1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Darmstadt tayari kuangushana na vigogo wa ligi

7 Agosti 2015

Darmstadt 98 imejiandaa kwa mchuano wa kwanza wa Bundesliga dhidi ya Hannover katika kile kitakachokuwa ni mpambano wao wa kwanza katika ligi kuu ya Ujerumani baada ya miaka 33

https://p.dw.com/p/1GBlD
Deutschland SV Darmstadt - Fans
Picha: picture-alliance/dpa/R. Holschneider

Darmstadt 98 imejiandaa kwa mchuano wa kwanza wa Bundesliga dhidi ya Hannover katika kile kitakachokuwa ni mpambano wao wa kwanza katika ligi kuu ya Ujerumani baada ya miaka 33.

Darmstadt ilipata kibali cha Bundesliga mwezi Mei baada ya kuishinda Sr Pauli goli moja kwa sifuri na kumaliza msimu pointi tano nyuma ya Ingolstadt, ambayo tayari ilikuwa imepata tikiti ya kurejea katika Bundesliga.

Wanaanza kampeni yao wiki ijayo Jumamosi Agosti 15 dhidi ya Hannover, waliomaliza katika nafasi ya 13 msimu uliopita. Kocha Dirk Schuster, beki wa zamani, amesema kila mchuano utakuwa changamoto mpya katika ligi kuu.

Katika uwanja wa klabu hiyo wa Bollenfalltor, ambao ulijengwa mwaka wa 1921, mshambuliaji Marco Sailer mwenye umri wa miaka 29, ambaye amecheza muda mrefu katika ligi ya daraja la tatu, anasema kitu cha msingi ni kufanya kazi kwa pamoja kama timu. "Sidhani kama unaweza kuuita kuwa ni mpango. Kilichochangia ni ushirikiano baina ya timu na mkufunzi. Kila mtu alifanya kazi kwa ushirikiano mzuri. Na tulikuwa na hisia za umoja katika siku ya kwanza. Na bila shaka tutayasherehekea mafanikio hayo. Hisia za kuwa pamoja zinaongezeka kila mara, imani ya kila mmoja inaongezeka na taswira hii yote imechangia pakubwa katika ukweli kwamba tulikuwa na mafanikio makubwa na tukasonga nafasi mbili juu".

Mashabiki wa klabu hiyo nao pia wana matumaini kuwa vijana wao watakuwa na msimu mzuri

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Iddi Sessanga