1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DHAKA:Wanasiasa walaumiwa kuchagiza maandamano

26 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBVp

Mkuu wa jeshi la Bangladesh Jenerali Moen U Ahmed analaumu wanasiasa walioondolewa madarakani na serikali inayoungwa mkono na jeshi kwa kuchangia katika maandamano yaliyosababisha muda wa kutotembea kutangazwa na serikali.Hali hiyo ilitangazwa katika miji sita ya Bangladesh tangu jumatano iliyopita baada ya maandamano kusambaa kutoka mji wa Dhaka.Nchi hiyo imekuwa katika hali ya tahadhari tangu mwanzoni mwa mwaka huu baada ya uchaguzi mkuu kufutwa.

Serikali inayosimamiwa na jeshi ilichukua jukumu la kuongoza nchi siku moja baada ya hali ya tahadhari kutangazwa na uchaguzi kufutwa baada ya kipindi cha miezi kadhaa ya ghasia kwasababu ya madai ya wizi wa kura.Jeshi linawakamata wanasiasa wa zamani katika juhudi za kupambana na ufisadi.Wanasiasa zaidi ya 150 wamekamatwa akiwemo waziri mkuu mmoja wa zamani.

Kulingana na mkuu wa jeshi ,uchaguzi mwengine umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka ujao.Kiongozi wa serikali hiyo ya muda Fakhruddin Ahmed anatangaza kuwa hatua ya kutangaza hali ya kutotembea ililazimika kuchukuliwa ili kuepuka ghasia baada ya waandamanaji kupambana na polisi katika mji mkuu wa Dhaka na kwengineko.

Serikali ilisitisha kwa muda amri hiyo hapo siku ya Ijumaa na Jumamosi vilevile kutanganza kuwa hali hiyo itaendelea hii leo kwa kipindi cha saa 18.