1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

De Maziere afanya ziara ya ghafla Afghanistan

Mohammed Khelef22 Desemba 2011

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Thomas de Maziere, amefanya ziara ya kushtukizia nchini Afghanistan ambako ameelezea matarajio yake kuhusiana na mpango wa kujiondoa kwa wanajeshi wa Ujerumani nchini humo.

https://p.dw.com/p/13XRo
Thomas de Maiziere (katikati) akiwa ziarani Afghanistan.
Thomas de Maiziere (katikati) akiwa ziarani Afghanistan.Picha: dapd

De Maziere amesema kuwa hali ya usalama nchini Afghanistan imeimarika kwa mara ya kwanza baada ya miaka kadhaa. Matukio yanayohatarisha usalama yamepungua kwa asilimia 25 katika nchi hiyo na asilimia 50 kwa eneo la kaskazini. Waziri huyo wa Ulinzi amesindikizwa na kamati ya ulinzi ya Bunge la Ujermani na pia kamishna wa Bunge wa Vikosi vya Ulinzi, Hellmut Königshaus.

Hivi karibuni, jeshi la Ujerumani (Bundeswehr) lilikabidhi kituo cha kwanza cha kijeshi kwa serikali ya Afghanistan, ikiwa ni hatua ya kwanza kuelekea kujiondoa kabisa kijeshi nchini humo. Kwa sasa Ujerumani ina wanajeshi 5,000 wanaotumika kwenye kikosi cha kimataifa cha walinda amani Kaskazini mwa Afghanistan. Wanajeshi 1,200 kati ya hao wako mjini Kunduz.