Brown: Tutawarudisha nyumbani wanajeshi 1000 | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.10.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Brown: Tutawarudisha nyumbani wanajeshi 1000

Kwenye ziara ya kwanza kama waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown alitangaza idadi ya majeshi ya Uingereza huko Irak itapunguzwa na elfu moja kati wao watarudi nyumbani kabla ya mwaka huu kuisha. Serikali ya Irak imearifu iko tayari kuchukua dhamana ya kuhakikisha usalama jimboni Basra Kusini mwa nchi hiyo ambayo ni muhimu kwa uchumi wa Iraq.

Wairaqi kwenye kituo cha zamani cha Waingereza mjini Basra

Wairaqi kwenye kituo cha zamani cha Waingereza mjini Basra

“Naamini katika miezi miwili ijayo tutaweza kuwa na uthibiti wa kijimbo huko Iraq na kwamba ni juu ya Wairaqi kubeba jukumu la usalama wao katika jimbo zima la Basra." Haya aliyasema Gordon Brown alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kukutana na waziri mkuu wa Iraq, Nuri al-Maliki leo mchana na kabla ya kuendelea kwenda Basra kukutana na majeshi yake.

Waziri mkuu wa Iraq, Nuri al-Maliki alithibitisha mpango wa kiongozi mwenzake wa Uingereza na kusema kuwa vikosi vya usalama vya Iraq viko tayari kuchukua jukumu la Waingereza huko Basra. Kwa sasa kuna wanajeshi 5250 wa Uingereza nchini Iraq na Gordon Brown alisema idadi hiyo itapunguzwa kufikia 4500 mwishoni mwa mwaka huu. Huko Basra, waziri mkuu huyu alisifu wanajeshi wake na aliwaambia kuwa wanafanya kazi muhimu kujenga demokrasia.

Mwezi mmoja uliopita, Uingereza iliondosha majeshi yake kutoka kati kati mwa Basra na kuna ripoti kadhaa zinazosema kuwa hali imetulia kidogo mjini humo. Hata hivyo lakini bado ni mahala ambapo makundi tofauti ya wanamgambo wa Kishia wanapigana wakati mji huo na bandari yake ina umuhimu mkubwa kwa uchumi wa Iraq.

Kwa mujibu wa waziri mkuu Gordon Brown, ambaye ziara yake inakuja katika wakati ambapo idadi ya mashambulizi imepungua, Uingereza inataka kubadilisha mkakati wake huko Iraq. Brown amesema: “Kile ambacho sisi tunakipendekeza kufanya katika miezi ijayo ni kumaliza hali ambapo tulikuwa na jukumu la kupigana kuelekea kuwa na kazi ya kusimamia tu na Wairaqi wakubali wajibu na jeshi la watu 30.000. Yaani wao wabebe jukumu juu ya hali ya usalama na sisi Waingereza tuiangalie na tuwe tayari kusaidia na kuingilia kati ikiwa italazimika. Lakini wakati huo huo tujihusishe zaidi katika kuwafundisha maafisa wa usalama kwa Iraq.”

Licha ya waziri mkuu wa Iraq al-Maliki kukubali mpango huu, kuna pingamizi pia. Waziri wa zamani wa masuala ya mafuta, Bw. Ibrahim Bahr al-Oloum alisema ni mapema mno kuzungumzia upungufu mkubwa wa jeshi la Uingereza huko Iraq na kwamba vikosi vya Iraq haviko tayari kuhakikisha usalama huko Kusini.

Kamanda wa jeshi la Marekani nchini Iraq, jenerali David Petraeus ambaye pia alikutana na Gordon Brown, alisema haamini kama uamuzi wa kupunguza idadi ya Wanajeshi wa Uingereza umeshachukuliwa. Idadi kamili ikaamuliwa kati ya makamanda ya Marekani na Uingereza katika siku zijazo.

Wakati huo huo, nchini Uingereza, kumezuka uvumi kwamba hatua hiyo ya Gordon Brown ni ishara kwamba waziri mkuu huyu baada ya kuchukua wadhifa kutoka mtangulizi wake Tony Blair hapo June anataka kuitisha uchaguzi wa mapema na kwamba uamuzi wa kuwarudisha nyumbani idadi kubwa ya wanajeshi utampatia kura nyingi.

 • Tarehe 02.10.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH7H
 • Tarehe 02.10.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CH7H

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com