1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Borussia kuumana na Juve Champions League

23 Februari 2015

Champions League duru ya mtoano Dortmund yaelekea Turin kupambana na Juventus na je Barcelona itaunguruma dhidi ya Manchester City? Bayern yapata tena karamu ya magoli katika Bundesliga.

https://p.dw.com/p/1EgB0
Fußball Bundesliga 2014/2015 VfB Stuttgart Borussia Dortmund
Borussia DortmundPicha: picture-alliance/dpa/Ronald Wittek

Viongozi wa Ligi ya Ujerumani Bundesliga, Bayern Munich wameirarua Paderborn kwa mabao 6-0 siku ya Jumamosi ikiwa ni mchezo wa pili mfululizo kutoa dozi kubwa kiasi hicho. Wiki iliyopita Bayern Munich iliiadhibu Hamburg SV kwa kuikaanga bila mafuta katika kipigo cha mabao 8-0.

Lakini Hamburg SV ilijirekebisha jana Jumapili na kuwapa matumaini mashabiki wake kwa kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Borussia Moenchengladbach , timu ambayo iko katika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi ya Ujerumani Bundesliga. Mshambuliaji wa Hamburg ambaye alipachika bao la kuongoza kwa timu yake Zoltan Stieber anasema baada ya bao hilo aliamini kuwa watatoka uwanjani na pointi zote tatu lakini haikuwa hivyo:

Fußball Bundesliga 22. Spieltag SC Paderborn FC Bayern München
Wachezaji wa Bayern MunichPicha: Lars Baron/Bongarts/Getty Images

"Inatia uchungu sana, kwasababu niliamini, kwamba tulicheza vizuri sana tangu mwanzo. Kwa kweli, inatia uchungu sana katika dakika za mwisho kufungwa bao na kupoteza pointi mbili muhimu."

Borussia Dortmund ilipata ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya VFB Stuttgart , likiwa ni pambano muhimu kwa timu hizo ambazo zote zimo katika hatua ya kujinasua kutoka katika eneo la kushuka daraja. Borussia Dortmund imeweza kujitoa kutoka eneo hilo na kuonekana kuelekea kupata mafanikio zaidi katika sehemu hii ya pili ya Bundesliga.

Schalke 04 hata hivyo ilikubali sare ya bao 1-1 siku ya Jumamosi dhidi ya werder Bremen ambayo imeonesha kuimarika katika kila mchezo mwaka huu na kujitoa kabisa kutoka katika eneo la hatari ya kushuka daraja. Kocha wa Schalke 04 Roberto Di Mateo nae anasema inakera kufungwa bao la dakika za mwisho ambalo linakosesha ushindi.

Fußball Bundesliga 23. Spieltag HSV vs. Borussia Mönchengladbach
Zoltan Stieber wa Hamburg SVPicha: M. Rose/Bongarts/Getty Images

"Inakera mno, ambapo katika dakika za majeruhi tumefungwa bao la kusawazisha. Nafikiri tulistahili kupata ushindi leo. Tulistahili kupata goli la kuongoza. Tuliweza kuidhibiti timu bora kabisa kwa sasa Werder Bremen ambayo imekuwa katika hali ya kujiamini. Timu ambayo imeweza kupata jibu la mchezo wetu kwa mkwaju wa frii kick. Na hii inakera sana, kwasababu tulicheza vizuri sana, tulipambana na tungestahili kushinda."

Bao lililofungwa na mlinda mlango Marvin Hitz wa Augsburg liliiokoa timu hiyo katika kipigo dhidi ya Bayer Leverkusen wakati timu hiyo ikiwa nyuma kwa mabao 2-1 na hatimaye timu hizo kuridhika na sare ya mabao 2-2. Marvin Hitz anazungumzia bao hilo muhimu.

"Kwangu mimi inakuwa taabu kidogo , kwa kuwa mimi ni mchezaji wa kuzuwia mabao. Lakini inafurahisha pia , kufunga bao."

Katika ligi ya Uhispania ushindi mara 11 wa Barcelona ulifikia kikomo siku ya Jumamosi wakati Malaga ilipofanikiwa kutumia makosa ya mlinzi Dani Alves kupata ushindi wa bao 1-0 katika La Liga.

Fußball Yaya Toure von Manchester City
Yaya Toure wa Manchester CityPicha: Alex Livesey/Getty Images

Matokeo hayo yameiruhusu Real Madrid , ambayo ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Elche jana Jumapili kufungua mwanya wa pointi nne juu ya msimamo wa ligi ya Uhispania La Liga.

Atletico Madrid inapumulia hivi sasa katika kisogo cha Barcelona baada ya kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Almeira na kukaa pointi 3 nyuma ya barcelona.

Viongozi wa Premier League Chelsea ilitoka sare ya bao 1-1 na Burnley wakati mahasimu wao wa karibu waliichakaza Newcastle kwa mabao 5-0. Jana Jumapili "The Reds " Liverpool ilipata ushindi muhimu wa mabao 2-0 dhidi ya Southampton na kukaa pointi moja nyuma ya timu hiyo iliyoko katika nafasi ya tano, wakati Tottenham Hot Spurs imepata sare muhimu ya mabao 2-2 jana Jumapili dhidi ya West Ham United.

Champions League uwanjani tena

Manchester City na Barcelona zinakutana kwa mara ya pili mfululizo katika kinyang'anyiro cha Champions League , wakati Borussia Dortmund na Juventus Turin zinafufua kumbukumbu za fainali ya mwaka 1997 mjini Munich ambapo Borussia Dortmund iliibuka na ushindi wake wa kwanza katika Champions League, zitakapokutana kesho Jumanne katika duru ya mtoano ya timu 16 bora barani Ulaya.

