1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama lalaani mauaji ya Henning

Mohammed Khelef4 Oktoba 2014

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani vidio mpya inayoonesha kundi linalojiita Dola la Kiislamu (IS) likimkata kichwa mateka wa Kiingereza, Alan Henning, likisema mauaji hayo ni 'woga'.

https://p.dw.com/p/1DPf5
Alan Henning akiwa amebeba mtoto kwenye kambi za wakimbizi wa Syria wakati wa uhai wake.
Alan Henning akiwa amebeba mtoto kwenye kambi za wakimbizi wa Syria wakati wa uhai wake.Picha: Henning family handout via the British Foreign and Commonwealth Office/Handout via Reuters

Taarifa iliyosomwa na Balozi wa Argentina kwenye Umoja wa Mataifa na ambaye ndiye rais wa sasa wa Baraza hilo la Usalama, Maria

Cristina Perceval, inasema vidio hiyo "kwa mara nyengine inauelezea ukatili" wa kundi la IS, na inasisitiza kwamba wanachama wa Baraza hilo wanaamini kwamba "matendo kama hayo ya kinyama yanayofanywa na IS hayawatishi bali kuwaimarisha kwenye dhamira yao" ya kuliangamiza hilo.

Rais wa Baraza la Usalama pia lilitaka kuachiliwa kwa haraka na bila ya masharti kwa mateka wengine wanaoshikiliwa na kundi hilo, Al-Nusra Front na makundi mengine yenye mahusiano na mtandao wa al-Qaida.

Jana Ijumaa (3 Oktoba), kundi la IS lilitoa vidio inayoonesha kukatwa kichwa kwa Henning, ambaye ni mfanyakazi wa huduma za kibinaadamu kaskazini magharibi mwa Syria.

Viongozi wa kimataifa walaani

Maafisa wa Marekani wanasema hawana sababu ya kushuku ukweli ya vidio hiyo, ambayo inamuonesha mtu anayezungumza kwa lafudhi safi ya Kiingereza cha Uingereza, akililaumu bunge la Uingereza kwa kifo cha Henning. Hivi karibuni, bunge la Uingereza liliidhinisha ombi la Waziri Mkuu David Cameron kushiriki kampeni ya kijeshi inayoongozwa na Marekani dhidi ya IS.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron.Picha: Reuters/Luke MacGregor

Cameron na Rais Barack Obama wa Marekani wamelaani vikali mauaji hayo ya kikatili, huku Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ametoa wito wa kuimarishwa kwa kampeni ya kimataifa dhidi ya kundi la IS.

Henning anakuwa raia wa nne wa mataifa ya Magharibi kukatwa kichwa na kundi la IS, tangu Marekani kuanza operesheni yake dhidi ya kundi hilo takribani mwezi mmoja sasa, na bado linaaminika kuwa na mateka wengine 10, akiwemo mwandishi wa habari wa Uingereza, John Cantlie, ambaye amekuwa akionekana kwenye vidio nyingi za kundi hilo.

Canada kujiunga na vita dhidi ya IS

Katika hatua nyengine, Canada imekuwa nchi ya karibuni kabisa kutangaza kujiunga na muungano wa kimataifa dhidi ya IS. Kiasi cha wanajeshi 600 wa kikosi cha anga watatumwa eneo la Mashariki ya Kati.

Waziri Mkuu wa Canada, Stephen Herper (kushoto) na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.
Waziri Mkuu wa Canada, Stephen Herper (kushoto) na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.Picha: Reuters

Ikiwa bunge litalipitisha ombi la Waziri Mku Stephen Harper hapo Jumatatu, hii itakuwa operesheni ya kwanza ya Canada nje ya nchi baada ya ile ya Libya mwaka 2011.

Kwa mujibu wa Harper, wabunge watapigia kura operesheni ya "miezi sita dhidi ya ugaidi", ambapo ndege za kijeshi zitatumwa kwenye mipaka ya Iraq, lakini mashambulizi dhidi ya wanamgambo ndani ya Syria yatafanyika tu ikiwa yataungwa mkono na serikali ya Syria.

Chama cha kihafidhina cha Harper kina wingi wa viti bungeni, hivyo ombi hilo ambalo halijumuishi kutumwa kwa wanajeshi wa ardhini, linatazamiwa kupita kirahisi.

Mateka mwengine atishiwa kukatwa kichwa

Wakati hayo yakiendelea, familia ya raia mmoja wa Kimarekani kutokea jimbo la Indiana ambaye ameonekana kwenye vidio iliyotumwa mtandaoni akitishiwa kukatwa kichwa na wanamgambo nchini Syria, inasema mtoto wao alikuwa ameenda eneo la Mashariki ya Kati kwa ajili ya kutoa msaada wa kibinaadamu.

Mripuko kwenye mji wa Kobane ambako kundi la Dola la Kiislamu (IS) linapambana na Wakurdi na vikosi vya kimataifa.
Mripuko kwenye mji wa Kobane ambako kundi la Dola la Kiislamu (IS) linapambana na Wakurdi na vikosi vya kimataifa.Picha: picture-alliance/dpa/S. Suna

Vidio hiyo iliyotolewa jana inamuonesha Peter Kassing mwenye umri wa miaka 26 akiwa amepiga magoti, huku mwanamgambo aliziba uso wake akisema watamuua. Ni vidio ya pili baada ya hiyo, ndiyo inayoonesha kukatwa kichwa kwa Henning.

Wazazi wa Kassig wanasema mtoto wao alisilimu akiwa mikononi mwa watekaji nyara, na amebadilishwa jina na kuitwa Abdul-Rahman. Wanasema kijana wao alipigana vita vya Iraq na kisha akawa daktari wa dharura baada ya kuacha jeshi kwa sababu za kiafya.

Kassig alikwenda Lebanon mwaka 2012 akiwa daktari msaidizi katika hospitali za mpakani na amekuwa akishikiliwa mateka tangu Oktoba mwaka jana.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Sekione Kitojo