1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich mabingwa mara tano

Sekione Kitojo
22 Mei 2017

Ligi ya Bundesliga imekunja janvi siku ya Jumamosi(20.05.2017),huku kukiwa na vilio na furaha isiyo kifani kwa baadhi ya vilabu. Bayern Munich kwa mara ya tano mfululizo imefanikiwa kulinyakua taji la ligi ya Bundesliga.

https://p.dw.com/p/2dOkr
Bundesliga 34. Spieltag Saisonende - FC Bayern Deutscher Meister
Mabingwa wa Bundesliga Bayern Munich 2017Picha: Getty Images/Bongarts/M. Hangst

Bayern  imetawazwa mabingwa kwa  mara  ya 27. Nahodha  Philipp  Lahm  hata  hivyo anatundika  madaluga  yake  akiwa  mchezaji  wa  kulipwa, akicheza  mchezo  wake  wa  mwisho  akiwa  mchezaji  na nahodha  wa  Bayern  kwa  kuichapa Freiburg  kwa  mabao 4-1.

"Kwa  wengi  ilikuwa  ni urafiki  kwa  miaka mingi.Tumeshuhudia  mengi  kwa  pamoja. Kwa kweli inanisikitisha, kwamba  hayo  yote  yanaondoka. Na kwangu  mimi hilo lilinigusa sana  wakati  nikitoka uwanjani. Huo  ulikuwa  wakati  mgumu sana  kwangu."

Bundesliga Saisonende - Abschied - Philipp Lahm - Meister
Nahodha wa Bayern Munich Philipp LahmPicha: Bongarts/Getty Images

RB Leipzig timu  ambayo  ilitoka  daraja  la  pili  msimu uliopita ,  hakuna  mtu  aliyeipa  nafasi  kwamba  itafikia katika  hatua  ya  kuchukua  nafasi  ya  pili  katika Bundesliga  na  kwamba  itashiriki  msimu  ujao  katika Champions League. Mvutano  hata  hivyo  ulituwama katika  kutafuta  nani atachukua  nafasi  ya  tatu ambayo ni ya  kucheza  moja  kwa  moja  katika  awamu  ya  makundi ya  Champions League kati  ya  Hoffenheim  na makamu bingwa  msimu  uliopita  Borussia  Dortmund. Ilibidi kusubiri  hadi  dakika  za  mwisho  katika  mchezo  huo  wa 34  wa  Bundesliga  kujua  nafi  ananyakua  nafasi  hiyo. Jibu lilipatikana  baada  ya  Borussia  Dortmund kuiangusha  Werder Bremen  kwa  mabao 4-3  katika mchezo  ambao ulikuwa  wa  vuta nikuvute, kama anavyothibitisha  kocha  wa  Dortmund Thomas Tuchel.

Deutschland Borussia Dortmund - Werder Bremen | Thomas Tuchel
Kocha wa Borussia Dortmund Thomas Tuchel na mshambuliaji mahiri Pierre Emerick Aubameyang wakishangiria ushindi wa timu hiyo mwishoni mwa msimu wa 2017Picha: picture alliance/dpa/B. Thissen

"Vijana wanapaswa  kujisikia furaha, na kwa  kweli wamefanikiwa. Wamecheza vizuri  msimu  huu. Naamini kwa  watu wote na klabu  ulikuwa  msimu mzuri na wa aina ya  pekee. Na aina  ya  pekee  huwezi  kuieleza  kwa  jumla katika  mistari miwili  au  mitatu."

FC Koln na  Hertha Berlin zitashiriki  msimu  ujao  katika kombe  la  ligi  ya  Ulaya , ambapo FC Koln wanaingia katika  kinyang'anyiro  cha  Ulaya  kwa  mara  ya  kwanza katika  muda  wa  miaka  24  iliyopita. SC Freiburg inaweza pia  kuingia  katika  kinyang'anyiro  cha  kombe  la  ligi  ya Ulaya  iwapo , Borussia  Dortmund  itaishinda  Eintracht Frankfurt  katika  kombe  la  shirikisho DFB Pokal  tarehe 27  mwezi  huu  mjini  Berlin. Mshindi  wa  kombe  hilo huingia  katika  kombe  la  Champions League, lakini  kwa kuwa  Borussia  tayari  wameshafuzu  kuingia  katika kombe  hilo, ikishinda timu  iliyoshika  nafasi  ya  7  katika ligi inaingia  katika  kombe  la  ligi  ya  Ulaya katika  nafasi ya  mchujo.

Bundesliga 34. Spieltag  - 1. FC Köln vs FSV Mainz 05
Mshambuliaji wa FC Kolon Yuya Osako akipambana na mchezaji wa kati wa Mainz 05 Jean-Philippe GbaminPicha: picture alliance/dpa/J. Güttler

FC Ingolstadt  na  Damstadt zimeaga  ligi  ya  Bundesliga na  msimu  ujao zitashiriki ligi  daraja  la  pili. Lakini  kutoka ligi  daraja  la  pili Stuttgart  pamoja  na  Hannover 99 zinarejea  katika  Bundesliga  msimu  ujao, wakati Wolfsburg  itacheza  michezo  miwili  na  Braunschweig iliyoshika  nafasi  ya  tatu  katika  ligi  daraja  la  pili  ili kuamua  nani  anaingia  katika  ligi ya  Bundesliga msimu ujao.

Bayer Leverkusen  inatarajia  kuwa  na  kocha  mpya  katika muda  wa  wiki  chache  zijazo akichukua  nafasi  ya Tayfun Korkut, amesema  mkurugenzi mtendaji  wa  timu hiyo Michael Schade leo. Korkut  alichukua  nafasi  ya Roger Schmidt mwezi  Machi  lakini  mkataba  wake haukurefushwa  kupindukia  msimu  huu baada  ya Leverkusen  kumaliza ikiwa  ya  12.

Bayer Manager Rudi Völler Portrait
Viongozi wa Bayer Leverkusen Rudi Voeller na Michael Schade(kulia)Picha: picture alliance/augenklick

Mwanamke polisi  mwezi  umri  wa  miaka  38 Bibiana Steinhaus  atakuwa  mwanamke  wa  kwanza  msimu  ujao kuwa  mwamuzi mwanamke  katika  ligi  kubwa  barani Ulaya baada  ya  kupandishwa  kuweza  kusimamia   ligi ya  Bundesliga.

Bibiana Steinhaus Schiedsrichterin
Refa wa Bundesliga Bibiana SteinhausPicha: Imago/Sportfoto Rudel

Steinhaus  amekuwa  mwamuzi  wa  nne kwa  akisimamia  michezo  ya  Bundesliga na  licha  ya kuwa  mwamuzi  wa  shirikisho  la  soka  la  Ujerumani DFB tangu  mwaka  1999, na  anatambua  kwamba  macho yatakuwa  kwake  kila  mara  wakati  atakapokuwa mwamuzi  wa  mchezo mkubwa  katika  Bundesliga.

 

Mwandishi: Sekione  Kitojo

Mhariri: Mohammed Khelef