwa mojawapo ya misururu ya matokeo duni na sasa Chelsea inakumbwa na kibarua cha kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa msimu ujao. Bevan aliiambia redio ya BBC kuwa kumtafuta kocha wa nane katika miaka tisa ni aibu kubwa kwa mmiliki, klabu, mashabiki na ligi.

Nani atakayevaa vyatu vya AVB?

Andre Villas-Boas alitimuliwa baada ya matokeo duni

Andre Villas-Boas alitimuliwa baada ya matokeo duni

Roberto di Matteo ambaye amekuwa msaidizi wake sasa amepewa jukumu la ukaimu na ana kibarua cha pambano la marudiano la duru ya tano ya kombe la FA dhidi ya Birmingham, na kisha mchuano wa mkondo wa pili wa awamu ya 16 ya ligi ya mabingwa dhidi ya Napoli ambapo Chelsea ilifungwa magoli matatu kwa moja katika mkondo wa kwanza. Bevan alisema ikiwa unataka ufanisi basi ni sharti uzingatie mkakati wa muda mrefu.

Kunayo majina ambayo yanapigiwa upatu kuchukua nafasi ya AVB, nayo ni Mkufunzi wa zamani, Jose Mourinho wa Real Madrid, Pep Guardiola wa Barcelona, Rafa Benitez, na Jurgen Klopp wa Borussia Dortmund. Aidha Fabio Capello ambaye alijiuzulu hivi majuzi kama kocha wa Timu ya taifa ya Uingereza pia anaorodheshwa kuwa mrithi.

Ubingwa wa Ulaya

Nembo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya - UEFA

Nembo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya - UEFA

Mechi za marudiano za awamu ya 16 ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya zitanerejea ambapo mechi za kufuzu kwa robo fainali za AC Milan na Barcelona zinaonekana kuwa tu burudani kwa maana tayari wana faida ya magoli kutokana na mechi zao za kwanza. Michuano ya Zenit St Petersburg na Olympique Lyon itakuwa ya kukata na shoka kwa sababu watatetea faida ya goli moja ugenini.

Jumanne AC Milan watakutana na Arsenal uwanjani Emirates lakini wana faida ya magoli manne kwa nunge kutokana na mkondo wa kwanza. Kisha nchini Ureno, Zenit St Petersburg ya Urusi itatetea ushindi wa mkondo wa kwanza wa magoli matatu kwa mawili dhidi ya Benfica.

Katika mechi zitakazochezwa Jumatano, Barcelona ambao ndio mabingwa watetezi wa kombe hilo watacheza na Bayer Leverkusen nyumbani Camp Nou wakiwa tayari na magoli matatu kwa moja kutokana na mkondo wa kwanza. Olympique Lyon wanapeleka faida ya goli lao moja kwa nunge nyumbani kwa APOEL Nicosia nchini Ugiriki.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters

Mhariri: Josephat Charo