1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRUSSELS : Makubaliano ya anga huru ya Atlantiki

23 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCGP

Umoja wa Ulaya umeunga mkono kwa kauli moja makubaliano na Marekani ambayo yataongeza ushindani na idadi ya abiria wanaosafiri kupitia anga la Atlantiki kati ya Ulaya na Marekani.

Chini ya makubaliano hayo yanayojulikana kama ya anga huru ndege za mashirika ya ndege ya Ulaya zitaruhusiwa kuruka kutoka uwanja wa ndege wowote ule wa nchi wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya kuelekea katika uwanja wa ndege wowote ule wa Marekani na vivyo hivyo kwa Marekani.

Mawaziri wa Umoja wa Ulaya wameamuwa kuchelewesha kuanza kutumika kwa makubaliano hayo kwa miezi mitano hadi hapo mwezi wa Machi mwaka 2008 ili kuiridhia Uingereza ambayo ina mashaka kuwa mageuzi hayo ya usafiri wa anga hayakuchukuwa hatua za kutosha kuhusiana na haki miliki za mashirika ya ndege ya Marekani.

Waziri wa Uchukuzi wa Ujerumani Wolfgang Tiefensee ameyapongeza makubaliano hayo lakini amekiri kwamba makubaliano hayo hayakufunguwa kikamilifu soko la usafiri wa anga kati ya Ulaya na Marekani.