1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga yapata mshtuko refa ajaribu kujiua

Sekione Kitojo21 Novemba 2011

Refa wa ngazi ya juu wa Ujerumani Babak Rafat amejaribu kujiua kabla ya mchezo ambao alikuwa ausimamie kati ya FC Koln na Mainz 05. Wakati huo huo Augsburg imesalia mkiani mwa Bundesliga.

https://p.dw.com/p/13ERy
Ni pambano kati ya Stuttgart na FC Kaiserslautern katika bundesliga.Picha: picture-alliance/dpa

Tukianza na Bundesliga, Augsburg iliyopanda daraja msimu huu imekwama mkiani mwa ligi hiyo baada ya jana Jumapili kupigwa mwereka wa mabao 2-1 mbele ya VFB Stuttgart wakati ligi hiyo ya Bundesliga bado imo katika mshutuko baada ya jaribio la kujiua lililofanywa na mwamuzi wa ngazi ya juu nchini Ujerumani.

Hamburg SV ilifanikiwa kumtupia mawe bundi aliyekuwa amejikita katika paa lake kwa muda mrefu wa msimu huu pale walipoishinda Hoffenheim kwa mabao 2-0 jana Jumapili na kupanda ngazi kuondoka katika eneo la kushuka daraja na kumpatia kocha Thorsten Fink ushindi wake wa kwanza tangu kuanza kuiongoza klabu hiyo.

Tuliamini kuwa tunaweza na tulipambana, Finki amesema baada ya ushindi huo. Wachezaji wa Hamburg walirukaruka na kucheza mbele ya mashabiki wao firimbi ya mwisho ilipolia baada ya kupata ushindi wao huo wa kwanza nyumbani katika majaribio kumi tangu pale timu hiyo iliposhinda kwa mabao 6-2 dhidi ya FC Kolon Machi mwaka huu. Hamburg ambayo imekuwa ikining'inia mkiani kwa muda mrefu tangu kuanza msimu huu haijafungwa tangu pale Fink alipoanza kuifunza timu hiyo Oktoba 17.

Lakini michezo ya mwishoni mwa juma ya Bundesliga iliingia dosari kutokana na jaribio la kujiua lililofanywa na refa Babak Rafat, mwenye umri wa miaka 41, ambaye aligunduliwa akiwa bafuni katika chumba cha hoteli alimofikia mjini Cologne na refa msaidizi wake akiwa amejikata mshipa wa damu mkononi.

Rafati anatibiwa katika hospitali mjini Kolon, lakini jaribio lake la kujiua linakuja miaka miwili baada ya golikipa wa timu ya taifa ya Ujerumani, Robert Enke kujiua na taarifa hizo zimewashtua wengi wa wapenzi wa soka hapa Ujerumani

Rais wa shirikisho la soka la Ujerumani DFB, Theo Zwanziger ameeleza kushtushwa kwake siku ya Jumamosi.

Babak Rafati
Refa wa bundesliga Babak RafatiPicha: picture alliance/ZB

Sifahamu nini la kusema kuhusiana na hali hii na naweza kuwaambia tu , kwamba mbinyo kwa waamuzi wetu kutokana na sababu mbali mbali ni mkubwa mno.

Ni rais wa shirikisho la kandanda nchini Ujerumani Theo Zwanziger, akizungumza na waandishi habari baada ya kupata taarifa kuhusu jaribio hilo la kujiua lililofanywa na mwamuzi huyo Babak Rafat. Mkurugenzi wa spoti wa klabu ya soka la FC Kolon ,ambayo ilikuwa jioni hiyo ya Jumamosi ikumbane na Mainz 05, Volker Finke alisema.

Kati ya saa nane na saa nane na robo tulipata taarifa kuwa kuna ajali imetokea kuhusiana na mwamuzi wa mchezo wetu.

Kutokana na tukio hili mchezo hautafanyika na hakuna uwezekano wa kufanya vinginevyo. Huu si uamuzi wa FC Kolon ama Mainz , timu zote mbili zinazungumza, kuhusiana na suala la mchezo huu.

Mchezo kati ya Kolon na Mainz ambao Rafat alikuwa awe refa ulifutwa dakika 40 kabla ya kuanza, lakini michezo mingine iliendelea.

Borussia Dortmund ilishikilia nafasi ya pili kutokana na kuwa na mabao mengi ya kufunga baada ya Borussia Moenchengladbach kuipa kipigo cha mbwa mwizi Werder Bremen cha mabao 5-0 na kujiunga na Dortmund katika nafasi ya points 26, wakati Bayern Munich ikiwa na points 28.

Kama alivyo Mario Goetze, Marco Reus ni mmoja kati ya vijana chipukizi nyota wa Ujerumani ambao wanakuja kwa kasi ya ajabu na mabao yake matatu dhidi ya Werder Bremen siku ya Jumamosi yamemfanya kuwa na mabao saba hadi sasa aliyoweka wavuni katika michezo mitatu ya ligi na kufukisha mabao 10 katika msimu huu. Manchester City na Bayern Munich ni timu mbili ambazo zinatamani kumsajili chipukizi huyo.

