Condoleezza Rice ahimiza kusuluhisha mgogoro wa Wakurd | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.11.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Condoleezza Rice ahimiza kusuluhisha mgogoro wa Wakurd

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani,Condoleezza Rice anaehudhuria mkutano nchini Uturuki kuhusu mgogoro wa Wakurd amesema,ataiomba Uturuki isihatarishe usalama kaskazini mwa Irak,kwa kuwashambulia waasi wa Kikurd katika eneo hilo la mpakani.

Waziri Condoleezza Rice alipokuwa njiani kuelekea Uturuki aliwambia waandishi wa habari waliofuatana nae katika ndege,hatua yo yote ile itakayochafua usalama kaskazini mwa Irak haitokuwa kwa maslahi ya Uturuki wala Irak.Kwa hivyo anaihimiza Uturuki iwe na uvumilivu.

Suala muhimu atakalosisitiza wakati wa majadiliano yake pamoja na Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan,Rais Abdullah Gul na Waziri wa Nje Ali Babacan mjini Ankara ni kuwa Uturuki,Marekani na Irak zote zina adui mmoja yaani PKK akimaanisha chama cha waasi wa Kikurd.

Condoleezza Rice amesema,wakati wa majadiliano yake pamoja na viongozi wa Uturuki,wanatazamia kuzindua mkakati utakaosaidia kukabiliana na kitisho cha Uturuki,lakini bila ya kuichafua zaidi hali iliyopo.

Juma lililopita Bibi Rice alizungumza kwa simu na kiongozi wa Kikurd wa Iraq,Massud Barzan na alieleza waziwazi umuhimu wa kujitenga na chama cha PKK.Amesema,amehakikishiwa kuwa serikali ya Irak ya Kaskazini,haina azma ya kuwaficha wanamgambo wa PKK bali yadhamiria kuzuia ugaidi katika eneo hilo linalopakana na Uturuki.Hata Iran iliyoombwa na Irak kusaidia kuutenzua mgogoro huo,imempeleka waziri wake wa mambo ya nje,Manouchehr Mottaki.

Hii leo na kesho Jumamosi,mjini Istanbul, Condoleezza Rice,Manouchehr Mottaki,Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon na Waziri Mkuu wa Irak,Nuri al-Maliki watahudhuria mkutano wa mawaziri kutoka nchi jirani za Irak na madola makuu ya Magharibi.

Uturuki inaituhumu serikali ya Wakurd kaskazini mwa Irak kuwa inatoa hifadhi na misaada kwa wanamgambo wa PKK na imetishia kuchukua hatua ya kijeshi dhidi ya wanamgambo hao.Lakini Baghdad na Washington zinapinga vikali zikisema,mashambulizi ya aina hiyo yatavuruga eneo pekee la utulivu katika nchi iliyoteketezwa kwa vita.

Chama cha PKK hutumia eneo la milimani kuvuka mpaka na kuishambulia Uturuki kutoka kaskazini mwa Irak.Hiyo ni sehemu ya kampeni ya Wakurd wanaotaka kujitawala katika eneo lenye Wakurdi wengi,kusini mashariki mwa Uturuki.

Uturuki,Marekani na baadhi kubwa ya jumuiya ya kimataifa hukihesabu chama cha PKK miongoni mwa makundi ya kigaidi.Zaidi ya watu 37,000 wamepoteza maisha yao tangu kuanza kwa uasi wa PKK mwaka 1984.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com