1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Berlusconi ang'oka madarakani

14 Novemba 2011

Italia bila ya Berlusconi,kitandawili cha mfululizo wa mauwaji cha fumbuliwa na mkutano mkuu wa chama cha CDU mjini Leipzig ni miongoni mwa mada kuu magazetini

https://p.dw.com/p/13ADF
Wataliana washerehekea kujiuzulu BerlusconiPicha: picture alliance / dpa

Tuanzie lakini Italia ambako malaki walisherehekea tangazo la kujiuzulu Silvio Berlusconi.Gazeti la "Rhein-Necker-Zeitung la mjini Heidelberg linaandika:

Hata kama kujiuzulu tajiri mwenye kumiliki vyombo vya habari kumepelekea shangwe na vigelegele kuhanikiza katika barabara za mjini Roma,bado lakini kuna wanaompenda mzee huyo wa miaka 75 miongoni mwa wataliana.Si wameshamchagua mara nne hapo awali.Cha kutarajia ni kuwaona wataliana safari hii wakidhihirisha wamechoshwa kweli na visa vya Bunga Bunga,dhana za rushwa,na kufilisika taifa na kutompatia tena nafasi Berlusconi ya kurejea tena madarakani.

Gazeti la "Donaukurier" linahisi enzi za Berlusconi zimekwisha.

Basta.Enzi za Berlusconi kweli zimepita.Wenye wasiwasi walikuwa bado wakihofia pengine Cavalieri angebadilisha maoni na kutong'atuka.Lakini shinikizo lilikuwa kubwa mno kwa tajiri huyo anaemiliki vyombo vya habari.Amefanikiwa Berlusconi alieitawala nchi hiyo tangu mwaka 1994, kutoitumbukiza katika janga la muflis .La muhimu amefungua njia ya kuanza enzi mpya ya mageuzi.

Mada yetu ya pili magazetini inahusu mashamabulio ya wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia.Gazeti la "Kieler Nachrichten linaandika

Mordopfer Döner-Morde Neonazis Terrorismus Mord Rechtsextremismus
Picha za wahanga wanane wa mauwaji ya wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia,(kutoka kushoto) Enver Simsek, Abdurrahim Özüdogru, Süleyman Tasköprü na Habil Kilic pamoja na Yunus Turgut, Ismail Yasar, Theodorus Boulgarides naMehmet KubasikPicha: picture alliance/dpa

Mashambulio hayo yanalingana kwa kila hali na yale ya kundi la magaidi wa siasa kali za mrengo wa kushoto-RAF.Hata kinadharia,wafuasi hawa wa siasa kali za mrengo wa kulia hawatofautiani na wale wa RAF.Hawa lakini wanawalenga na kuwaandama moja kwa moja wageni.Cha kustaajabisha ni kwamba kwa kadiri mwongo mmoja sasa kuna mtandao wa siasa kali za mrengo wa kulia humu nchini na idara ya upelelezi haijaugundua.Kumefanyika uzembe kwa kila hali; naiwe walifikiria wakati wote kuhusu uwezekano wa kufanyika mauwaji ya kikatili dhidi ya waturuki au walifumba macho.

Gazeti la Stuttgarter Zeitung linaandika:

Hata kama hadi wakati huu masuala yanaonekana kuwa mengi zaidi ya majibu-kimoja lakini mtu anaweza kukisema tangu sasa kuhusiana na mlolongo wa mauwaji dhidi ya wenye kumiliki maduka ya nyama choma:Kwa mtazamo wa waendesha uchunguzi-kila kitu kimekwenda kombo.Kabla ya wanasiasa kupiga makelele na kuonya dhidi ya hisia za chuki dhidi ya wageni,kuna baadhi ya masuala watu wanayobidi kujiuliza:Idara gani ,zilijua nini?Makosa yamefanywa na nani?Ni shida kuyajibu masuala hayo ili kuweza kwa mara nyengine tena kupendekeza chama cha siasa kali za mrengo wa kulia NPD kipigwe marufuku.Lakini masuala hayo hayo yanaweza kusaidia pakubwa katika kujikinga dhidi ya visa vya uhalifu vya makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia.

Dossierbild CDU Merkel 3
Kansela Angela Merkel na chama chake cha CDUPicha: picture alliance / dpa

Tumalizie na gazeti la "Leipziger Volkszeitung lililoandika kuhusu mkutano mkuu wa chama cha Christian Democratic Union-CDU.Gazeti linaandika:

Mikutano mikuu inayoitishwa Leipizig ndiyo inayoamua kwa sehemu kubwa mkondo na majaaliwa ya chama cha CDU kinachoongozwa na Angela Merkel.Badala ya kukwepa mfumo wa shoto wa kijamii,Merkel anaujenga mfumo wa ujamaa wa kijamii wa CDU.Ananyemelea mrengo wa shoto ili kuwapokonya uwanja wapinzani wake wa kisiasa-huo ndio mkakati wake.Lakini kwa namna hiyo amewapokonya pia wapiga kura wengi asilia wa CDU kitambulisho chao .Kuanzia azma ya kujitenganisha na nishati ya kinuklea hadi kufikia kusitishwa kipindi cha watu kulitumikia jeshi-yote hayo amefanikiwa Merkel kuyapigia mhuri wa CDU katika kipindi kifupi tu.

Mwandishi:Hhamidou Oummilkheir/DPA

Mhariri:Josephat Charo