1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Champions League:Schalke 04 kuwavaa Inter Milan

4 Aprili 2011

Robofainali ya ligi ya mabingwa Ulaya Champions League inaanza kwa mechi mbili, Jumanne hii

https://p.dw.com/p/10nMm
Raul kuongoza safu ya ushambuliaji ya Schalke 04Picha: dapd

Katika mechi hizo,Schalke 04 inayopepesuka katika Bundesliga itakuwa mjini Milan kuumana na Inter, mechi ambayo Schalke itashuka dimbani bila ya Mario Gavranovic na Peer Kluge, huku wasiwasi wa kuweza kuvaa njumu ukiwepo kwa Christoph Metzelder na Klaas Jan Huntelaar.

Schalke inakamata nafasi ya 11 katika msimamo wa ligi ya Bundesliga.

Hata hivyo katika michuano ya Ulaya Schalke imeonesha kandanda na ari ya juu tofauti na kiwango chao katika ligi ya nyumbani Bundesliga.

Lakini kocha Inter mbrazil Leonardo amepuuza kiwango hicho cha chini cha Schalke katika Bundesliga akisema ni timu inayotisha.Inter Milan kwa upande wao mwishoni mwa wiki walichapwa mabao 3-0 na mahasimu wa AC Milan katika ligi ya Italia.

Kocha huyo hajawahi kuiongoza timu ya Italia na kushinda mechi nyumbani katika michuano ya ligi ya mabingwa.

Katika mechi tano alizoongoza nne akiwa na AC Milan na moja na Inter ambayo ndiyo anayoifundisha hivi sasa, hakuwahi kushinda hata mechi moja.Lakini hilo halimpi shaka.

Leonardo atalazimika kutatua tatizo la ngome yake ambayo imeonekana kuwa na matundu.Hata hivyo kurejea kwa Lucio aliyekuwa akitumikia adhabu kufungiwa huenda kukaimarisha ngome yake.

Inter Milan iliwatoa mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich na sasa Schalke wanajiwinda kutaka kuwafuta machozi wajerumani kwa kulipiza kisasi na kuwatoa Inter.

Timu hizi mbili zimewahi kukutana mara nne katika michuano ya kombe la UEFA, ambapo Inter imeshinda mechi mbili na Schalke mechi moja huku nyingine ikimalizika kwa sare.

Schalke katika mechi saba ilizocheza na timu kutoka Italia imeshinda mechi moja tu, na mwaka 2008 ilikaribia kufikia hatua hii ya robofainali lakini ikafungwa bao 1-0 nyumbani na ugenini na Barcelona.

Katika mechi nyingine, hii leo Real Madrid itakuwa nyumbani mjini Madrid kuwakaribisha Tottenham Hotspur ya Uingereza.Real wanaofundishwa na Jose Morinho ´´the special one´´ itaingia uwanjani ikiwa na kidonda cha kupigwa ngwala katika mechi za ligi ya nyumbani mwishoni mwa wiki ilipofungwa bao 1-0 na Sporting Gijon.

Hii ni mara ya kwanza kwa Real kufika hatua hiyo ya robofainali tokea mwaka 2004.Real na Tottenham zimewahi kukutana mara mbili tokea mwaka 1985 ambapo Real Madrid walishinda.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters/AFP

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman