1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Brahimi aonya kuhusu hali mbaya kabisa Syria

30 Desemba 2012

Mjumbe wa kimataifa anayeshughulikia mpango wa amani nchini Syria, Lakhdar Brahimi ameonya kwamba hali nchini humo itakuwa mbaya sana iwapo pande zote zonazozozana zitasusia mazungumzo.

https://p.dw.com/p/17BFJ
FILE - In this Dec. 17, 2012 file photo, a man runs between debris after a mortar shell hit a street killing several people in the Bustan Al-Qasr district of Aleppo, Syria. 2012 was a year of storms, of raging winds and rising waters, but also broader turbulence that strained our moorings. Old enmities and grievances resurfaced in the Middle East, clouding the legacy of the 2011 Arab spring. And the number of dead in the Syrian civil war passed 40,000. (Foto:Narciso Contreras, File/AP/dapd)
Syrien - Kämpfe in AleppoPicha: dapd

Urusi imewashutumu wapinzani wa rais Assad kwa kukataa kushiriki mazungumzo ya upatanishi wakati waasi wakisema kwamba Urusi inafaa kuomba msamaha kwa kumuunga mkono rais Assad.

Katika mkutano na waandishi habari mjini Moscow, Brahimi amesema watu wenye wajibu ndani na nje ya Syria wanapaswa kuwasaidia Wasyria kusitisha mapigano ambayo yanaendelea kusasabisha umwagikaji mkubwa wa damu, na kutokea machafuko zaidi na hata labda kuifanya Syria kuwa taifa lililoshindwa. Brahimi anatarajiwa kukutana na wanadiplomasia wa ngazi za juu wa Marekani na Urusi kwa pamoja katika wiki chache zijazo. Wanaharakati nchini humo wanasema takribani watu 400 wameuawa jana katika siku mbaya kabisa ya machafuko nchini humo.

Brahimi amefanya mazungumzo mjini Moscow na Waziri wa Mambo ya kigeni Sergei Lavrov
Brahimi amefanya mazungumzo mjini Moscow na Waziri wa Mambo ya kigeni Sergei LavrovPicha: Reuters

Urusi imekiri kuwa rais wa Syria Bashar al-Assad hatalazimishwa kuondoka madarakani, lakini imesisitiza kuwa bado kuna nafasi ya kupatikana ufumbuzi wa kisiasa kwa mgogoro huo uliodumu miezi 21. Waziri wa mambo ya Kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amesema yeye na Brahimi wamekubali kwamba kuna matumaini ya kupatikana suluhisho mradi tu nchi zenye nguvu ulimwenguni ziendelee kuziwekea shinikizo pande zote zinazolumbana.

Urusi imekuwa chini ya shinikizo kubwa la kuutaka uongozi wa mshirika wake wa mwisho katika Mashariki ya Kati kukubali mpango ambao utawafanya waasi kupata nguvu hatua kwa hatua wakati mapigano yakiendelea ndani ya Damascus.

Brahimi ameleezea picha ya namna majirani wa Syria, Jordan na Lebanon wanavyoweza kuzidiwa na wakimbizi milioni moja kama mapigano ya kutaka mamlaka yatalipuka katika mji mkuu wa Damascus wenye wakaazi milioni tano.

Rais wa Syria Bashar al-Assad na mshirika wake wa Urusi Wladmir Putin
Rais wa Syria Bashar al-Assad na mshirika wake wa Urusi Wladmir PutinPicha: dapd

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi Sergei Lavrov ameunga mkono matamshi hayo akionya kwamba Syria imo katika hatari ya kusambaratika na kuwa taifa lililoshindwa kama Somalia, nchi inayotatizwa na mibabe ya kivita na wapiganaji wa Kiislamu wenye itikadi kali.

Ziara ya Brahimi inakuja wakati kukiwa na shughuli nyingi za kidiplomasia mjini Moscow ambazo zimeifanya Urusi kutoa mwaliko wa mazungumo kwa upinzani wenye silaha, Muungano wa Kitaifa, ambao unatambulika na serikali za Magharibi kama mwakilishi pekee halali wa watu wa Syria.

Mwaliko huo ulikataliwa na mkuu wa kundi la Upinzani Ahmed Moaz al-Khatib, hali iliyosababisha jibu la hasira kutoka kwa Lavrov. Lavrov amesema Khatib siyo mtu anayefahamu siasa na hivyo ingekuwa vyema kutosikiliza yanayosemwa katika vyombo vya habari na badala yake kuyasikia moja kwa moja kutoka kwa wanadiplomasia.

Nchini Syria kwenyewe, jana Jumamosi(29.12.2012) imekuwa siku mbaya sana ya umwagikaji damu ambapo takribani watu 400 wameuawa, miongoni mwao zaidi ya raia 76. Shirika la Kuangalia haki za binaadamu la Syria limesema watoto wanane ni miongoni mwa watu 17 waliouawa katika shambulizi la angani dhidi ya vitongoji vya mji mkuu Damascus. Rais wa Misri Mohammed Mursi amesisitiza kuwa utawala wa sasa hauna nafasi katika mustakabali wa Syria.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Sekione Kitojo