DAR ES SALAAM:SADC yakutana huku Morgan Tsvangirai akamatwa tena | Habari za Ulimwengu | DW | 28.03.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

DAR ES SALAAM:SADC yakutana huku Morgan Tsvangirai akamatwa tena

Viongozi kutoka mataifa ya kusini mwa Afrika wanakutana mjini Dar es Salaam nchini Tanzania hii leo kwa kikao maalum ili kuzungumzia matatizo ya kisiasa na kiuchumi yanayokabili nchi ya Zimbabwe vilevile Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Kikao hicho cha siku mbili kinacholeta pamoja mataifa 14 wanachama wa Jumuiya ya mataifa ya Kusini mwa Afrika SADC kinaandaliwa na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania.Mkutano huo unafanyika huku kukiwa na shinikizo kutoka jamii ya kimataifa kufuatia hali mbaya inayokumba nchi ya Zimbabwe inayotishia hali ya mataifa ya jirani.

Aidha mkutano huo unafanyika baada ya wafuasi wa upinzani nchini Zimbabwe kupigwa vibaya na polisi akiwemo kiongozi wa chama cha Movement For Democratic Change MDC vilevile mapigano yaliyozuka katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kati ya wafuasi wa kiongozi wa Upinzani Jean Pierre Bemba na wanajeshi wa serikali.

Wakati huohuo kiongozi wa upinzani Morgan Tsvangirai wa chama cha Movement for Democratic Change, MDC amekamatwa tena na polisi alipokuwa akijiandaa kwa mkutano na waandishi wa habari mjini Harare katika makao makuu ya chama chake.Mataifa ya magharibi yanazidi kumkashifu Rais Mugabe na uongozi wake unaokandamiza upinzani nchini Zimbabwe.Mataifa jirani ya Jumuiya ya SADC kwa upande wao hayajasema chochote tangu yote hayo kutokea.

Chama tawala cha ZANU-PF kilipanga kukutana hii leo ili kujadilia pendekezo la kuongeza muhula wake unaokamilika mwaka 2008 hadi 2010.Mkutano huo umeahirishwa hadi atakaporudi kiongozi huyo anayehudhuria kikao cha SADC cha leo mjini Dar es Salaam.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com