1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS: Mazungumzo kuhusu Kosovo yafanyika

20 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CPb0

Serbia imesema leo kwamba imependekeza kuigeuza Kosovo kuwa mkoa utakaojitawala wenyewe mfano wa Aland, mkusanyiko wa visiwa zaidi ya 6,000 vilivyo himaya ya Finland.

Pendekezo hilo limewasilishwa na maafisa wa serikali ya Serbia wanaohudhuria mkutano mjini Brussels, Ubelgiji unaowajumulisha wajumbe kutoka jimbo la Kosovo, Umoja wa Ulaya, Marekani na Urusi.

Waziri mkuu mteule wa Kosovo, Hashim Thaci, amesema leo kwamba atashauriana na Marekani na Umoja wa Ulaya kabla kutangaza uhuru wa jimbo lake kutoka kwa Serbia, iwapo juhudi za kufikia uamuzi kuhusu hatima ya Kosovo zitakwama kufikia tarehe ya mwisho iliyopangwa Disemba 10.

Umoja wa Ulaya umewatolea mwito Walbania wa Kosovo wasitangaze uhuru kutoka kwa Serbia. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, amesema hatua hiyo itasababisha matatizo makubwa na kwamba suluhisho litakalofikiwa litafaa kwa pande zote husika.

´Tangazo la uhuru kutoka upande mmoja, litasababisha hatimaye kuwepo na watu wengi na pande nyingi zilizoshindwa kwa kuwa hivi sasa wazo hilo halileti maana ya kutosha.´

Hapo awali kiongozi muasi wa zamani wa Albania, Hashim Thaci, ambaye chama chake kilishinda uchaguzi uliofanyika Jumapili iliyopita, alitishia kutangaza uhuru wa Kosovo ikiwa makubaliano kuhusu hatima ya jimbo hilo hayatafikiwa kufikia tarehe 10 mwezi ujao.