1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bundesliga uwanjani leo

15 Aprili 2008

Bayern munich ina miadi leo na Frankfurt kuania pointi 3 nyengine kabla jumamosi hii kucheza finali ya kombe la DFB na Dortmund.

https://p.dw.com/p/DiU9

Kabla ya finali ya jumamosi hii ya kombe la shirikisho la dimba la Ujerumani-DFB Pokal,Bundesliga-Ligi ya Ujerumani inarudi leo jioni uwanjani kwa mapambano 5 .

Munich iliofungua mwanya wa pointi 9 kileleni, ina miadi leo na Eintracht Frankfurt .Mpambano huu unafuatia ushindi wa Munich maridadi ajabu mwishoni mwa wiki walipoikongoa meno Borussia Dortmund kwa kuichapa mabao 5-0. Ushindi mwengine leo huko Frankfurt,utapiga msumari wa mwisho katika jeneza la watetezi wengine wa taji la Bundesliga msimu huu na kuzusha shangwe na shamra shamra mjini Munich.

Bayer Leverkusen ambayo hadi majuzi ikifukuzia Munich kileleni baada ya Bremen kusalim amri, ina miadi na Armenia Bielefeld.Mabingwa Stuttgart ambao karibuni wamekuwa wakija kwa meno ya juu, wanatamba nyumbani leo wakicheza na Nüremberg.Borussia Dortmund inafuta machozi ya msiba wa mabao 5 nyumbani inapocheza na hannover 96.Duisburg ina miadi na karlsruhe.

Wakati bayern munich ina miadi na Borussia Dortmund jumamosi mjini Berlin kwa finali ya kombe la taifa, AS Roma ya Itali inapambana leo na Catania katika nusu-finali ya kwanza ya kombe kama hilo nchini Itali.Nusu-finali yapili ni kati ya Inter Milan na Lazio Roma.Ufaransa wao wako katika hatu ya robo-finali ya kombe hili: Leo ni zamu ya Girondins Bordeaux kutoana na Sedan Ardennes wakati Paris St.Germain wana kibarua cha kuitimua nje Carquefou.

Taarifa kutoka premier League-Ligi ya uingereza inasema,mlinzi mashuhuri wa Manchester united Rio Ferdinand amekubali kurefusha mkataba wake na Manchester United.Kwa muujibu wa mkataba huo mpya,Ferdinand atavuna dala 260,000 kwa wiki.

Mwishoe, michezo ijayo ya Olimpik:jiji la Beijing,limeandaa sherehe kubwa kabisa za kitamaduni wakati wa michezo ya Olimpik hapo august.Maalfu ya wanasanaa wakishiriki katika tafrija mbali mbali.

Wanamuziki,waimbaji na wachezangoma kutoka China na sehemu nyengine za ulimwengu watatia fora sio tu mjini Beijing bali miji mingine pia ya China inayoaanda Olimpik.Tafrija hiyo ya kuwasahaulisha walimwengu misukosuko ya mwenge wa olimpik itaanza Juni 23 hadi septemba 17.

China imekuwa ikiandaa sherehe zilizofungamana na michezo ya olimpik ya mwaka huu tangu pale 2003.Sherehe hizo zikijumuisha filamu,mashindano ya nyimbo,maonesho pamoja na harakati zilizohusiana na Olimpik kama vile kuvitangaza vikatuni vya olimpik.Sherehe hizo zitajumuisha michezo ya mwanacinema mashuhuri wa hong Kong Jackie Chan,mwanamuziki wa kitaliana Andrea Bocelli na muingereza Sarah Brightman.