1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ali wird 70

Oumilkher Hamidou17 Januari 2012

Bingwa wa zamani wa masumbwi duniani, Muhammad Ali, ametimiza umri wa miaka 70hivi leo (17.01.2012), licha ya kusumbuliwa na maradhi ya Parkinson kwa muda mrefu sasa.

https://p.dw.com/p/13ki4
Muhammad Ali (kulia) na mke wake Lonnie.
Muhammad Ali (kulia) na mke wake Lonnie.Picha: AP

Muhammad Ali alikuwa bondia kwa sababu kuna mtu aliyemuibia baskeli yake. Alikuwa na umri wa miaka 12 wakati ule na alikuwa akiishi Louisville katika jimbo la Kentucky akijuilikana kwa jina la Cassius Mercellus Clay Jr.

Joe Martin, aliyekuja kuwa kocha wake baadaye, anaelezea jinsi kijana huyo alivyokuwa akilia huku akiahidi kumtandika magumi aliyemuibia baskeli yake pindi akimpata. Kocha huyo wa ubondia alimchukua Clay, kijana mweusi anayetokea katika familia ya watu maskini, na kumjumuisha na watoto wengine aliokuwa akiwafundisha.

"Alikuwa na bidii zaidi kuliko waatoto wote wengine niliokuwa nikiwasimamia," anasema Joe Martin.

Ingawa Clay wakati ule hakuwa na nguvu ya kuvurumisha masumbwi, alikuwa mwepesi wa kuranda randa kupita kiasi. Mnamo mwaka 1960, akiwa na umri wa miaka 18, alishinda katika pambano la ndondi la michezo ya Olympiki mjini Rome, Italia. Medali yake ya dhahabu inasemekana aliitupa ndani ya Mto Ohio kwa sababu alikasirishwa na jinsi watu weusi wanavyobaguliwa nchini mwake.

Muhammad Ali akimcharaza Joe Frazier mwaka 1975.
Muhammad Ali akimcharaza Joe Frazier mwaka 1975.Picha: picture-alliance/dpa

Cassius Clay alikamilisha michuano ya wasiolipwa baada ya kuibuka na ushindi mara 100 katika jumla ya mapambano 108 aliyopigana. Wafanyabiashara 11 wa Kizungu kutoka Louisville walishirikiana ili kumfungulia njia Cassius Clay ya kuingia katika ulingo ya mabondia wa kulipwa.

Bondia huyo mwenye kipaji alikuwa akitajikana pia kuwa ni mtu aliyekuwa na majivuno na mdomo mpana. Kabla ya mapambano yake, Cassius Clay daima alikuwa akijinata kuwa yeye "ndie mbabe wa wababe na mzuri kuliko mabondia wote na kuwakejeli wapinzani wake.

Katika pambano lake la kwanza la kuwania ubingwa wa dunia Februari 1964 dhidi ya mtetezi wa taji hilo, Sonny Liston, Clay hakuwa akijulikana ni nani na watu waliamini angeshindwa tu. Lakini baada ya raundi ya sita, Liston aliungama. "Mie ndie mbabe," alinguruma Cassius Clay kupitia kikuza sauti.

Mwaka huo huo, alisilimu na kujiunga na kundi la Nation of Islam lililokuwa likiongozwa wakati huo mwanaharakati wa haki wa Wamarekani Weusi, Malcolm X. Akabadilisha jina la Cassius Clay na kujiita wakati huo huo Muhammad Ali.

Muhammad Ali akiwacha mwenge wa Olimpiki mjini Atlanta mwaka 2001.
Muhammad Ali akiwacha mwenge wa Olimpiki mjini Atlanta mwaka 2001.Picha: picture-alliance/dpa

Muhammad Ali hakuwa bondia tu, alikuwa mwanaharakati pia. Alipinga vita vya Marekani nchini Vietnam na alikataa kutekeleza sheria ya kutumikia jeshi. Mnamo mwaka 1967, akapokonywa sio tu leseni yake ya ubondia, bali pia alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela, ingawa baadaye bondia huyo wa aina pekee aliachiwa kwa dhamana.

Wasanii na wasomi mfano wa Richard Burton na Henry Fonda au mwandishi vitabu Truman Capote wakampigania mpaka Muhammad Ali akaruhusiwa tena kurejea ulingoni baada ya kulazimika kukaa nje kwa miaka mitatu.

Machi 8, 1971 Muhammad Ali aliteremka ulingoni Madison Square Garden mjini New York kwa kile kilichotaajwa "kuwa pambano la ndondi la karne" dhidi ya bingwa wa wakati ule, Joe Frazier. Lilikuwa pambano kati ya mafahali wawili, kati ya mpinzani na yule aliyekuwa akiangaliwa kama mwakilishi wa mtindo wa maisha wa Kimarekani. Katika pambano hilo la kusisimua la zaidi ya raundi 15, Frazier akashinda kwa pointi. Ali akalazimika kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya ubondia kunusa jamvi.

Yakafuata mapambano mengine ya kusisimua mfano wa lile la mjini Kinshasa dhidi ya George Foreman mnamo mwaka 1974, ambapo Muhammad Ali anasema "aliranda mfano wa kipepeo na kuuma kama nyuki"

Muhammad Ali (kulia) katika pambano na George Foreman mwaka 1974.
Muhammad Ali (kulia) katika pambano na George Foreman mwaka 1974.Picha: picture-alliance/dpa

Muhammad Ali alilipiza kisasi dhidi ya Joe Frazier mwaka 1975 na kumlazimisha kusalimu amri mnamo rauni ya 14. Mohammed Ali alistaafu mwishoni mwa mwaka 1981 baada ya kuranda kwa karibu miaka 40.

Wakati huo tayari alikuwa anasumbuliwa na maradhi ya Parkinson. Licha ya maradhi hayo, Muhammad Ali ndiye aliyewasha mwenge wa Olimpiki huko Atlanta mnamo mwaka 1996 na kuusisimua ulimwengu mzima. Mwaka 1999 aliteuliwa na kamati kuu ya michezo ya Olimpiki kuwa "mwanaspoti bora wa karne."

Mpinzani wake wa zamani George Foreman amegeuka hivi sasa kuwa rafiki yake mkubwa na kuungama "Muhammad Ali ndie bingwa wa mabingwa."

Mwandishi: Stefan Nestler
Tafsiri: Oummilkheir Hamidou
Mhariri: Yusuf Saumu