Desmond Tutu asherehekea leo miaka 80 ya kuzaliwa kwake | Masuala ya Jamii | DW | 07.10.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Desmond Tutu asherehekea leo miaka 80 ya kuzaliwa kwake

Desmond Tutu, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel na mmojawapo wa wanaharati waliopinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, anatimiza leo miaka 80 tangu alipozaliwa.

default

Desmond Tutu

Desmond Tutu alizaliwa Octoba 7 mwaka 1931 huko Klerksdorp, Transvaal. Ni mtoto wa pili kati ya watoto watatu wa mzee Zachariah Zililo Tutu na mkewe, Aletta, na ni mtoto pekee wa kiume. Familia yake ilihamia mjini Johannesberg wakati alipokuwa na umri wa miaka 12. Babake alikuwa mwalimu na mamake mpishi na mfanyakazi wa kufagia katika shule moja ya watu wenye ulemavu wa kuona.

Ingawa Desmond Tutu alitaka kuwa daktari, familia yake haingeweza kugharimia karo yake kwa hiyo akafuata nyayo za babake na kuwa mwalimu. Alikuwa askofu mkuu wa kwanza mwafrika mjini Cape Town.

Kwa miongo mingi iliyopita askofu huyo mkuu wa zamani wa kanisa la Kianglikana mjini Cape Town alikosoa vikali ubaguzi wa rangi, ubaguzi wa kimbari na kila aina ya ubaguzi Afrika Kusini na ulimwenguni kote kwa jumla.

Tangu kujiuzulu kwake kama askofu mkuu wa Cape Town, Tutu alikuwa mwenyekiti wa tume ya ukweli na maridhiano iliyokuwa na kibarua cha kusikiliza ushahidi na kutafuta msamaha na maelewano katika visa vya uhalifu na ukiukaji wa haki za binadamu vilivyofanyika wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi.

Desmond Tutu Südafrika Mexiko

Tutu wakati wa michuano ya kombe la dunia Afrika Kusini

"Haiaminiki! Naota jamani, naota mimi. Niamsheni. Ndoto nzuri iliyoje....Tunauonyesha ulimwengu. Sisi ndio ulimwenguni!"

Mtu hujiuliza kwa mshangao, huyu Tutu ana akili timamu, kufuatia maneno hayo aliyoyasema wakati aliposimama mbele ya umati mkubwa wa watu katika uwanja wa mpira akiwa amevalia jezi ya timu ya taifa ya kandanda ya Afrika Kusini wakati wa mashindano ya kombe la dunia la kandanda lililofanyika nchini humo mwaka jana.

"Tunauonyesha ulimwengu kuwa sisi ndio ulimwenguni, kwa kuwa Afrika ni chimbuko la binaadamu"

Hapana Tutu yeye sio mwendawazimu, ni mtu wa kawaida kabisa, wa kipee, mwenye bashasha na furaha tele! Anapenda kufanya mizaha pia kama alivyowahi kuwaambia waandishi wa habari siku moja akisema, "Na hatutapatikana tena kwa mahojiano na vyombo vya habari."

Tutu anapendwa sana duniani kote katika vichekesho, michezo ya kuigiza kwenye televisheni na nyimbo za miondoko ya 'pop'. Ni mtu ambaye licha ya changamoto zilizomkabili, hakupoteza heshima na taadhima yake. Ana huzuni kubwa akikumbuka wakati alipokuwa mwenyekiti wa tume ya kitaifa ya ukweli na maridhiano mwaka 1995 iliyochunguza uhalifu wa utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini. Picha ya askofu huyo wa zamani ilisambaa ulimwengu mzima akiwa analia na huku akiwa amekiinamisha kichwa chake mezani.

"Ilikuwa hali ya kutisha. Mimi hulia kirahisi na nililia siku ya kwanza ya kusikiliza ushahidi. Nikasema haikuwa haki. Mungu hungeruhusu jambo hili kutokea kwa sababu vyombo vya habari baadaye viliniangazia mimi badala ya watu waliokuwa wahanga halisi. Nilipojihisi nataka kulia, ningefanya hivyo nyumbani au kanisani, lakini maombi yaliniimarisha na kunihifadhi."

Südafrika Apartheid Schild White Area

Bango likionyesha eneo la Wazungu wakati wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini

Lakini kuna misimamo yake mingine ambayo haipaswi kusahaulika wala kupuuzwa. Tutu anaweza kuwa mwiba pia dhidi ya rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, aliyemtaka ang'atuke madaraki kwa ajili ya masilahi ya Zimbabwe na Afrika nzima.

Kazi yake kubwa inabakia ile aliyoifanya wakati alipoingoza tume ya ukweli na maridhiano ambapo kwa kipindi cha miaka mitano watu waliofanya uhalifu wakati wa utawala wa kibaguzi pamoja na wahanga wao walikabiliana ana kwa ana, mfumo ambao umekuwa mfano wa kuigwa katika maeneo mengine ya mizozo katika kutafuta maridhiano. Ufanisi uliopatikana hata hivyo sio mkubwa sana kwa kuwa ni wahalifu wachache tu waliojitokeza na kubeba dhamana kama vile rais wa zamani wa Afrika Kusini, Frederik de Klerk.

Südafrika Präsident Frederik Willem de Klerk

Aliyekuwa rais wa Afrika Kusini wakati wa utawala wa ubaguzi, Frederik de Klerk, kushoto, na Nelson Mandela

Tume hiyo ilikuwa chombo muhimu kuiponya jamii. Wengi walibadilika baada ya mchakato mzima wa kusikilizwa kesi mbalimbali, jambo lililokuwa chanzo cha maneno ya Tutu yaliyojaa mafundisho muhimu kwamba, "Ni bora zaidi kuwa na rafiki kuliko kuwa na adui na kama adui yako atakuwa rafiki yako, itakuwa vyema zaidi."

Mwandishi: Josephat Charo/Stäcker, Claus

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 • Tarehe 07.10.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12nSw
 • Tarehe 07.10.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12nSw