1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yapongezwa kwa ushirikiano na timu ya WHO Mjini Wuhan

Tatu Karema
4 Februari 2021

Mmoja wa wataalmu wa timu ya Shirika la Afya Duniani WHO walioko mjini Wuhan nchini China kuchunguza chanzo cha virusi vya corona Peter Daszak, amesema kuwa serikali ya China imetoa ushirikiano wa kiwango cha juu.

https://p.dw.com/p/3orgI
China | Coronavirus | WHO Experten in Wuhan
Picha: Thomas Peter/REUTERS

Katika ujumbe kupitia ukurasa wa twitter, Daszak ambaye pia ni  mtaalamu wa masuala ya wanyama, alipongeza mkutano wa jana Jumatano kati yao na wafanyakazi wa taasisi kuu ya elimu ya virusi ya Wuhan ikiwa ni pamoja na naibu mkurugenzi wake Shi Zhengli aliyefanya kazi na Daskaz kufuatilia chanzo cha virusi vya SARS vilivyotokea nchini China na kusababisha mripuko wa mwaka 2003:

Taasisi hiyo ya virusi ya Wuhan, imekusanya sampuli nyingi za virusi hatua inayosababisha kutolewa kwa madai ambayohayajathibitishwa kwamba huenda ilisababisha mripuko huo kwa kuvuja kwa virusi hivyo katika jamii iliyoko karibu. China imekanusha vikali uwezekano huo na kutoa nadharia ambazo hazijathibitishwa kwamba huenda virusi hivyo vilianzia kwengineko. Kundi hilo la waatalamu wa WHO linalojumuisha wataalamu kutoka mataifa 10 limefanya ziara katika hospitali, taasisi za utafiti na soko moja linalohusishwa na chanzo cha mripuko wa virusi vya corona.

Wakati huo huo, maelfu ya aina mpya ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Covid -19 vimerekodiwa huku vikijibadilisha na kujumuisha vile vinavyojulikana kama aina mpya ya virusi vya Uingereza, Afrika Kusini na Brazil vinyavyoonekana kuenea kwa haraka kushinda aina nyingine ya virusi .

Oxford I AstraZeneca COVID-19 Impfung
Dosi ya chanjo ya Oxford/AstraZenecaPicha: Jason Cairnduff/REUTERS

Zahawi amekiambia kituo cha habari cha Sky kwamba hakuna uwezekano mkubwa kwamba chanjo za sasa zitakosa kufanya kazi dhidi ya aina hiyo mpya ya virusi hasa inapokuja katika suala la ugonjwa mkali na kulazwa hospitalini. Amesema kuwa kampuni zote za kutengeneza chanjo , Pfizer- BioNTech, Moderna, Oxford-AstraZeneca na nyinginezo zinatafuta jinsi zinavyoweza kuimarisha chanjo zao kuhakikisha ziko tayari kwa aina yoyote mpya ya virusi. Kulingana na Jarida la matibabu la Uingereza, huku maelfu ya aina mpya ya virusi vikijitokeza wakati virusi vinapojibadilisha, ni vichache ambavyo huenda vikawa muhimu na kukibadili kirusi hicho katika njia inayothaminika.

Huku hayo yakijiri jopo kazi la ikulu ya White House nchini Marekani linaloshughulikia janga la virusi vya corona, jana  limesema kuwa  visa vya maambukizi ya virusi vya corona nchini humo vinaonekana kupungua  huku utawala wa rais Joe Biden ukiwa na matumaini kwamba unaweza kufikia malengo yake ya kutoa chanjo milioni 100 katika siku 100. Hata hivyo mkurugenzi wa vituo vya kuzuia na kuthibiti magonjwa Rachel Walensky ameonya kuwa aina mpya ya virusi vya corona inayojitokeza nchini humo huenda ikaathiri ufanisi huo.