1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama lagawika kuhusu Iran

Daniel Gakuba
6 Januari 2018

Iran imeuambia Umoja wa Mataifa inao ushahidi kwamba maandamano ya upinzani yaliyotokea nchini humo yameratibiwa kutoka nje, na Urusi imelitaka Baraza la Usalama kuiacha Iran ishughulikie yenyewe masuala yake ya ndani.

https://p.dw.com/p/2qQdN
USA Treffen UN Sicherheitsrat Vassily Nebenzya und Nikki Haley
Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Vassily Nebenzya na mwenzake wa Marekani Nikki Haley walitofautiana waziwazi kuhusu maandamano ya Ira.Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Altaffer

Iran imeuambia Umoja wa Mataifa kwamba inao ushahidi wa kutosha kwamba maandamano ya upinzani yaliyotokea nchini humo yameratibiwa kutoka nje, na Urusi imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuiacha Iran ishughulikie masuala yake ya ndani. Marekani kwa upande wake imesema Iran isije ikasema haijatahadharishwa.

Hayo yalijiri katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama mjini New York ambacho kiliitishwa na Marekani jana Ijumaa, kujadili wimbi la maandamano ambalo liliitikisa Iran wiki iliyopita. Kikao hicho kilianzia faraghani, lakini baadaye Marekani ilifanikiwa kukifanya cha wazi licha ya upinzani kutoka Urusi, Ufaransa, Bolivia na baadhi ya wanachama wengine.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Nikki Haley alitoa hoja kwamba maandamano hayo ya Iran, kwanza yale ya kuipinga serikali na baadaye yale ya kuinga mkono, yanaweza kuitumbukia nchi hiyo katika mzozo wa vita mithili ya ile ya Syria. ''Uhuru na heshima ya binadamu haviwezi kutenganishwa na amani na usalama'', alisema Bi Haley. Balozi huyo wa Marekani aliitahadharisha Iran, akisema dunia inafuatilia yanayofanyika.

Trump apigia debe waandamanaji wa upinzani

Iran Proteste gegen Regierung in Teheran
Waandamanaji wa upinzani walipinga hali ngumu ya maisha na uongozi wa kidiniPicha: Getty Images/AFP

Rais wa Marekani alijizuia kuhimiza ghasia na vitendo vya fujo kwa waandamanaji wa upinzani nchini Iran, lakini alielezea heshima kwa kile alichokiita ''juhudi za watu wa Iran za kutaka kudhibiti tena serikali yao'' aliyoitaja kuwa ya kifisadi. Hali kadhalika Trump aliahidi msaada wa Marekani kwa waandamanaji hao kwa wakati wowote muafaka.

Gholamali Khoshroo, balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa aliliambia baraza kuwa serikali ya nchi yake inao ushahidi wa dhahiri kwamba maandamano ya kupinga serikali yalikuwa yakiongozwa kutoka nje, na aliishutumu Marekani kutumia vibaya nafasi yake kama mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuitisha kikao hicho cha dharura cha kujadili maandamano nchini Iran.

Urusi na Ufaransa pia zilikuwa zimehoji umuhimu wa kuitisha kikao hicho kwa pupa. Balozi wa Ufaransa Francois Delattre alisema ingawa aligutushwa na ghasia iliyoshuhudiwa katika mitaa ya miji ya Iran, matukio hayo hayakuwa kitisho kwa usalama na utengamano wa kimataifa, hadi yafikishwe mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Onyo kwa wanaotaka kujinufaisha na mzozo wa Iran

Demonstration von Regierungsanhänger im Iran
Maelfu pia walishuka mitaani kuinga mkono serikali ya IranPicha: Tasnim

Delattre alisema, ''Ni lazima tuwe makini sana na wanaoazimia kuutumia mzozo huu kwa maslahi yao binafsi'', na kuongeza kuwa dunia inapaswa kuendelea kufuatilia hali hiyo kwa karibu.

Mtazamo wake uliungwa mkono na mwenzake wa Urusi Vassily Nebenzia, ambaye alisema pamoja na kusikitishwa na vifo vilivyotokea, bado Iran inapaswa kuachwa kushughulikia matatizo yake ya ndani.

Awali naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Rybakov, aliishutumu Marekani kukosa aibu katika kujiingiza katika maandamano ya Iran ambayo alisema ni masuala ya ndani kabisa ya nchi hiyo.

Maandamano hayo ya upinzani nchini Iran yaliyoanzia katika mji wa Mashhad ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini humo, yalisababisha vifo vya watu wasiopungua 21. Mamia wengine waliwekwa kizuizini. Hayo yalikuwa maandamano makubwa zaidi nchini Iran, tangu yale ya mwaka 2009 yaliyofuatia matokeo ya uchaguzi wa rais yaliyoleta utata.

Mwandishi: Daniel Gakuba/msh/dm (AP, AFP, dpa, Reuters)

Mhariri: Zainab Aziz