1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Benki Kuu ya Marekani imepunguza kima cha riba ya mikopo

19 Septemba 2007

Vipi mtu anaweza kuzuwia mzozo wa kiuchumi huko Marekani baada ya hasara iliopatikana karibuni katika masoko ya majumba. Benki kuu ya nchi hiyo ilitafuta jibu la suali hilo hapo jana kwa kupunguza riba kwa asilimia 0.5 kwa mikopo ambayo inatoa kwa mabenki ya kibiashara na baadae mabenki hayo kuwakopesha wateja. Riba hiyo sasa itakuwa ya asilimia 4.75. Kiwango hicho cha kupunguzwa riba kiliwashangaza mabingwa wa masuala ya fedha waliotarajia riba kwenda chini kwa asilimia 0.25 tu.

https://p.dw.com/p/CHjG
Waziri wa uchumi wa Ujerumani, Michael Glos
Waziri wa uchumi wa Ujerumani, Michael GlosPicha: picture-alliance/dpa/webdpa

Tukumbuke kwamba hasara iliopatikana katika masoko ya majumba huko Marekani imewaacha wananchi wengi kutowezi kumudu kulipa mikopo ya majumba yao waliochukuwa wakati riba za mabenki katika nchi hiyo zilikuwa ziko chini mno. Waziri wa uchumi wa Ujerumani, Michael Glos, amesema mzozo huo wa biashara ya majumba huko Marekani huenda ukauathiri pia uchumi wa Ujerumani kwa kuifanya thamani ya sarafu ya Euro iwe juu zaidi ukilinganisha na dola ya Kimarekani. Jana dola ilifikia thamani ya chini kabisa ikiuzwa kwa dola 1.40 kwa Euro moja. Uchumi wa Ujerumani unategemea sana kusafirisha bidhaa zake ngambo, huku biashara ya ndani hapa nchini ikiwa ni nguzo ndogo ukilinganisha na nchi kama vile Marekani. Makisio ya serekali yanasema uchumi wa Ujerumani utapanda kwa asilimia 2.3 mwaka huu, lakini baadhi ya wachunguzi wanasema unaweza ukapanda hadi asilimia 1.8

Sababu iliotolewa jana na Benki Kuu ya Marekani kuchukuwa hatua hiyo ni kukuwa kwa wastani uchumi wa Marekani katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, na pia nia ya kuimarisha masahihisho yaliofanywa katika masoko ya majumba ambayo ama sivyo uchumi ungekwama. Kupunguzwa kima cha riba kutazuwia kuchafuliwa masoko ya fedha.

Mtu atauliza mafungamano gani yalioko baina ya riba za mikopo na mzozo wa masoko ya majumba huko Marekani? Mafungamano ni mengi. Kutokana na riba inayotozwa na benki kuu, mkuu wa benki hiyo, Ben Bernarke, anakuwa na ushawishi kwa mabenki ya kibiashara, hivyo kuwa na ushawishi pia kwa mikopo ya kawaida. Kila riba ikiwa ndogo, ndipo mikopo inapokuwa si ya gharama kubwa, ya kuvutia, na ndipo wafanya biashara na raia wa kawaida wanapokuwa na hamu ya kukopa na kuwekeza, hivyo fedha kupata njia ya kutumiwa.

Lakini tangu kutokea mzozo wa mikopo ya kununua majumba, mabenki yamezuwia mirija. Kwa vile haijulikani taasisi gani ilioathirika kwa kiwango gani kutokana na mzozo huo, mabenki yamejizuwia kutoa mikopo yeyote, na kama yanatoa basi masharti wanayotoa kwa wateja ni mabaya mno. Biashara hiyo ya fedha ni jambo la kawaida kabisa baina ya mabenki na ni jambo la muda mfupi, kwani mwishowe kila siku hesabu hupigwa fedha ngapi ambazo lazima mabenki ya kibiashara yatoe kama hifadhi yao ya usalama. Kwa hivyo kupunguzwa riba kwa asilimia 0.5 kunayapa mabenki ya kibiashara nafasi ya kuvuta pumzi, na pumzi hiyo ikivutwa wanaofaidika ni wafanya biashara na wateja wa kawaida. Kuna hatari ya mfumko wa bei kupanda pindi mikopo inapokuwa rahisi mno kuipata.

Kutokana na mzozo huo ulioanzia Marekani, hapa Ujerumani kuna mabenki mbili ambazo zilikuwa ukingoni kutangazwa kuwa zimefilisika, ile ya mkoa wa Saxony na ile inayoitwa Mittelstandsbank ambayo hutoa mikopo kwa wafanya biashara wa wastani. Na huko Uengereza wawekezaji wa benki ya Northern Rock walisimama milangoni kuitaka benki yao ilipe akiba zao walizoweka katika benki hiyo. Kwa umbali gani mzozo huo umeathiri mambo ni jambo litakalojulikana katika ripoti ya robo mwaka. Ni sifa kwa benki kuu ya Marekani kwamba katika hali hii ya vuta n’kuvute, mikopo bado inatolewa kwa bei nzuri. Benki hiyo haijajificha nyuma ya ile hoja kwamba kipa umbele kipewe utulivu wa bei za bidhaa. Athari ya kupunguzwa riba huko Marekani inawagusa moja kwa moja pia watu hapa Ulaya. Sarafu ya Euro bado itakuwa na nguvu zaidi, ukilinganisha na dola ya Marekani. Makampuni ya Kijerumani yanayotegemea kusafirisha ngambo bidhaa hayatapenda sana kuiona hali hii.