1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bashir ataka ufufuo wa kisiasa, kiuchumi Sudan

28 Januari 2014

Rais wa Sudan Omar Hassan Al-Bashir ametoa wito wa kuwepo na mwanzo mpya wa kisiasa na kiuchumi katika taifa lake lililoathiriwa na vita, umaskini na machafuko ya kisiasa.

https://p.dw.com/p/1AyDt
Rais Omar Hassan al-Bashir.
Rais Omar Hassan al-Bashir.Picha: Reuters

Huu ndiyo wito wa hivi karibuni kutoka kwa Al-Bashir katika kipindi cha mwaka mmoja uliyopita, wa kufanyika kwa majadiliano mapana ya kisiasa, yakiwahusisha hata waasi wenye silaha nchini humo.

Lakini mara hii rais Al-Bashir alielekeza wito wake moja kwa moja kwa wapinzani, wakiwemo wanachama wa chama chake waliojitenga na kujiunga na vyama vilivyo na uhusiano na serikali, wajumbe wa baraza la mawaziri na wanadiplomasia wa kigeni, katika hotuba aliyoitoa katika ukumbi uliyopo kandoni mwa mto wa Blue Nile.

Maandamano ya kupinga serikali Septemba mwaka 2013.
Maandamano ya kupinga serikali Septemba mwaka 2013.Picha: picture alliance/AP Photo

"Sisi katika chama cha National Congress tunatoa wito kwa Wasudan wote kushiriki katika ufufuo huu. Tunatoa wito wa kufanyika kwa majadiliano mapana ambayo yanavihusisha vyama vyote vya kisiasa na hata waasi wanaotumia silaha," alisema Bashir.

Tukio muhimu

Hotuba ya Al-Bashir, ambayo ilitajwa kuwa tukio muhimu na chama chake, inafuatia mabadiliko katika baraza la mawaziri mwezi Desemba, ambayo wachambuzi walisema yalimuacha rais akiwa na udhibiti thabiti.

Wakosoaji wa utawala wa Al-Bashir wamezidi kupaza sauti tangu serikali ilipopunguza ruzuku kwenye nishati ya mafuta mwezi Septemba, na kusababisha ghasia mbaya zaidi, na kuongeza wasiwasi katika taifa ambalo linapambana pia na waasi katika majimbo ya mipakani kusini na magharibi.

Vyombo vya habari vya Sudan vilichapisha makala kadhaa katika wiki iliyopita kuelekea hotuba hiyo, vikiripoti kuwa maafisa wa serikali walisema ingehusisha mageuzi muhimu.

Hassan al-Turabi ndani ya ukumbi

Kiongozi mwenye msimamo mkali wa dini Hassan al-Turabi, ambaye alipanga mapinduzi ya mwaka 1989 yaliyomleta al-Bashir madarakani, alikuwa miongoni mwa waliokuwepo kusikiliza hotuba ya rais jana Jumatatu, hii ikiwa ndiyo mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 14 kwake kuhudhuria tukio la chama cha NCP.

Al-Turabi alijitenga na chama hicho mwaka 2000 na kuanzisha chama cha upinzani cha Popular Congress. "Hotuba hiyo haikukidhi matarajio yetu. Sikusikia chochote kuhusu uhuru wa wanaharakati wa kisiasa, na wala sikusikia chochote kuhusu uhuru wa vyombo vya habari."

Hassan al-Turabi.
Hassan al-Turabi.Picha: picture-alliance/dpa

Nguzo za muhimu za ufufuo

Wapinzani wengine waliohudhuria katika hotuba hiyo ya Al-Bashir ni pamoja na mwanachama aliekiasi chama cha NCP hivi karibuni Ghazi Salahuddin Sadiq Atabani, mshauri wa zamani wa Bashir alieanzisha chama cha Mageuzi mwezi Desemba, na kiongozi wa chama cha Umma Sadiq al-Mahdi, ambaye aliondolewa kama waziri mkuu katika mapinduzi ya Al-Bashir yasiyokuwa na umuagaji damu.

Rais Bashir hakutoa taarifa zaidi kuhusu mkakati wake wa ufufuo, lakini alisema kuwa laazima ushughulikie mambo makuu manne, ambayo ni amani, uhuru wa kisiasa, kupunguza umaskini na utambulisho wa Sudan.

Al-Bashir, afisa wa zamani wa jeshi, anaetafutwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu ICC kwa uhalifu wa kivita jimboni Darfur, ameitawala Sudan tangu mapinduzi ya mwaka 1989. Aliahidi kuachia ngazi mwaka ujao baada ya uchaguzi wa rais na bunge. Lakini hakuna tarehe iliyopangwa kwa ajili ya chaguzi hizo.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre,afpe
Mhariri: Daniel Gakuba