1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

China na Marekani zalaumiana katika mkutano wa shirika la kimataifa la biashara, WTO

Mkutano WTO ulifunguliwa jana mjini Geneva, Uswisi na ulianza na mazungumzo baina ya China na Marekani.

Waziri wa biashara wa China, Chen Deming

Waziri wa biashara wa China, Chen Deming

Kila nchi imekuwa ikimlaumu mwenzake kwamba ndiye aliyosababisha mazungumzo ya biashara yaliyofanyika miaka 10 iliyopita mjini Doha, Qatar, kutokuleta muafaka.

Waziri wa biashara wa China, Bwana Chen Deming, na mwenzake wa Marekani, Bwana Ron Kirk, waliutumia mkutano wa Geneva kulaumiana. Kirk alisema kwamba shirika la kimataifa la biashara, WTO, bado halijafanikiwa kugawanya wajibu kati ya nchi zenye mafanikio zaidi. Aliendelea kusema kwamba pamekuwa na mabadiliko mengi sana duniani tangu kufanyika kwa mazungumzo huko Doha, Qatar, miaka 10 iliyopita, lakini mazungumzo ya sasa hayaendi sambamba na mabadiliko yaliyotokea.

Kukua kwa uchumi wa nchi nyingi, hasa ule wa China, kumefanya mazungumzo yaliyofanyika Doha kutokuwa na uzito tena. Kusudi la kuanzishwa kwa soko huria la biashara lilikuwa kuziwezesha nchi zinazoendelea kukua lakini sasa nchi hizo, mojawapo ikiwa China, zimekuwa mabingwa wa biashara, na hivyo swali linazuka kama kuna haja ya kuendelea kuzisaidia nchi hizo.

Lakini China pamoja na nchi nyingine zinazoendelea hazijakata tamaa kuhusu maamuzi yaliyofanywa Doha. Waziri wa biashara wa China, Deming, amesema mazungumzo yanayoendelea sasa yanakwamishwa na maandalizi ya uchaguzi wa Marekani, na hivyo inafaa yasimamishwe na kuendelezwa mwakani. "Ninafahamu kwamba matatizo yaliyopo sasa hayakusababishwa na mgogoro wa kifedha pekee yake," alisema Deming. "Yamesababishwa pia kwa sababu kuna nchi ambazo zinatarajia kufanya uchaguzi hivi karibuni, na hivyo viongozi wao hawako tayari kubadili mawazo yao."

Mkurugenzi wa shirika la WTO, Pascal Lamy

Mkurugenzi wa shirika la WTO, Pascal Lamy

Naye Mkurugenzi wa shirika la WTO, Pascal Lamy, alisema yapo mambo yanayozuia shirika hilo kufanya kazi ipasavyo.

"Tunahitaji mazingira mazuri ya kufanyia biashara. Tungeweza kuwageuza wapiga kura wengi wanaopinga soko huria," alisema Mkurugenzi huyo. "Jambo la msingi ni kuwapo kugawanya sawa kipato. Kutokowapo na usawa kati ya nchi moja na nyingine au kati ya makundi mbali mbali yanayoishi katika nchi moja, kunawafanya watu wengi kutokuwa na imani na soko huria."

Wakati huo huo, shirika la WTO lilipitisha mkataba wa kupokea maagizo ya bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani billioni 100. Lamy alisema hiyo ni hatua kubwa kwa nchi mwanachama wa WTO na biashara ya kimataifa kwa ujumla.

Mkutano wa Geneva ulifunguliwa jana na unatarajiwa kumalizika kesho.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/RTRE

Mhariri: Othamn Miraji