1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich yaongoza Bundesliga katika nusu ya kwanza ya msimu

16 Desemba 2011

Wakati ligi ya Ujerumani ikiingia katika mapumziko ya majira ya baridi kwa michezo ya leo ya wiki ya 17 katika Bundesliga , Bayern Munich yatawazwa mabingwa wa nusu msimu.

https://p.dw.com/p/13UTX
Wachezaji wa timu ya Bayern Munich
Wachezaji wa timu ya Bayern MunichPicha: dapd

Ligi ya Ujerumani, Bundesliga, inakaribia mapumziko ya majira ya baridi jioni ya leo katika mchezo wa 17 wa nusu msimu. Hata hivyo hakuna shaka kabisa kuwa Bayern Munich itatawazwa kuwa mabingwa wa nusu msimu, kwani hakuna timu inayoifuatia ambayo inaweza kufikisha points 34 ambazo Bayern tayari inazo kibindoni. Mabingwa watetezi Borussia Dortmund ambayo inaifuatia Bayern inasafiri hadi nyumbani kwa SC Freiburg ambayo katika hali halisi inaonekana kuwa ni mpambano rahisi kwake. Freiburg imeweza kushinda mara moja tu katika mapambano 11 yaliyopita dhidi ya Borussia Dortmund nyumbani kwake. Lakini si vizuri kuidharau Freiburg kama anavyoeleza kocha wa mabingwa hao watetezi Borussia Dortmund, Jürgen Klopp.

Kocha wa timu ya Borussia Dortmund, Jürgen Klopp
Kocha wa timu ya Borussia Dortmund, Jürgen KloppPicha: dapd

"Timu yangu kwa bahati nzuri si wendawazimu. Hii ni changamoto kubwa kwetu," alisema kocha huyo. "Mchezo huu ni kati ya timu iliyoko katika nafasi ya pili ya msimamo wa ligi na timu iliyoko mkiani, kwa hiyo ndio sababu , FC Freiburg itatoa ushindani wa hali ya juu."

Pia timu iliyoko katika nafasi ya tatu Schalke 04 katika mpambano wake na Werder Bremen itahitaji kujiimarisha katika nafasi hiyo ama kupanda zaidi. Ni mara mbili tu Schalke imeshindwa katika mapambano 13 dhidi ya Bremen na ni mara moja tu imeshindwa katika mapambano yao tisa yaliyopita nyumbani. Kutokana na hali hiyo meneja wa sport wa Bremen Klaus Allofs anatoa tathmini bila ya tambo kabla ya mchezo huo dhidi ya Schalke.

"Ushindi wa bao 1-0 utakuwa ni matokeo mazuri sana kwetu. Japo mchezo huo huenda usiwe mzuri sana , lakini pamoja na hayo wapinzani wetu hatutawapa nafasi nyingi, hicho ndio tunachowania na itakuwa jambo zuri," alisema Allofs. "Nadhani hii itakuwa ishara nzuri kwa ajili ya hali ya mambo katika msimu huu."

Michezo mingine ni pamoja na FC Nürmberg ikiwa na miadi na Bayern Leverkusen , Wolfsburg ikijaribu kubadilisha majaliwa yake baada ya kipigo wiki iliyopita , inapambana na VFB Stuttgart. Hertha BSC Berlin inaikaribisha Hoffenheim , na SV Hamburg inakwaana na FC Augsburg. Na katika michezo ya Jumapili FC Kaiserslautern inaikaribisha Hannover 96 na Borussia Moenchengladbach inapimana ubavu na Mainz 05.

Katika premier league nchini Uingereza, Manchester City inasema kuteleza si kuanguka , na ina nia ya kuweka kando kumbukumbu za kipigo kwa mara ya kwanza katika ligi msimu huu , wiki iliyopita dhidi ya Chelsea , wakati viongozi hao wa ligi wakiikaribisha Arsenal London kesho Jumapili. Michezo mingine ni pamoja na Blackburn inaikaribisha West Bromwitch, Everton inaivaa Norwich City, Fulham itaonyeshana ubabe na Bolton Wanderers, New Castle United ina miadi na Swansea City nyumbani, wakati Wigan Athletics ina pimana nguvu na Chelsea na Wolveshampton iko nyumbani dhidi ya Stoke City. Na Jumapili Aston Villa itaikaribisha nyumbani Liverpool, na Qeens park Rangers ina kibarua dhidi ya Manchester United na Tottenham Hotspurs itakwaana na Sunderland.

Wachezaji wa timu ya Barcelona
Wachezaji wa timu ya BarcelonaPicha: picture alliance/dpa

Katika kombe la dunia la vilabu , michezo inayofanyika huko Japan , Barcelona mabingwa watetezi wa kombe hilo wanapambana na Santos mabingwa wa America ya kusini katika fainalia kesho Jumapili. Mlinzi wa kulia wa Santos Danilo anapanga kuwapatia mabingwa hao wa America ya kusini zawadi ya kuagana kwa kuisaidia timu hiyo kushinda ubingwa wa dunia kwa vilabu kwa kuishinda Barcelona katika fainali hapo kesho.Danilo anaelekea FC Porto baada ya mchezo huo.

Na timu 16 zilizofuzu kuingia katika duru ya mtoano ya ligi ya mabingwa mabarani Ulaya, Champions League, zitapambana kuanzia Februari 14 na 22 katika mchezo wa kwanza na mchezo wa pili utafanyika March 6 na 14. Olympique Lyon itakwaana na Apoel Nicosia ya Cyprus, AC Milan itaumana na Arsenal London, wakati Basel ya Uswisi itapambana na Bayern Munich. Bayer Leverkusen ya Ujerumani itaonyeshana kazi na mabingwa watetezi Barcelona , CSKA Moscow itapambana na Real Madrid , wakati Zenit St. Petersburg ina miadi na Benfica ya Ureno. Marseille itaonyeshana kazi na Inter Milan.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre / ZR - Kops, Calle / Sekione Kitojo

Mhariri: Othman Miraj