1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bolt amekiri kuwa mita 100 zilikuwa mbio ngumu kwake

24 Agosti 2015

Bingwa wa dunia wa mbio fupi kwa upande wa wanaume Mjamaica Usain Bolt amenyakua dhahabu katika mita 100 baada ya kuwapiku wapinzani wake wakuu

https://p.dw.com/p/1GKM1
15. Leichtathletik-Weltmeisterschaft in Peking 2015 Usain Bolt und Justin Gatlin
Picha: Reuters/K. Pfaffenbach

Bolt amehifadhi taji lake la dunia mbele ya umati mkubwa uliojitokeza kushuhudia fainali hiyo katika uwanja wa kimataifa Kiota cha Ndege mjini Beijing China, katika mashindano yanayoendelea ya riadha ya dunia.

Licha ya kupigiwa upatu kuwa mashindano magumu kwa kujumuisha majina yote tajika yakiwemo wanariadha wakuu wa mbio hizo, Mjamaica Asafa Powell, Wamarekani Tyson Gay na Justin Gatlin, Bolt alijitahidi na kuonyesha ubabe wake.

Justin Gatlin, alikuwa ameandikisha muda bora katika nusu fainali. Na katika fainali akamaliza chini ya nukta moja nyuma ya Bolt aliyeandikisha muda wa sekunde 9.79.

Gatlin aliwahi kutumikia adhabu ya kutoshiriki mashindanoni kwa miaka minne kutokana na hatia ya kutumia dawa za kuongeza nguvu mwilini.

Raia wa Canada, Andre de Grasse na Mmarekani Trayvon Bromell walisajili muda wa sekunde 9.92 na kutuzwa medali ya shaba.

Mwandishi: Brice Amani/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo