Dondoo za spoti | Michezo | DW | 19.12.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Dondoo za spoti

Bayern yaanza kipindi cha mapumziko ya msimu wa theluji wakiwa kileleni mwa ligi ya Ujerumani Bundesliga huku nako nchini Uingereza Manchester United na Manchester City zikizidi kujiimarisha kileleni mwa ligi ya primia.

Wachezaji wa Bayern Munich Mario Gomez na David Alaba wakisherekea bao lao dhidi ya FC Cologne

Wachezaji wa Bayern Munich Mario Gomez na David Alaba wakisherekea bao lao dhidi ya FC Cologne

Mkurugenzi wa spoti wa klabu ya Bayern Munich Christian Nerlinger ameelezea furaha yake baada ya miamba hao wa Ujerumani kumaliza nusu ya kwanza ya msimu wa ligi ya Ujerumani Bundesliga wakiwa kileleni. Ushindi wa Bayern wa mabao matatu kwa nunge dhidi ya Cologne siku ya ijumaa uliwaweka alama tatu mbele ya mahasimu wao Borussia Dortmund na Schalke huku ligi ya Bundesliga ikiingia kipindi cha mapumziko cha wiki nne cha msimu wa theluji. Kocha wa Bayern Jupp Henckes alifurahia matokeo hayo baada ya firimbi ya mwisho.

Bayern watapambana na waangamizaji wa Manchester United Basel katika awamu ya 16 ya ligi ya mabingwa barani ulaya Uefa na Nerlinger amesema ana furaha kutokana na maendeleo yaliyofanywa kufikia sasa msimu huu chini ya kocha Jupp Heynckes. Bayern sasa wataumiza nyasi dhidi ya klabu ya divisheni ya pili Bochum katika awamu ya tatu ya Kombe la Ujerumani hapo kesho katika mchuano wao wa mwisho mwaka huu. Licha ya hayo yote, Nerlinger amesema Borussia Dortmund ambao ni mabingwa wa msimu uliopita wa Bundesliga, ndio wapinzani wao namba moja msimu huu.

Katika matokeo mengine ya Bundesliga, Borussia Moenchengladbach ilikamilisha msimu wake bora zaidi wa nusu ya kwanza ya ligi katika miaka 35 kwa kuwazaba Mainz moja bila hapo jana. Baada ya ushindi huo kocha wa Moenchengladbach Lucien Favre ambaye timu yake haijawahi kushindwa nyumbani, alisema watapigania kila pointi na kwamba wataukabili kila mchuano jinsi utakavyokuja. Moenchengladbach wanashikilia nafasi ya nne kwenye jedwali la ligi ya Bundesliga alama moja nyuma ya Borussina Dortmund na Schalke na nne nyuma ya viongozi Bayern Munich ambao wana alama 37. awamu ya pili ya msimu itarejea januari 20. Kwingineko klabu ya Hertha Berlin imemtimua kocha wake Markus Babbel baada ya miaka 39 baada ya mgawanyiko kuibuka baina yake na mkurugenzi wa spoti wa klabu hiyo.

Tukivuka hadi nchini Uingereza nahodha wa Chelsea John Terry anatarajiwa kuwa katika hali shwari kupambana na dhidi ya Tottenham siku ya Alhamis licha ya kukumbwa na jeraha la kifundo cha mguu wakati wa mazoezi hii leo. Hata hivyo taarifa ya klabu hiyo imesema Terry atakuwa tayari kwa mchuano wa Alhamis. Wachezaji Ramires na David Luiz walikuwa nje ya mazoezi kutokana na majeraha.

Kocha Sir Alex Ferguson anaamini kuwa timu yake ya Manchester United imejinyanyua, kujipanguza vumbi na kusahau mshtuko wa kubanduliwa nje ya mechi za ligi ya mabingwa na watasalia na lengo la kuhifadhi taji la ligi ya primia nchini Uingereza. Ushindi wa mabao mawili kwa nunge dhidi ya QPR hapo jana ulikuwa wao wa pili mfululizo tangu Basel walipowadunisha vijana hao wa Fergie na kuwateremsha hadi michuano ya Europa league. Huku United ikijiandaa kukabiliana na timu tatu Fulham, Wigan na Blackburn, Fergie anataka timu yake isalie kileleni mwa ligi na kuchukua mweleko wa taji la primia katika nusu ya pili ya msimu huu.             

Wayne Rooney wa Manchester United na Gareth Barry wa Manchester City

Wayne Rooney wa Manchester United na Gareth Barry wa Mnchester City

Kwa upande mwingine naye Mkufunzi Roberto Mancini amewaonya wachezaji wake wa Manchester City kuwa wanakabiliwa na vita vikali vya kuwania taji la primia kutoka kwa mahasimu wao Manchester united hadi mwishoni mwa msimu.

China leo imeanzisha kesi za takriban wachezaji soka 60 wa kitaifa, marefa, makocha na maafisa wengine wanaoshtumiwa kwa kuhusika katika visa vya kupanga mechi na sakata za kucheza kamari ambazo zimesababisha mashabiki wasioathirika kuupa mchezo kisogo. Zhang Jianqiang, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa kamati ya marefa ya chama cha soka cha Japan, alifika mahakamani hii leo miezi tisa baada ya kutiwa mbaroni kwa madai ya kupanga mechi na kupokea rushwa. Haijabainika wazi muda ambao mashtaka hayo yatachukua lakini hukumu zinatarajiwa kutangazwa katika kipindi cha muda usiojulikana.

Nchini italia polisi wamewakamata watu 17 kuhusiana na uchunguzi wa kupanga mechi na ubahatishaji. Wale waliokamatwa ni pamoja na kiungo wa kati wa klabu Atalanta na timu ya Italia Cristiano Doni. Ukamataji huo ulifanywa katika miji kadhaa nchini Italia baada ya uchunguzi wa mwanzo na mahakimu katika mji wa kaskazini wa Cremona.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Josephat Charo