Schalke 04 ilipanda hadi nafasi ya nne baada ya ushindi dhidi ya Nuremberg na Hannover iliangukia pua pale ilipopata kisago cha mabao 4-1 dhidi ya Wolfsburg. Hertha BSC Berlin ilitoka sare ya mabao 2-2 na Freiburg na Bayer Leverkusen ilikuwa mshindi dhidi ya Kaiserslautern kwa mabao 2-0.

Manchster City imeendelea kutamba katika ligi ya daraja la kwanza nchini Uingereza, Premier League ikiweka mwanya wa points tano kwa ushindi wa mabao 3-1 nyumbani dhidi ya Newcastle United. Mabingwa watetezi Manchester United iliendelea kuweka mbinyo kwa viongozi wa ligi hiyo majirani zao Manchester City kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Swansea City iliyopanda daraja msimu huu.

Chalsea iliteleza na kupata kipigo chake cha pili mfululizo nyumbani wakati goli la dakika ya 78 la Glen Johnson liliipa ushindi Liverpool wa mabao 2-1.

Naye kocha wa Chelsea, Andre Villas-Boas, amepinga maelezo kuwa kiti chake kama meneja wa Chelsea kimo hatarini na kusisitiza kuwa anaungwa mkono kwa kiasi kikubwa na mmiliki wa timu hiyo, Roman Abramovich, licha ya kipigo cha jana Jumapili dhidi ya FC Liverpool.

Wakati huo huo Meneja wa Tottenham Hotspurs Harry Redknapp amesema kuwa anatarajia kuwa katika benchi la ufundi la timu hiyo leo Jumatatu wakati wa mchezo na Aston Villa uwanjani White Hart Lane.

Huko Hispania vigogo vya soka nchini humo Real Madrid na FC Barcelona vimeendelea kupata ushindi, wakati viongozi wa ligi Real Madrid walipata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Valencia na Barca iliipa kipigo Real Zaragoza cha mabao 4-0.

Ushindi huo wa Real Madrid umeweka mwanya wa points tatu dhidi ya mahasimu wao Barcelona ambayo iko nafasi ya pili.

Na huko Ufaransa Paris St Germain ilipata kipigo chake cha kwanza katika ligi ya nchi hiyo katika muda wa miezi mitatu wakati ilipokubali bao 1-0 nyumbani dhidi ya Nancy jana Jumapili. Olympique Lyon nayo ilisalimu amri kwa mara ya kwanza nyumbani katika muda wa mwaka mmoja wakati ilipokubali kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Stade Rennes. Olympique Marseille ilishindwa kuhimili vishindo vya Montpellier na kuonja kipigo cha bao 1-0. Licha ya kipigo hicho Olympique Marseille inashikilia bado nafasi ya pili katika ligue 1.

Baada ya wiki ya mtafaruku uliosababishwa kwa kiasi kikubwa na matamshi ya rais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA , Sepp Blatter juu ya ubaguzi wa rangi katika michezo , shirikisho la kandanda katika bara la ulaya UEFA litakuwa na matumaini kuwa kinyang'anyiro wiki hii cha michuano ya champions League kitakuwa kivutio katika vyombo vya habari wakati michuano hiyo inafikia hatua yake ya kufa na kupona. Mabingwa wa zamani wa champions League Manchester United , Bayern Munich, Inter Milan na Ajax Amsterdam watataka kukamilisha azma yao ya kukata tikiti zao katika timu 16 bora na kujiunga na Real Madrid, AC Milan na mabingwa watetezi Barcelona katika duru hiyo ya mtoano.

Arsenal London, Manchester City na Chelsea zinaweza pia kukata tikiti zao mchezo mmoja kabla ya kukamilika kwa duru hii wakati timu ya APOEL Nicosia itakuwa timu ya kwanza kutoka Cyprus kufikia katika timu 16 bora barani Ulaya iwapo itaishinda Zenit St Petersburg.

Nafasi ya kuingia 16 bora bado ziko wazi katika makundi mengine saba kati ya nane. Ni kundi H pekee ambalo tayari limepata wawakilishi wake, ambapo Barcelona na AC Milan tayari zimefuzu.

Napoli na Manchester City zinakutana katika kundi A mjini Sao Paolo kesho Jumanne, zote zikilenga kusonga mbele, wakati viongozi wa kundi hilo Bayern Munich wana uhakika wa kukata tikiti yao kwa ushindi dhidi ya Vilareal ya Hispania nyumbani.

Chelsea inakumbana na Bayer Leverkusen ya Ujerumani ikiwa na uhakika wa kukata tikiti yake kufikia katika kundi hilo la timu 16, na Arsenal inakumbana na upinzani pia kutoka Ujerumani wakati Borussia Dortmund ikisafiri kwenda mjini London kwa pambano hilo na wenyeji wanaweza kujikuta katika timu 16 bora iwapo watapata ushindi.

Na hadi hapo ndio tunafikia mwisho wa kuwaletea habari za michezo, kwa leo , jina langu ni Sekione Kitojo, hadi mara nyingine kwaherini.

Mwandishi : Sekione Kitojo / ape / rtre / dpa

Mhariri : Josephat Charo.