1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CHANJO YA MALARIA ITAPATIKANA

Christopher Buke26 Oktoba 2006

Hii ni baada ya jopo la utafiti wa chanjo ya malaria kutathmini hatua zilizokwisha fikiwa.

https://p.dw.com/p/CHmG

Mtandao wa kupambana na ugonjwa wa malaria barani Africa AMANET wenye makao yake makuu nchini Tanzania umesema kuwa chanjo ya ugonjwa sakili wa malaria ipo mbioni kupatikana.

Hii ni baada ya jopo la watafiti wa chanjo hii kutoka pande nne za dunia hasa barani ulaya Marekani, nchi za Nordic na Barani Afrika kukutana nchini Tanzania katika mji wa kihistoria wa Bagamoyo kutathmini kipi wamefikiwa hadi sasa.

Mkutano huu ulioendeshwa na AMANET unasema kimsingi chanjo kadhaa zimeisha patikana lakini zinafanyiwa majaribio kadha wa kadha kabla ya kusonga mbele.

“ …… hiyo inatupa matumaini lakini hizi chanjo lazima zipitie katika ngazi mbalimbali na ngazi za kisayansi ngazi za maadili ngazi za kuweza kuingiza hiyo chanjo katika jamii”, anasema Profesa Wen Kilama ambaye ni Managing Trustee wa AMANET.

Ikiwa chanjo hii itathibitishwa na kuanza kutumika ni habari njema kwa walimwengu lakini zaidi wakazi wa Afrika ambao malaria sio tu imewaua watoto, wazazi na ndugu zao lakini pia imewaacha katika dimbwi la umasikini.

Katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara inakadiriwa kuna kadhia za ugonjwa huu kadiri milioni 500. Na tena mtoto mmoja hufa katika kila sekunde 20.

Wahanga wakubwa wa malaria ni watoto wenye umri wa nchini ya miaka 5, wanawake wajawazito zaidi sana ambao ni mara yao ya kwanza kupata uja uzito, na makundi yanayohama-hama kama vile wakimbizi.

Kwa mjibu wa Shiria la Afya Ulimwenguni WHO, Chuo kikuu cha Harvard na chuo kimoja nchini Uingereza kama sio ukatili wa ugonjwa wa malaria pato la GDP katika Afrika lingekuwa limepanda hadi dola za kimarekani bilioni 100 mwaka 2000 endapo ugonjwa huo ungekuwa umeangamizwa miaka 35 iliyopita.

Wataalamu wanaasa kuwa ugonjwa huu unarudisha nyuma ukuaji wa uchumi kwa asilimia 1.3 kwa mwaka barani Afrika.

Nchini Tanzania pekee watoto 12,000 hufa, kutokana na malaria kila baada ya siku nne, wakati watoto milioni 5, hupata maabukizo mapya kila mwaka.

Katika kila watu 40 ambao hutibiwa katika hospitali nchini Tanzania bila kulazwa 25 huwa wanasumbuliwa na malaria.

Kwa mujibu wa utafiti wa Benki ya dunia wa mwaka 1994, malaria huigharimu Tanzania dola milioni 120, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 120 pesa za kitanzania, kupitia nguvu kazi, ambayo ni sawa na asilimia 3.4 ya pato la Taifa GDP.

Nchini Uganda kadiri watu 79,000 hufa kila mwaka kutokana na malaria theluthi mbili kati ya hao wakiwa watoto wenye umri wa nchini ya miaka 5.

Ndio maana Profesa Kilama anasema kupatikana kwa chanjo hiyo kumestahiki kupokelewa kwa mikono miwili. “ mtakumbuka kwamba miaka ya nyuma ugonjwa wa malaria ulikuwa ugonjwa wa kawaida, kadiri miaka ilivyopita tumekuwa na usugu kuanzia dawa za qroloquine badae ukaja usugu kwa dawa SP”.

Anasema hali imefikia kuwa vimelea vya malaria havisikii chochote kwa sehemu zilizo nyingi mpaka kutumia mchanganyiko wa madawa ujulikanao kama SCTL.

Nilimdadisi mtaalamu huyu hasa nikitaka kupata undani wa ikiwa kweli chanjo ya malaria, ugonjwa mbaya sana barani Afrika inamatumaini kupatikana. “ chanjo inaweza ikapatikana”, alinisisitizia msomi huyo.

Kama walivyonena wahenga kuwa ndege mjanja hunasa kwenye tundu bovu ndivyo ilivyotokea kwa vimelea vya malaria. Japo vimekuwa mara vijijengee usugu dhidi ya madawa, wataalamu hao wanasema wamegundua kuwa mtu anayeshambuliwa mara kwa mara na malaria mwili wake hujijengea usugu dhidi ya vimelea hivyo. Na hiki hasa ndicho kiliwaongoza watafiti hawa kugundua chanjo hii.

“kuna chembe chembe zinazoonyesha kwamba hawa watu wana kinga asilia ya malaria na hii kinga inatokana na kupata maambukizo ( ya mara kwa mara ya malaria)” anadokeza Profesa na kuongeza

“ Kadiri unavyopata maambukizi ya malaria ndio kadiri unavyokuwa na hiyo kinga na …..ndio sisi ….tunatumia kwamba ni chanzo cha kuanza kufanya shughuli kama hii”.

Kitakacho wafanya walimwengu hasa wana wa Africa waendelee kunyong’onyea ni kwa vile watafiti wananadi chanjo hii haiweza kuanza kutumika kabla ya kipindi cha muda wa miaka 5 kuanzia sasa.

“ tuseme itakuwa kama miaka mitano hivi ijayo tunaweza au sita saba ijayo tunaweza tukasema aah hapa afadhali lakini katika zile ngazi za kwanza tunazo chanjo ambazo sasa hivi tunazishughulikia”.

Juhudi hizi za ugunduzi na utafiti wa chanjo ya malaria zilianza kwenye miaka ya 1990 baada ya Kamisheni ya Ushirikiano wa Kimataifa ya Ulaya Katika Utafiti kwa kushirikiana na nchi zinazoendelea INCO DC kupanua wigo wa utafiti juu ya chanjo ya malaria.

Ili kufanikisha mkakati huu yalianzishwa mashirika na vikundi vya kiutafiti kama vile AMVTN sasa ikijulikana kama AMANET na VINCOMAL.

Juhudi hizi zilizidi kushika kasi pale zaidi ya watafiti 81 kutoka Bara la Afrika, Ulaya na Marekani walipokutana mjini Arusha Tanzania mwezi wa February 1995 kuongeza kasi ya kupatikana chanjo ya malaria.

Mwisho.