1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona huenda ikasababisha dharura ya madeni Afrika

Tatu Karema
25 Juni 2020

Ripoti mpya ya utafiti uliofanywa na taasisi kadhaa za kimataifa, inasema nchi nyingi za barani Afrika zinaweza kushindwa kulipa madeni yao kwa sababu ya kuongezeka kwa gharama ya malipo kutokana na sarafu dhaifu,

https://p.dw.com/p/3eJUO
Bildergalerie Kulturelle Gesichtsbedeckungen - Kenia
Picha: picture-alliance/ZumaPress/D. Sigwe

Utafiti huo umegundua kuwa mataifa mengi barani Afrika yanakabiliwa na hatari ya kudorora kwa chumi zao kutokana na mriupuko wa virusi vya corona. Matokeo ya utafiti huo yaliotolewa na taasisi ya masomo ya ulinzi,  taasisi ya sayansi ya biashara ya Gordon  na kituo cha hali ya kimataifa ya baadaye cha Frederick S Pardee, yameonesha kuwa gharama ya kulipa madeni na viwango vya riba tayari imeongezeka kufikia takriban dola bilioni 40 kwa mwaka kwasababu ya kushuka thamani kwa sarafu nyingi za mataifa ya Afrika.

Ripoti hiyo kwa jina''Vifo, madeni na fursa- athari za COVID-19 barani Afrika'' imewahimiza wakopeshaji na wawekezaji kuahirisha ama kufutilia mbali madeni ya bara Afrika kulisaidia kujikwamua baada ya athari za mripuko wa virusi vya corona.Mwaka 2020 pekee,  mataifa hayo yanakadiriwa kupoteza mapato ya dola bilioni 45 hali inayochangiwa kwa kiasi na janga la virus vya corona lakini pia kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta.

Uchumi wakadiriwa kudorora

Utafiti huo pia umeonesha kuwa ijapokuwa uchumi wa bara Afrika umekadiriwa kukua kwa zaidi ya asilimia 130, bara hilo kwasasa liko nyuma zaidi kwa ukadiriaji wa kadri wa kiuchumi wa asilimia 4.3 kutoka mwaka 2020-2040. Janga la virusi vya corona pia limewasababishia umaskini takriban waafrika milioni 12 na idadi hii huenda ikaongezeka kufikia milioni 26 kufikia mwaka 2021.

Kulingana na utafiti huo, karibu waafrika milioni 570 wamekadiriwa kuishi katika hali ya uchochole kufikia mwaka 2030 ijapokuwa janga hilo huenda likaongeza idadi hiyo kufikia milioni 631.

Jakkie Cilliers, mwanzilishi na aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya masomo ya ulinzi, ameiambia DW kwamba ugonjwa wa COVID-19 utakuwa na athari kubwa katika ukuaji wa bara la Afrika na huku ikilazimu kushughulikia athari za kiafya na vifo katika kipindi kifupi, hali hii inaonesha umuhimu wa kufanyia marekebisho chumi za mataifa ya bara hilo kwa ukuaji wa haraka zaidi.Hata hivyo, utafiti huo pia unaangazia siku njema za baadaye kwa uchumi wa Afrika iwapo serikali hazitategemea tu hatua za dharura kukabiliana na janga hilo na badala yake kuwa na malengo ya muda mrefu kwa kuwekeza raslimali zaidi katika sekta za afya na miundo mbinu ya kimsingi.