1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Condoleza Rice kuwasili Ethiopea kwa ajili ya amani pembe ya Afrika

5 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/CXEd

ADDIS ABABA.Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleza Rice anatarajiwa kuwasili nchini Ethiopea asubuhi hii katika hatua za kujaribu kutafuta suluhu za mizozo kwenye eneo hilo la pembe ya Afrika.

Condoleza Rice anatarajiwa kuwa na mazungumzo na viongozi wa serikali ya mpito ya Somalia mjini Addis.

Hata hivyo Rais Abdullaye Yusuf Ahmed atashindwa kuwa na mkutano na waziri huyo wa Marekani kutokana na kuumwa.

Rais huyo wa serikali ya mpito ya Somalia amelazwa katika hospitali moja jijini Nairobi ambapo hali yake inaelezwa kuwa mbaya.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 72 amekuwa akisumbuliwa na maradhi ya kutetemeka na afya yake imekuwa ikidhofu kila siku.

Wakati huo huo Serikali ya Somalia imezuia shughuli zote za misaada katika eneo la kusini mashariki mwa nchi hiyo ambalo limeathiriwa zaidi na mizozo ya kibinaadamu inayoendelea nchini humo.

Vikwazo hivyo ni pamoja na kuzuia ndege zote za misada ya kibinaadamu kutua katika eneo hilo la Shabelle na pia inazuia meli ya msaada wa chakula kupakua shehena hiyo.