1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Daftari la wapigakura Kenya lina maiti 92,000

22 Juni 2017

Uchunguzi wa mwezi mmoja uliofanywa na kampuni ya mahisabu nchini Kenya iitwayo KPMG umebaini kuwa kuna majina 92,000 ya watu waliokwishafariki dunia katika daftari la sasa ya wapiga kura nchini Kenya.

https://p.dw.com/p/2fC9t
Kenyatta zum Sieger der Präsidentenwahl in Kenia erklärt
Picha: picture alliance/Photoshot

Ripoti hii ya kampuni ya KPMG inayatia doa maandalizi ya Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC) kabla ya uchaguzi mkuu na kuibua hofu iwapo tume hiyo iko tayari kuandaa uchaguzi mkuu ujao kwa njia ya haki na huru, zikiwa zimesalia chini ya siku sitini.

KPMG inapendekeza tume hiyo itowe maelezo kamili ya watu waliokufa kwa mujibu wa daftari la wapigakura la mwaka 2012 hadi mwaka 2016.

"Tumegundua kuwa kuna majina ya wafu 92, 277 ambayo wako kwenye sajili. Wafu wale wana Umri wa zaidi ya miaka 18. Majina yao na vitambulisho vyao vinafanana. Kwa hivyo jukumu la IEBC ni rahisi mno kuenda kuyaondoa majina 92,277 kwenye daftari la wapiga kura," anasema Gerald Kasimu wa KPMG.

Kwenye chaguzi za awali, upinzani nchini Kenya umekuwa ukidai kuibiwa kwenye matokeo ya uchaguzi mkuu na sasa IEBC ina kibarua cha ziada kutakasa jina lake ambalo huenda likatiwa doa na ugunduzi wa ripoti hiyo.

Kenia Wahlen Auszählung
Picha: SIMON MAINA/AFP/Getty Images

Idara ya Usajili Vifo inasema ina maelezo ya watu wengine 350,000 ambayo itawayasilisha IEBC, jambo ambalo anasema Kasimu wa KPMG kwamba inaifanya idadi ya majina ya watu waliokwishakufa kwenye daftari hilo kufikia 1,037,260.

Ripoti hiyo pia imefichua kuwa wapiga kura 5,427 hawana alama za vidole kwenye mashine za kielektroniki, huku maelezo ya wengine milioni 2.9 yakiwa na hitilafu.

Hata hivyo, mkuu wa IEBC, Ezra Chiloba, anawaondolea hofu Wakenya kuhusu ugunduzi huo, akisema kuwa majina yote ya watu waliokwishakufariki dunia yataondolewa.

"Kuna majina mengine ambayo tunatarajia kutoka Idara ya Usajili wa Umma. Tukipata ripoti hiyo tutaendelea kutoa majina."

Huku hayo yakiarifiwa, IEBC  inaanda kongamano la siku tatu na wadau mbalimbali kwa lengo la kujaribu matumizi ya teknolojia ya mitambo yao itakayotumika kwenye uchaguzi mkuu.

Kwa mara ya kwanza, IEBC ilifanikiwa kujaribu utendajikazi wa mitambo yao miezi miwili kabla ya uchaguzi mkuu kwa mujibu wa tume hiyo.

Mwandishi: Shisia Wasilwa/DW Nairobi
Mhariri: Josephat Charo