1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BRISBANE: Afisa wa Uingereza kumhoji daktari wa India

4 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBm2

Uingereza imemtuma afisa wa ngazi ya juu wa polisi kwenda Australia kumhoji daktari wa India kuhusiana na njama ya mashambulio ya kigaidi mjini London na Glasgow Scotland.

Waziri mkuu wa Australia, John Howard, amesema mtaalamu huyo wa ugaidi kutoka Uingereza atawasili Australia leo asubuhi kumhoji Mohammed Haneef, msajili wa hospitali aliyekamatwa katika uwanja wa ndege wa Brisbane akijaribu kuikimbia nchi hiyo juzi Jumatatu usiku.

Howard amesema mwanamume huyo amezuiliwa na anahojiwa na kuna mtu wa pili ambaye anawasaidia polisi na uchunguzi wao.

Haneef alikamatwa kufuatia ushauri uliotolewa na polisi ya Uingereza baada ya maafisa kugundua alikuwa na mazungumzo ya simu na mmoja kati ya washukiwa saba waliokuwa tayari wametiwa mbaroni nchini Uingereza na Australia.

Mahakama moja ya Australia imewaruhusu maafisa wa polisi kuendelea kumzuilia mshukiwa huyo kwa saa 48 zaidi mpaka leo usiku ili ahojiwe.

Wakati huo huo, daktari mwingine aliyekuwa akihojiwa na polisi wa Australia kuhusina na njama ya mashambulio ya mabomu mjini London, ameachiliwa huru na wala hatachukuliwa hatua yoyote kisheria.