1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

David Cameron afafanua malengo ya serikali yake.

Abdu Said Mtullya12 Mei 2010

Serikali mpya ya Uingereza yaahidi kupunguza nakisi.

https://p.dw.com/p/NMS7
Waziri Mkuu mpya wa Uingereza David Cameron na makamu wake Nick Clegg .Picha: picture-alliance/dpa

Waziri  Mkuu mpya wa  Uingereza David Cameron, kiongozi wa chama cha Conservative, leo  ameanza kazi kufuatia mapatano  ya kuunda serikali  ya mseto aliyofikia na kiongozi  wa   chama cha waliberali, Nick Clegg, hapo jana.

Serikali hiyo mpya inaingia  madarakani baada ya utawala  wa miaka 13 wa  chama cha Labour.

Pamoja na malengo   aliyofafanua ni kupunguza   nakisi ya bejeti  ambayo sasa imefikia  asilimia  zaidi  ya 11 ya pato  jumla la taifa.

Serikali ya waziri Mkuu David  Cameron  pia inatazamiwa  kuutekeleza mpango wa chama chake  wa  kupunguza   matumizi kwa kiasi cha  paundi Bilioni sita mnamo mwaka huu.

Waziri Mkuu mpya huyo amesema leo kwamba serikali ya mseto aliyoiunda na chama  cha Liberal Democrats  inadhamiria kuwapa watu wa  Uingereza uongozi  imara.

Akizungumza na waandishi   habari kwa mara ya kwanza  leo alasiri bwana Cameron pamoja na makamu wake, Nick  Clegg, alifafanua malengo ya serikali  yake.

Amesema lengo mojawapo kuu  ni kuipa Uingereza uongozi wenye nguvu, imara na wenye  dhamira  utakaohitajika  kwa muda mrefu.

Waziri Mkuu Cameron pia amesema mpango wa  kupunguza nakisi ya serikali ni  muhimu sana na kutokana na   umuhimu huo serikali yake mpya imethibitisha kuwa mpango wa kubana matumizi utatekelezwa  utakaookoa kiasi  cha paundi Bilioni sita mnamo mwaka huu.

Serikali hiyo mpya pia  itatekeleza mpango wa kupunguza idadi ya wakimbizi.

Bwana Cameron pia ameahidi kwamba ushirikiano baina ya vyama vya Conservative na  Liberal  Democratic  utadumu  kwa kipindi chote cha miaka  mitano ijayo.

Wakati huo huo, majina ya mawaziri wa serikali mpya  yameanza kutajwa ikiwa pamoja  na  la  waziri  wa   fedha George Osborne.

Mwandishi:Mtullya  abdu/AFPE/ZA.

Mhariri: Miraji Othman