Bayern Munich yawania kujiimarisha zaidi kileleni mwa ligi | Michezo | DW | 25.11.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Bayern Munich yawania kujiimarisha zaidi kileleni mwa ligi

Baada ya kukamilisha kibarua cha kukata tikiti ya kucheza katika duru ya mtoano ya timu 16 bora katika ligi ya mabingwa barani Ulaya, Bayern Munich inawania kutumisha misuli katika ligi ya nyumbani bundesliga.

default

Franck Ribery wa Bayern Munich akifunga goli katika mchezo wa Champions League dhidi ya Villareal ya Hispania siku ya Jumanne

Baada ya kukamilisha kibarua cha kukata tikiti ya kucheza katika duru ya mtoano ya timu 16 bora katika ligi ya mabingwa barani Ulaya, Bayern Munich inawania sasa kutunisha misuli yake bara bara katika ligi ya Ujerumani Bundesliga Jumapili ikikaribishwa na Mainz 05 . Mabingwa watetezi Borusia Dortmund wanakibarua kigumu tena katika wiki ambayo kwa wao ilielezwa kuwa ni ya kujua mbivu na mbichi, wakati ikikabiliana na watani wao wa jadi Schalke 04.

Huko Uingereza baada ya kuyumbayumba kwa timu za Uingereza Manchester United, Manchester City na Chelsea katika Champions League , hatimaye wanataka kumuondoa bundi katika mapaa yao kwa ushindi katika Premier League.

Ushindi wa mabao 3-1 wa Bayern Munich dhidi ya Villareal ya Uhispania siku ya Jumanne umeithibitisha timu hiyo kuwamo katika kundi la timu 16 bora zitakazoumana katika awamu ya mtoano ya Champions League, Bayern inahitaji kurejea katika njia ya ushindi katika Bundesliga baada ya kupata point moja tu kutoka katika michezo yao miwili iliyopita.

Bayer Leverkusen ambayo nayo imekata tikiti yake ya duru ya mtoano ya Champions League ina miadi na Hertha BSC Berlin, Hoffenheim inaikaribisha Freiburg, Hannover iko nyumbani ikiikaribisha Hamburg SV katika mpambano mwingine wa watani wa jadi, Augusburg inaikaribisha VFL Wolfsburg na Nuremberg itaonyeshana kazi na Kaiserslautern. Jumapili Werder Bremen itaingia uwanjani dhidi ya VFB Stuttgart na Bayern itaumana na Mainz 05.

Huko nchini Uingereza vilabu kadha ambavyo ni vigogo wa soka nchini humo na barani Ulaya vitaelekeza nguvu zao katika kuzika kumbukumbu mbaya ya wiki ya kukatisha tamaa katika Champions League kwa kurejea katika kinyang'anyiro cha ligi ya nyumbani Premier League leo.

Champions-League-Vorschau Manchester gegen Schalke

Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson akizungumza na waandishi habari uwanjani Old Trafford Stadium mjini Manchester.

Stoke City inakumbana na Blackburn Rovers, Bolton Wanderers ina miadi na Everton, wakati Chelsea inajaribu kumuondoa bundi nyumbani kwake kwa kupambana na Wolvehampton. Manchester United inakwaana na Newcastle United , Norwich City inaikaribisha Queens Park Rangers, Sunderland inakibarua na Wigan Atheletics na West Bromwich Albion itaonyeshana kazi na Tottenham Hotspurs. Arsenal London iko nyumbani kuikaribisha Fulham.

Real Madrid na Barcelona nchini Hispania zinaanza mpambano wao wa binafsi katika kilele cha ligi ya nchi hiyo leo Jumamosi. Real wanawakaribisha watani wa jadi Atletico Madrid, wakati Barcelona inasafari hadi kitongoji cha mji mkuu Madrid kuumana na Getafe.

Real Madrid vs Dinamo Zagreb

Mchezaji Mesut Özil wa Real Madrid akituliza mpira.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe /

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman