Conte aendelea kuiimarisha Chelsea
2 Novemba 2016Eden Hazard na Diego Costa walifunga mabao hao na kukinyanyua kikosi cha Antonio Conte hadi katika nafasi ya nne, pointi moja nyuma ya manchester City, Arsenal na Liverpool ambazo zina pointi sawa kilelele na kutenganishwa na wingi tu wa mabao.
Katika La Liga timu zinazocheza katika Europa League Villareal, Athletic Bilbao na Celta Vigo zote zilipata pigo Jumapili katika juhudi zao za kujiunga na mbio za kuwania ubingwa wa Uhispania.
Villareal iliangukia pua mbele ya Eibar kwa mabo 2-1 , Bilbao iliridhika na sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya mahasimu wao upande wa kaskazini mwa nchi hiyo Osasuna na Celta ilishikwa shati na kutoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya Las Palmas. Siku ya Jumamosi Barcelona ilidonoa Granada kwa bao 1-0 , wakati Alaves ilikandamizwa kwa mabao 4-1 dhidi ya Real Madrid, nayo Atletico Madrid ikaishindilia Malaga kwa mabao 4-2.
Ligi ya Ulaya inarejea tena uwanjani kesho Jumanne na Jumatano, ambapo Manchester City itakuwa nyumbani ikiisubiri Barcelona baada ya kipigo cha kudhalilisha cha mabao 4-0 katika uwanja wa Camp Nou katika kundi C wiki mbili zilizopita. Manchester City imepata pointi moja tu kutokana na michezo yake miwili ya Champions League iliyopita.
Ushindi wa tatu mfululizo wa kikosi cha Barcelona kutoka katika jimbo la Catalan unatkuwa na maana kwamba watahitaji sare tu katika mchezo unaofuatia kujihakikishia tikiti yao katika awamu ya mtoano. katika kundi hilo Borussia Moenchengladbach inaikaribisha nyumbani Celtic Glasgow , ambapo katika mchezo wa kwanza baina ya timu hizo , Gladbach ilipata ushindi muhimu wa mabao 2-0 ugenini. Bayern Munich ni wageni wa PSV Eindhoven na Atletico Madrid iko nyumbani ikiisubiri Ristov ya Urusi katika kundi D.
Paris St. Germain ina miadi na basel ya Uswisi na Arsenal iko nyumbani kwa Ludogorets Razgrad ya Bulgaria katika mchezo wa kundi A ambalo linaoongozwa na Arsenal ikifuatiwa na PSG.
Mabingwa wapya wa Champions League barani Afrika Mamelodi Sundowns walionya kipigo cha mabao 2-1 jana katika ligi ya Afrika kusini dhidi ya Cape Town City na inabakia mkiani mwa ligi hiyo siku saba baada ya kutawazwa mabingwa wa Afrika. Jua kali , mipango ya haraka haraka ya mchezo huo na sherehe za baada ya ushindi vilionekana kuathiri kwa kiasi kikubwa mmchezo wa mabingwa hao wa Afrika na Cape Town City wangeshinda kwa mabao mengi kutokana na kutengeneza nafasi nyingi za mabao.
Mbio za magari.
Dereva Muingereza Lewis Hamilton ameshinda mbio za magari za Mexico Grand Prix na kuendeleza mbinyo dhidi ya dereva mwenzake wa magari ya Mercedes Nico Rosberg katika mvio za Formula one zilizofanyika nchini Mexico jana Jumapili.
Na kwa taarifa hiyo nasema sina la ziada na nakutakia jioni njema , jina langu ni Sekione Kitojo , kwaherini.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre
Mhariri: Yusuf saumu