Jürgen Klopp Bayer Leverkusen - Borussia Dortmund
Jürgen Klopp wa Borussia DortmundPicha: picture-alliance/dpa/Revierfoto

Kocha wa Arsenal , Arsene Wenger anakabiliana na klabu yake ya zamani ya monaco wakati Bayer Leverkusen ya Ujerumani inatiana kifuani na mabingwa wa Uhispania Atletico Madrid katika mchezo utakaopigwa siku ya Jumatano na kukamilisha ratiba ya duru ya kwanza ya awamu ya mtoano ya Champions League.

Wakati Juve iko kileleni mwa ligi ya Italia Serie A , Borussia Dortmund imekuwa ikihangaika msimu huu, lakini hali ya kujiamini inaonekana kurejea taratibu katika kikosi hicho cha Jurgen Klopp baada ya kupata ushindi mara tatu mfululizo katika Bundesliga.

Na licha ya kwamba mbinyo bado ni mkubwa katika Bundesliga, kocha Jurgen Klopp amesema "Champions League ni hadithi tofauti kabisa."

"Hatuendi huko tukiwa tunatarajiwa kupata ushindi, lakini tutajitahidi," amesema Klopp.

"Tunataka kupata matokeo mazuri, tutaona nani ataweza kesho Jumanne. Lakini tunaweka umuhimu bado katika Bundesliga , Champions League ni kionjo tu." Ameseongeza.

Klopp huenda akatumia mchezo huo dhidi ya Juventus kufanya mabadiliko kiasi. Mlinzi Mats Hummels amepona homa ya mafua na mchezaji wa kati Jakub Kuba Blaszczykowski, Sven Bender na Sebastian Kiel wamerejea kundini baada ya kuwa majeruhi.

Kocha wa Juve Massimiliano Allegri amesema anawasi wasi mkubwa na Dortmund katika Champions League, kwani hata kama wanalega lega katika ligi ya nyumbani , inapokuja katika Champions League Borussia inaonesha rangi zake halisi.

Pirlo ana matumaini

Hata hivyo mchezaji wa kati wa Juventus Andrea Pirlo ana matumaini kuwa msimu huu hatimaye watajionesha kuwa vigogo katika jukwaa la Ulaya wakati akiwa na ndoto ya kushinda kombe la Champions League tena kabla hajastaafu.

Njia ya Barcelona kuelekea kuingia katika duru ya robo fainali kwa mara ya nane mfululizo inaweza kuzibwa na kikosi cha Manchester City ambacho kinahamu kubwa ya kufikisha mwisho miaka mitatu ya kuvurunda katika kinyang'anyiro hicho.

Kwa mabingwa hao wa Uingereza kuna suala ka kulipiza kisasi cha kutolewa na Barcelona katika awamu kama hiyo msimu uliopita wakati kipigo katika michezo yote miwili kiliiwezesha Barca kupata ushindi wa jumla wa mabao 4-1.

Misri yabwaga manyanga

Katika bara la Afrika Misri imejitoa katika kinyang'anyiro cha kuwania kuwa mwenyeji wa fainali za mwaka 2017 za kombe la mataifa ya Afrika wiki mbili baada ya watu 19 kufariki nje ya uwanja wa mjini Cairo , amesema waziri wa serikali ya Misri jana.

Gabon na Ghana ni nchi mbili nyingine zinazowania nafasi hiyo kuchukua nafasi ya Libya inayokabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe hivi sasa. Mshindi atapatikana kwa kupiga kura katika shirikisho la kandanda barani Afrika CAF mjini Cairo mwezi Aprili mwaka huu.

Na michezo ya bara la Afrika , All africa Games inyofanyika kila baada ya miaka minne itakayofanyika nchini Congo mwaka huu imeanza duru ya kuwania kufuzu kucheza katika michezo hiyo ambapo Nigeria imeanza vizuri kwa kuishinda Gabon kwa mabao 4-1 mwishoni mwa juma.Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo ilishindwa nyumbani dhidi ya Burundi kwa bao 1-0 , wakati Msumbiji na Uganda zilitoka sare bila kufungana. Misri inatarajiwa kuwa mwenyeji katika pambano kati yake na Kenya Machi mosi.

Michuano ya Champions League na kombe la shirikisho barani Afrika itafanyika tena wiki hii, ambapo Azam FC ya Tanzania inatarajiwa kwenda huko Sudan kesho Jumanne 24.02.2015 , ambako itapambana na mabingwa wa huko El-Mereikh na Dar Young Africans inasafiri kwenda Botswana kupambana na timu ya jeshi la nchi hiyo.

Ngumi.

Mwanamasumbwi kutoka ufilipino Manny Pacquiao amedokeza leo kuwa pambano lake lililokuwa likisubiriwa kwa hamu kubwa na wapenzi wa ndondi duniani dhidi ya Mmarekani Flyod Mayweather huenda likawa la mwisho kwake, akisema ataingia katika pambano hilo la mwezi Mei akiwa anafikiria kustafu kabisa mchezo huo.

Floyd Mayweather
Floyd MayweatherPicha: Getty Images/Afp/John Gurzinski

Baada ya miaka ya kushindwa majadiliano, Pacquiao na Mayweather walifikia makubaliano kupambana mjini Las Vegas Mei mbili ambapo hatimaye mashabiki wa mchezuo huo watapata fursa ya kuwaona wapiganaji hao wa zama zao wakitiana kifuani.

Mwandishi : Sekione Kitojo

Mhariri: Iddi Ssessanga